Unajua ili ufanikiwe ni lazima uweze kufanya mambo makubwa, ambayo hujawahi kuyafanya kwenye maisha yako. kwa sababu ukiendelea kufanya kile ambacho unafanya, utaendelea kupata matokeo ambayo unayapata sasa.

Lakini unapofanya mambo haya makubwa na mageni kwako, mara nyingi unakuwa huna uhakika na matokeo unayotaka kupata. Hujui kama kweli utapata kile unachotazamia kupata. Tofauti na kufanya kile ulichozoea kufanya, ambapo kwa asilimia kubwa una uhakika na matokeo.

Hivyo basi unapofanya jambo jipya na kubwa, unaweza kuweka akili yako kwenye moja ya maeneo haya mawili;

1. Unaweza kufikiria sana kuhusu yale matokeo ambayo unataka kuyapata, na hivyo kupata hamasa ya kuendelea zaidi, japo ni wachache sana wanaofanya hivi.

2. Unaweza kufikiria sana kuhusu kile usichokijua, kile ambacho huna uhakika nacho, na hii inakukatisha tamaa kuendelea. Na hapa ndipo watu wengi wanapokuwepo.

Unaweza kufikiria yale matokeo unayotaka kupata au unaweza kufikiria kile usichokijua ambacho kinaweza kutokea.

Kufikiria usichokujua, hakuna msaada wowote kwako, zaidi ya kukuogopesha na kufanya uone mambo ni magumu sana.

Kufikiria yale matokeo makubwa unayotegemea kupata, kunakufanya uone inawezekana na hivyo kuweka juhudi zaidi.

Muda wote ifanye akili yako ifikirie zaidi kile ambacho unategemea kupata na sio kile ambacho unahofia.

SOMA; Haya Ndio Mambo Matatu Yatakayokuletea Matokeo Ya Kushangaza.

TAMKO LANGU;

Najua ninapofanya jambo kubwa la mafanikio, kuna majibu ninayotegemea na kuna hofu ya kile nisichojua. Najua navutiwa sana kufikiria kuhusu hofu, lakini hili halina msaada kwangu. Kuanzia leo nitakuwa nafikiria kuhusu yale matokeo makubwa ninayotegemea kupata. Pale mawazo ya hofu yanaponijia nitajikumbusha yale matokeo makubwa ninayotegemea kupata na njia ninazopita ili kuyapata. Kwa njia hii nina uhakika wa kufikia mafanikio makubwa.

NENO LA LEO.

“Whenever you want to achieve something, keep your eyes open, concentrate and make sure you know exactly what it is you want. No one can hit their target with their eyes closed.”
― Paulo Coelho

Pale unapohitaji kupata matokeo fulani, fungua macho yako na weka hakikisha unajua kwa hakika ni kitu gani hasa unataka. Hakuna mtu anayeweza kulenga kitu akiwa amefunga macho.

Fikiria zaidi kile unachokitaka na sio hofu ya kile usichokijua.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.