Wote tunajua ya kwamba ili biashara yako ikue zaidi kuna wakati unahitaji kupata fedha zaidi. Na fedha hizi zinaweza kutoka kwako binafsi au kwa watu wengine. Kama wewe binafsi huna fedha za kuweza kuweka kwenye biashara yako kuikuza, basi kuna taasisi zinaweza kukupatia fedha unazohitaji ili kukuza biashara yako. na moja ya taasisi hizo ni benki kupitia mikopo ya kibiashara.
Sasa hivi kila benki inatoa mikopo ya kibiashara. Na upatikanaji wa mikopo umekuwa rahisi siku hizi kuliko hapo zamani. Lakini pamoja na urahisi huu wa kupatikana kwa mikopo bado wengi wanapokwenda kuomba mikopo wanaambiwa hawakopesheki. Hili huwaumiza wengi na kuwarudisha wengi nyuma. Na kwa bahati mbaya sana huwa hawaambiwi kwa nini hawakopesheki, na hata wakiambiwa, bado hawapewi ile sababu halisi.
Leo kupitia kona hii ya mjasiriamali utajifunza jinsi ambavyo benki zinafanya kazi hasa kwenye utoaji wa mikopo ili unapoomba mkopo uombe kwa mtindo ambao benki itakuamini na kukupatia mkopo wako. Kwa sababu tu benki inatoa mkopo haimaanishi kila mtu anaweza kupewa mkopo huo.
Jinsi benki zinavyofanya kazi kupitia mikopo.
Kwanza kabisa ni muhimu wewe kujua ya kwamba benki inafanya biashara kupitia fedha. Na kama ulivyo wewe mfanyabiashara, biashara hii ya benki itaendelea kuwepo kama itaendeshwa vizuri na hakutakuwa na hasara. Kutokana na hii kuwa biashara basi benki zipo makini sana kwa nani wampe mkopo. Benki zinahakikisha mtu anayepewa mkopo ana uwezo wa kurudisha mkopo huo na hata akishindwa kurudisha huo mkopo basi kuna njia wanazoweza kutumia kuhakikisha mkopo wao umerudi. Na hii ndio sababu kubwa benki huwa zinaweka kuwa na mali isiyohamishika kama dhamana ya mkopo moja ya vigezo unavyohitaji ili kupata mkopo.
Benki ni lazima ijiridhishe kwamba wewe una thamani kubwa kuliko fedha unayokopa. Na kupitia thamani hii benki inakuwa na uhakika kwamba fedha wanayotoa itarudi. Ni umakini huu ndio umefanya benki ziendelee kuwepo hadi leo. vinginevyo wangetoa mikopo hovyo, watu wasingerudisha na benki zingekufa.
Zamani ilikuwa thamani pekee unayoweza kuwapa benki ni kuwa na mali isiyohamishika. Lakini kwa sasa unaweza kuonesha thamani tofauti na mali hizo zisizohamishika. Na hii ni muhimu sana kwa wale wanaoanza biashara au wenye biashara ndogo na hawana mali za kuweka kama dhamana ya mkopo. Hapa utajifunza njia mbili muhimu unazoweza kutumia kuonesha benki thamani kubwa uliyonayo kupitia biashara yako.
Njia ya kwanza; anza biashara yako na iendeshe kitaalamu.
Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba wameandika pendekezo la mradi au wana wazo zuri sana la biashara ambalo kama benki ikiwapa fedha watapata faida sana. Lakini kila wakipeleka wazo hilo benki, benki zinashindwa kuwapa mikopo. Kitu kimoja ambacho watu hawa wamekuwa hawaelezi ni kwamba wazo sio kitu kikubwa sana kwenye dunia ya sasa. Kila mtu ana mawazo mazuri sana, tena makubwa, ambayo kwenye makaratasi yanaonekana ni mazuri sana.
Benki haiweki thamani kubwa kwenye wazo, bali inataka kuona kitu kinafanyika. Hivyo kama una wazo zuri, ambalo unajua litaleta faida kubwa, anza kufanya wazo hilo, anza kwa hatua ndogo sana na endesha kwa kitaalamu, kwa maana kwamba unaweza kupima na kuonesha matokeo. Hivyo ukishadhibitisha ya kwamba wazo lako ni zuri, na ukawa tayari una wateja wa kutosha kupitia wazo hilo, ni rahisi kwa benki kukuamini na kukupatia mkopo.
Na ukishaweza kulianza wazo lako kwa hatua hiyo, hata kama benki haitakupa mkopo, ni rahisi kwa taasisi nyingine kukupa msaada zaidi. Watu wanaamini zaidi kitu wanachoona kinafanyika kuliko vitu vilivyoandikwa kwenye makaratasi. Kwa sababu kuandika ni rahisi, ila kutekeleza ni vigumu, na yule aliye tayari kutekeleza kwa ugumu hata akipewa fedha atazitumia vizuri.
Hatua ya pili; jenga urafiki na benki.
Kwa mfano mtu akaja kwako, humjui wala hujui chochote kuhusu yeye na akakuambia nipe mkopo na nakuahidi nitakurudishia, utampa haraka? Lakini je vipi akija rafiki yako ambaye unamfahamu ana biashara yake na kukuambia anahitaji fedha ya kuongeza bidhaa fulani? Huyu itakuwa rahisi kwako kumwamini.
Sasa unahitaji kufanya hili kwenye benki pia, unahitaji kujenga urafiki na benki. Na unawezaje kujenga urafiki huo? Unajenga urafiki kwa kufungua akaunti ya biashara kwenye benki hiyo unayotaka kujenga nayo urafiki. Na kupitia akaunti hii ya biashara, fedha zako zote za kibiashara zipitishe kwenye akaunti hiyo. Kama kuna watu wanaweza waambie wakulipe kupitia benki, mauzo yako peleka benki kama ikiwezekana kila siku, hata kama utakwenda kutoa fedha hizo siku chache baadaye.
Kwa njia hii benki wataona mzunguko wako wa fedha na kujua ya kwamba biashara yako inakwenda vizuri. Na baadaye utakapowafuata na kutaka mkopo, wakiangalia akaunti yako wanaona biashara yako inavyokwenda na inakuwa rahisi zaidi kwao kukuamini kuliko mtu anayekuja kwa mara ya kwanza.
Naamini umeelewa vizuri benki zinafanyaje kazi na jinsi ya kuzitumia kupata mkopo unaohitaji kwenye biashara yako hata kama huna dhamana kubwa. Fanyia kazi mambo hayo mawili, yatakusaidia sana. Kila la kheri.
Rafiki na Kocha wako,