Unaweza kuwa mtu mmoja tu kati ya watu hawa wawili.

Huwezi kuwa wote wawili, au huwezi kuwa katikati, ni moja tu.

Unaweza kuwa mtu mwema au unaweza kuwa mtu mbaya.

Unaweza kuwa mchapakazi au unaweza kuwa mvivu.

Unaweza kuishi maisha ya furaha na mafanikio au unaweza kuishi maisha ya mateso na kushindwa.

Na uzuri ni kwamba wewe mwenyewe ndiye unayechagua uwe mtu yupi kati ya hao.

Hakuna mtu yeyote anayekuchagulia, hakuna mtu yeyote anayekulazimisha uwe mtu wa aina gani.

Ni wewe mwenyewe, kwa kujua au kutokujua, unachagua uwe mtu yupi kati ya hao.

Kupoteza muda.

Kuna watu wengi wamekuwa wakipoteza muda wakifikiri wanaweza kuwa katikati, au kuwa watu wote wawili.

Yaani mbele za watu uonekane mwema, lakini ukiwa mwenyewe au ukiwa na watu fulani unawafanyia ubaya.

Ukiwa mwenyewe unatega kufanya kazi, lakini mbele za watu unataka uonekane mchapa kazi.

Wewe mwenyewe ndani yako unajua maisha unayoishi siyo ya furaha, lakini nje unajionesha kama ni mtu mwenye furaha na mafanikio.

Huku ni kupoteza muda na kuchagua maisha ambayo mwisho wa siku kila mtu atajua ya kwamba uko upande upi, na mara zote upande utakaojulikana ni ule mbaya.

Amua leo ya kwamba unachagua kuwa mtu mwema, unachagua kujitoa kwenye kile unachofanya na chagua kuwa na maisha ya furaha na mafanikio. Ndio ni njia ngumu kuliko hiyo nyingine, lakini inalipa sana.

SOMA; Kama Utashindwa Kufanya Chochote Utakachojifunza, Basi Fanya Hiki Kimoja Tu, Na Maisha Yako Yatagusa Wengine.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba ni lazima nichague kama nataka kuwa mwema au mbaya, kama nataka kuwa mchapakazi au mvivu na kama nataka kuwa na maisha ya mafanikio au ya kushindwa. Mimi nimeshachagua kuwa mwema, kujitoa kwenye kile ninachofanya na kuishi maisha ya furaha na mafanikio. Haya ndiyo maisha niliyochagua kuishi mimi, na kamwe sitorudi nyuma.

NENO LA LEO.

The good and bad things are what form us as people… change makes us grow.

Kate Winslet

Vitu vizuri na vitu vibaya ndio vinatujenga sisi kama watu… mabadiliko ndiyo yanatufanya sisi kukua.

Amua sasa kuwa mtu mwema, kujitoa kwa kile unachofanya na kuishi maisha ya furaha na mafanikio. Haya yanaanzia ndani yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.