Siku Ya Usafi Kitaifa; Usafi Muhimu Sana Kwako Kufanya Kwenye Maisha Yako Ili Kufikia Mafanikio Makubwa.

Tarehe tarehe tisa ya mwezi wa kumi na mbili ni siku muhimu sana kwa taifa letu la Tanzania, hii ni siku ambayo tunakumbuka nchi yetu kupata uhuru kutoka kwenye ukoloni. Hii ni siku ambapo sisi kama taifa tulipata nafasi ya kufanya maamuzi yetu wenyewe. Ni siku muhimu sana kuikumbuka, na kila mwaka tumekuwa tukifanya maazimisho ya kukumbuka tukio hili kubwa.
Mwaka huu 2016 siku hii imeongezwa umuhimu zaidi na raisi wetu mpya Dkt John Pombe Magufuli kwa kutangaza kwamba hakutakuwa na maadhimisho ya sherehe kwa siku hii ya leo. badala yake, wananchi wote nchi nzima tushiriki kwenye shughuli za usafi kwenye maeneo yetu tunayoishi na kufanya kazi.

JIANDAE KUFANYA USAFI MUHIMU SANA KWENYE MAISHA YAKO.

 
Wote tunajua usafi ni muhimu sana kwenye maisha yetu hasa kwa afya. Na kwa hizi nchi zetu zinazoendelea, uchafu ndio unachangia sana magonjwa mengi ambayo yanalipa taifa gharama kubwa kwenye kuwatibu watu na hata kupoteza nguvukazi. Ugonjwa kama kipindupindu ambao kwa siku za karibuni umekuwa tishio, ni ugonjwa unaotokana moja kwa moja na uchafu, hakuna njia nyingine, ni uchafu. Na hata ugonjwa kama malaria, kwa sehemu kubwa uchafu wa mazingira unachangia ugonjwa huu kuendelea kuwa tishio.
Hivyo ni muhimu sana kufanya usafi wa mazingira yetu yanayotuzunguka. Tumpongeze mheshimiwa raisi kwa hili.
Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa usafi wa mazingira, kuna usafi muhimu sana ambao wewe unahitaji kuufanya kwenye maisha yako. huu ni usafi ambao huenda hujawahi kuufanya na umekuwa kikwazo kikubwa kwako kufanikiwa. Kwa kutofanya usafi huu kumefanya juhudi zote unazoweka zipotee bila ya kuona mafanikio uliyotarajia.
Kwa siku hii muhimu sana ya usafi kitaifa, nitakuomba wewe kama rafiki yangu, ufanye usafi huu. Ifanye siku hii kuwa ya kumbukumbu kwako kwa kufanya usafi huu ambao sio tu utakuwezesha kufikia mafanikio makubwa, bali pia utakupatia uhuru mkubwa sana.
Na hivyo kila mwaka tarehe 09/12 utakuwa ukisherekea msingi wa mafanikio yako, na kupatikana kwa uhuru wa maisha yako, pamoja na uhuru wa nchi.
Je upo tayari kufanya usafi muhimu sana kwenye maisha yako ambao utakuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa? Kama ndio karibu na tuangalie usafi huu muhimu sana.
Ila kabla hatujaangalia usafi huu muhimu, napenda kujua kama ulifanya ule uchaguzi muhimu sana kwenye maisha yako. wakati tunakwenda kufanya uchaguzi mkuu wa nchi yetu, nilikushauri ufanye uchaguzi mmoja muhimu sana kabla hujaenda kupiga kura. Je uliufanya? Maana kama hukuufanya basi usafi huu wa leo utakuwa mgumu kwako. Soma tena kuhusu uchaguzi ule muhimu sana kwako hapa; Huu Ndio Uchaguzi Mkuu Muhimu Kwenye Maisha yako
Naamini sasa umeshafanya uchaguzi mkuu muhimu sana kwako, na hivyo karibu kwenye usafi muhimu sana unaohitaji kufanya ili kufanikiwa.
Usafi muhimu sana kwako kufanya ili uweze kufikia mafanikio makubwa ni kusafisha maisha yako. ndio unahitaji sana kusafisha maisha yako kama kweli unataka kusonga mbele na kufanikiwa. Na ninaposema kusafisha maisha yako simaanishi kuoga au kufua nguo zako, huko ni kusafisha mwili wako, ninachosema hapa ni wewe usafishe maisha yako, maana hili ni eneo muhimu sana kwako. Huwezi kufikia mafanikio makubwa kama hutafanya usafi mkubwa kwenye maisha yako. na leo una nafasi nzuri sana ya kufanya usafi huu.
Je unawezaje kusafisha maisha yako? hapa ninakushirikisha maeneo matano muhimu sana ya kusafisha leo ili uwe na maisha bora, yenye furaha na yatakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa.
1. Safisha mahusiano yako.
Mahusiano ni eneo muhimu sana ambalo linaweza kukupeleka mbele au kukurudisha nyuma. Watu wengi tumekuwa na mahusiano ambayo hayana mchango wowote kwetu katika kuwa na maisha bora na kufikia mafanikio makubwa.
Leo hii fanya usafi mkubwa kwenye mahusiano uliyonayo sasa. Angalia wale watu ambao ni wa karibu kwako, marafiki zako na hata ndugu na jamaa zako. Ni wapi ambao wamekuwa wanakuunga mkono kwenye harakati zako za kuwa na maisha bora. Na pia angalia ni wapi ambao wamekuwa wanakurudisha nyuma, ambao wamekuwa wanakukatisha tamaa kwenye kila jambo kubwa unalotaka kujaribu.
Pia angalia ni marafiki wapi ambao wanakuzuia wewe kujijengea tabia za mafanikio, wale ambao wanakutafuta ukiwa na fedha mkatumie ila ukiwa huna huwaoni?
Leo ndio siku pekee ya kumaliza mahusiano yote ambayo hayana mchango kwako. Na sio lazima ugombane na watu hawa, bali punguza muda unaokuwa nao, na jenga zaidi yale mahusiano yanayokupeleka mbele zaidi.
2. Fanya usafi wa vipaji vyako.
Ulipokuwa mtoto ulikuwa na vipaji vingi sana, na kuna vitu vizuri ambavyo ulikuwa unapendelea kufanya. Lakini utu uzima ulipokuja na majukumu yakawa makubwa, umejikuta unamezwa na majukumu yako na hivyo kusahau kabisa vipaji vyako. Huenda kazi au biashara unayoifanya imekumeza kabisa na umesahau kabisa ni vitu gani ambavyo umekuwa unapendelea kufanya.
Siku hii nzuri ya leo fanya usafi kwenye eneo hili, jikumbushe ni vitu gani ulikuwa unapendelea sana kufanya, na anza kufikiri ni jinsi gani unaweza kuanza kufanya tena, hata kwa ngazi ya chini sana.
Pia fikiria ni namna gani unaweza kuwasaidia wengine kwa kile unachopenda kufanya na wao wakakulipa. Kwa njia hii unaweza kutengeneza kipato cha ziada na hatimaye kugeuza hii kuwa chanzo chako kikuu cha kipato baadae, hasa kama kazi au biashara unayofanya sasa huifurahii sana.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.
3. Fanya usafi wa kifedha.
Eneo jingine muhimu sana kufanya usafi kwa siku ya leo ni hali yako ya kifedha. Najua tunapofika kwenye fedha watu wengi huwa hawajisikii vizuri. Kwa sababu walichoamua kufanya ni kuziba akili zao zisijihusishe kabisa na fedha, wao wanachojua ni kufanya kazi, kupata fedha, kutumia mpaka iishe, kufanya tena kazi, kupata fedha, kutumia mpaka iishe, kukopa, kupata fedha, kulipa kidogo mkopo, kukopa tena zaidi. Na baada ya muda wanajikuta kwenye deni kubwa, kipato kidogo na matumizi makubwa sana.
Sasa leo fanya usafi kwenye eneo hili. Anza na kipato chako, je kinakutosheleza? Kama hapana fikiria ni njia zipi unazoweza kutumia ili kukiongeza. Baada ya kumaliza kipato njoo kwenye matumizi, je matumizi yote unayofanya ni muhimu kwako? Yapitie matumizi yako na angalia ni yapi ambayo sio muhimu na yafute kabisa. Kama kitu kisipokuwepo hutakufa, basi sio muhimu na kikate leo.
Baada ya kuangalia kipato na matumizi, sasa geukia sehemu moja muhimu sana ambayo ni madeni. Kwanza jua una madeni kiasi gani, na jua kabisa ya kwamba hayo madeni ni lazima uyalipe, huwezi kukwepa hilo. Angalia madeni hayo na weka mpango wa kuyalipa yote, na hakikisha unafanyia kazi mpango huo. Na wakati huu ambapo unalipa madeni, usiendelee tena kukopa.
4. Fanya usafi wa akili yako.
Kama kuna eneo ambalo umelisahau kulifanyia usafi kwenye maisha yako, basi ni akili yako. umekuwa unaruhusu kila mtu atupe uchafu kwenye akili yako. umeruhusu magugu yaote kwenye kitu hiki cha thamani sana kwako. Na umeamua kuweka akili yako kwenye boksi, huitumii kama ambavyo ungepaswa kuitumia.
Anza usafi huu kwa kuondoa mambo yote ambayo ni hasi, maana haya ndio yanakuletea hofu kubwa kwenye amisha yako na kukufanya ushindwe kuchukua hatua. Ondokana na mawazo yote hasi na yanayokukatisha tamaa. Na pia epuka vile vitu ambavyo vinakuletea mawazo hasi, na kitu namba moja ni kufuatilia habari, hasa za udaku, acha mara moja.
Ng’oa magugu yote ambayo yameota kwenye akili yako. kumbuka kwamba akili yako ina uwezo mkubwa sana, lakini isipotumiwa basi nayo hupoteza uwezo ule, ila inapoanza kutumiwa tena uwezo mkubwa unarudi. Anza kuhoji mambo, anza kujihoji mwenyewe, usifanye tu vitu kwa mazoea, bali fanya ukijua kwa nini unafanya na ungewezaje kuboresha zaidi.
Ondoa akili yako kwenye boksi ulipoiweka, ambapo umekuwa unafanya mambo kwa kuiga wengine wanachofanya, na anza kufanya mambo kwa sababu unajua ni muhimu sana kwako na sio kufanya kwa sababu wengine wanafanya au ili kuwafurahisha wengine.
SOMA; Mambo Nane(8) Yatakayokufanya Uwe Na Fikra Chanya Kila Wakati Ili Uweze Kufikia Mafanikio.
5. Fanya usafi kwenye ratiba zako na matumizi yako ya muda.
Muda! Hakuna eneo ambalo ni chafu kwenye maisha yako kama hilo. Umekuwa unapoteza muda wako mwingi sana, ambapo kama ungeweza kuutumia vizuri, hakika ungefanya mambo makubwa sana. Yale mambo yote ambayo unasema ungepeta muda ungeyafanya, unaweza kuyafanya yote kama utafanya usafi kwenye muda wako.
Anza usafi huu wa muda kwa kuangalia ni jinsi gani unatumia muda wako. Je unatumia muda wako kwa mambo ambayo ni muhimu kwako? Au umekuwa unaacha tu muda unapotea bila ya kujua ni kipi kikubwa umefanya. Kama unashindwa kwenye mitandao ya kijamii siku nzima, ukiangalia kila kitu na kuona ya kwamba ukiondoka unapitwa basi unapoteza muda mwingi sana. Kama upo kwenye makundi ya wasap zaidi ya kumi, na kote upo hai kuchangia kila kitu kinachowekwa, hata kama sio muhimu sana kwako, unapoteza muda mwingi sana.
Fanya usafi leo kwa kutenga muda maalumu wa kufanya kazi ambazo ni muhimu kwako, na muda maalumu wa kupumzika ambao ndio unaweza kutembelea mitandao ya kijamii. Na muda huu usiwe mrefu sana kwako. Hesabu kila saa yako ya siku unaitumiaje, na njia bora ya kufanya hivyo ni kuweka thamani kwenye muda wako. Soma hapa kujua jinsi ya kuweka thamani hiyo; UNAJUA THAMANI YA MUDA WAKO?
Huu ndio usafi muhimu sana kufanya kwenye maisha yako kwa siku hii nzuri ya leo. kama umeweza kusoma mpaka hapa, kwanza nikupe hongera na anza kufanya usafi huo muhimu. Na kama utakwama popote kwenye kufanya usafi huu, basi tuwasiliane ili tuweze kusaidiana zaidi.
Nakutakia kila la kheri kwenye kufanya usafi huu muhimu, tafadhali sana, usikubali siku ya leo ipite kabla hujafanya usafi huu muhimu. Tenga muda mchache leo hii ili ufanye usafi huu. Na kama unaona huna muda, basi anza kwa kusafisha muda wako, na nina hakika ukiusafisha, ni lazima utapata saa moja ya ziada. Kama unashindwa kupata tuwasiliane nikuoneshe unavyoweza kupata saa moja ya ziada kwenye muda wako kuanzia leo hii.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
0717 396 253

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: