Njia moja ya uhakika ya kuwa na maisha bora ni kuyaelewa maisha kwanza. Bila ya kufanya hivyo utateseka sana na maisha haya.
Bila ya kuelewa maisha kila mara utasema kwa nini haya yananitokea tu mimi.
Bila ya kuelewa maisha kila mara utaona maisha ya wengine ni bora kuliko yako.
Bila ya kuelewa maisha kila siku utajikuta unakimbizana nayo kama mtu anayekimbiza upepo.
Yaelewe maisha na kila linalotokea utalipokea vyema na kuweza kulitumia vizuri.
Ni yapi muhimu ya kuelewa kwenye maisha yako?
1. Maisha yoyote yana changamoto, hakuna maisha ambayo hayana changamoto, hata raisi wa nchi pamoja na kuwa na nafasi kubwa, bado maisha yake yana changamoto kubwa.
2. Kwenye maisha yako unapitia vipindi mbalimbali, maisha hayo ni kama zile bembea za watoto. Kuna kipindi unajiona uko juu kabisa kileleni, kila kitu kinakwenda kama ulivyopanga na mambo ni mazuri. Kuna kipindi unajiona uko chini kabisa, kila unalojaribu linashindikana na unaona kama ndio mwisho.
3. Changamoto za maisha ndio zinafanya maisha yawe bora. Hivyo unapozipokea na kuzitatua unajijengea uwezo mkubwa sana.
4. Unapokuwa juu tumia vizuri nafasi hiyo na unapokuwa chini jua ni kipindi tu na elewa vizuri pale ulipo na anza mpango wa kwenda juu.
5. Usijaribu kushindana na maisha, yaelewe, kuna mambo unaweza kuathiri na kubadili na kuna mengine yako nje ya uwezo wako. Elewa yale ambayo yapo ndani ya uwezo wako na jitoe kuyafanyia kazi. Na yajue yale ambayo yako nje ya uwezo wako na yapokee ili maisha yaendelee. Kujitesa kwa mambo ambayo yako nje ya uwezo wako, hata kama wewe ndio uliyasababisha yatokee hakutakusaidia kwa njia yoyote ile.
Chagua kuyaelewa maisha, ili uweze kuyaishi vizuri.
SOMA; Kuwa Na Maisha Bora Kunaanza Na Wewe Kuweza Kusimama Mwenyewe Na Unaweza Kusimama Hivi….
TAMKO LANGU;
Nimechagua kuyaelewa maisha, najua kwa kufanya hivi nitakuwa na maisha bora zaidi. Kila siku nitaendelea kujifunza kupitia maisha yangu. Nitafanyia kazi vile ambavyo vipo ndani ya uwezo wangu, na nitapokea na kukubali vile ambavyo viko nje ya uwezo wangu. Kuanzia sasa naacha kabisa kushindana na maisha.
NENO LA LEO.
We must accept life for what it actually is – a challenge to our quality without which we should never know of what stuff we are made, or grow to our full stature.
Robert Louis Stevenson
Ni lazima tuyakubali maisha kwa vile yalivyo, changamoto ambayo bila hii hatuwezi kujijua vizuri, au kukua kufikia uwezo wetu.
Yaelewe maisha yako na yakubali, kwa njia hii utakuwa na maisha bora sana.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.