Ili kufikia mafanikio makuba kwenye maisha yako, kupitia kazi au biashara unayofanya, kitu kimoja muhimu sana unahitaji, nacho ni kujenga himaya.
Ni lazima ujenge himaya kubwa ya watu ambao wanategemea sana kile ambacho unakifanya. Watu ambao wanasubiri kwa hamu kupata huduma au bidhaa yako. watu ambao wanajali kweli kwenye kile ambacho unakifanya.
Tumekuwa tunaona wengine wanajenga himaya zao, wanajenga biashara kubwa ambazo watu wanazizungumzia sana, wanafanya kazi bora ambayo inawafurahisha wengi. Je wewe umeshaanza kujenga himaya yako?
Na unawezaje kujenge himaya hii?
1. Kwa kuwahudumia watu, kuwasaidia watu kutatua matatizo yao, kuwapatia kile ambacho ni muhimu zaidi kwao.
2. Kwa kujali kuhusu watu wale unaowahudumia, kuhakikisha kwamba kwa kukutana na wewe maisha yao yanakuwa bora sana.
3. Kwa kuwasaidia wengine kuweza kujenga himaya zao pia. Kumbuka unachotoa ndio unachopokea.
4. Kwa kuona tayari ile himaya unayotaka kuijenga ipo ndani yako, ipo mikononi mwako na jukumu lako ni kutekeleza.
Ndio unaweza kujenga himaya kubwa ambayo itakuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa. Sio kazi rahisi, ndio maana wachache sana ndio wanaoweza. Na wewe ni mmoja wao, unaweza, anza sasa.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Biashara Kubwa Kwa Kuanzia Chini Kabisa, Hata Kama Huna Kitu.
TAMKO LANGU;
Nahitaji kujenga himaya ambayo itaniwezesha kufikia mafanikio makubwa. Na nitaijenga himaya hii kwa kutoa huduma bora sana kwa wengine, kuwajali, kuwasaidia wengine kujenga himaya zao na kuona tayari nipo kwenye himaya ninayotaka kuijenga. Nimejitoa kweli kujenga himaya na hakuna cha kunirudisha nyuma kwenye hili.
NENO LA LEO.
Passion gets an entrepreneur through the startup days and the enormous efforts it takes to build a business.
Peter Diamandis
Shauku inamsukuma mjasiriamali siku za mwanzo za biashara. Inahitaji juhudi kubwa sana kuweza kujenga biashara kubwa.
Sio kitu rahisi kujenga biashara kubwa, unahitaji kuweka juhudi kubwa sana, na kutokukata tamaa. Wachache wanaweza hili, na wewe ni mmoja wao.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.