Kwenye makala ya jana ya #BIASHARA_LEO tuliona kauli moja ambayo ukiisikia kwa mteja maana yake mteja huyo unampoteza.
Kama hukusoma makala ile bonyeza maandishi haya kuisoma kwanza kabla hujaendelea.
Kwenye makala hiyo tumekubaliana usikubali kupokea kauli hii ya mteja. Sasa leo tutaangalia ufanye nini pale mteja anapokupa kauli kwamba nikiwa tayari nitakwambia..
1. Mwulize ni kipi kinamzuia kufanya maamuzi sasa.
Mteja anapokwambia kwamba akiwa tayari atakuja kununua, usikubali tu kirahisi, badala yake muulize vizuri tu ni kwa nini anashindwa kufanya maamuzi ya kununua sasa. Kama ana sababu ya kweli ataitoa, na kama hana sababu ya kweli utaona kutoka kwenye maelezo yake.
2. Jiandae kumsaidia sababu anazotoa.
Utakapomwuliza mteja kwa nini anashindwa kununua sasa na akakupa sababu ya msingi basi msaidia kwenye sababu hiyo. Labda sababu yake inaweza kuwa hawezi kumudu gharama hiyo kwa sasa. Hapa msaidie kufikiri jinsi anavyoweza kuimudu. Au sababu yake inaweza kuwa kukosa uhakika kama itamfaa kweli, hapa unaweza kumpa uhaki na dhamana pia kwamba ikitokea haijamfaa anaweza kurudi.
3. Mwulize umkumbushe lini.
Kama mteja atakupa sababu ya msingi ya kushindwa kununua sasa, na ukaona ya kweli hawezi kufanya hivyo sasa, mwulize umkumbushe lini. Mwombe akupe tarehe kabisa na mawasiliano yake ili itakapofika umkumbushe. Jinsi atakavyokujibu na kuonesha ushirikiano kwenye hili utapata picha kama kweli atarudi kununua.
Wewe kama mfanyabiashara ni muhimu uweze kuwaelewa wateja wako vizuri na kuhakikisha unawasaidia kupata kile ambacho kitawasaidia.
Msikilize mteja vizuri kwa maneno anayosema, jinsi anavyoyasema na hata matendo yake ya mwili.
Kila la kheri.
Ni kitu gani cha biashara ungependa tukiandikie hapa kwa ufupi? Tafadhali weka maoni yako hapo chini.