Kitabu speak like ceo kimeandikwa na mwandishi Suzanne Bates, hiki ni kitabu ambacho kinatoa mbinu za mawasiliano bora kwa viongozi. Wote tunajua ya kwamba uongozi ni mawasiliano, na mafanikio yoyote ya mtu, yanatokana na jinsi gani anavyoweza kuwasiliana na kushirikiana na watu wengine.
Kama unataka kuwa kiongozi mkubwa na mwenye mafanikio kwenye kazi au biashara ambayo unaifanya, basi huna budi kufanyia kazi mawasiliano yako. maana hiki ndio kitu kimoja ambacho kinaweza kukuinua, kama utakifanyia kazi vizuri au kuweza kukuangusha, kama hutakifanyia kazi vizuri.
Kitabu hiki ni cha kusomwa na kila ambaye anataka kufikia mafanikio makubwa kama kiongozi. Hapa nakushirikisha yale mambo 20 muhimu niliyojifunza kwenye kitabu hiki. Karibu tujifunze kwa pamoja;
1. Watu wanaofanikiwa na kufika ngazi za juu sio wale wenye akili sana, bali wale wanaoweza kuwasiliana vyema. Kujifunza mbinu bora za mawasiliano kunakufungulia milango ya fursa nyingi ambazo watu wengi hawapati nafasi hiyo. Na mawasiliano haya ni ya pande zote mbili, kutoa na kupokea. Hivyo kama unataka kufika juu zaidi, ni lazima ujue ya kwamba mawasiliano ni kitu muhimu kufanyia kazi.
2. Viongozi wenye mbinu bora za mawasiliano wanafanikiwa zaidi kwa sababu wanaweza kuwashirikisha wengine maono yao, kuwapa hekima zao na hata kuweza kuwahamasisha watu kuchukua hatua fulani. Ushawishi wako kwa wengine ni kitu muhimu sana, iwe umeajiriwa au unafanya biashara. Kadiri unavyoweza kuwashawishi wengine wakakuunga mkono kwa ridhaa yao wenyewe, ndivyo unavyoweza kufanikiwa zaidi. Kumbuka kiongozi anashawishi watu wamfuate kwa ridhaa yao wenyewe, wakati mabosi au mameneja wanalazimisha watu wawafate kwa amri. Kama unataka kufanikiwa, weza kushawishi watu, na utaweza hivi kama uko vizuri kwenye mawasiliano.
3. Hatua ya kwanza kabisa kwa kiongozi kufanikiwa kupitia mawasiliano, ni kuwa yeye. Ndio hakuna kiongozi anayefanikiwa kwa kuiga wengine, kwa kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Kiongozi anahitaji kuwa yeye kwanza, kujua ni kipi anasimamia na kukisimamia kweli. Kwa njia hii watu wanakuwa na imani naye na wanashawishika kuwa pamoja naye. Unahitaji kuwa wewe, kuwa halisi na kuonesha hilo kwenye kila unachofanya, na kwa njia hii watu watakusikiliza na kukufuata.
4. Unapokuwa kiongozi wewe ndio ujumbe na ujumbe ni wewe. Kuonekana kwako tu tayari ni ujumbe tosha. Ndio maana unahitaji kuweza kuwasiliana vizuri sana. Kwa sababu wewe kama kiongozi umebeba maono ambayo unataka wengine wayakubali na kuyafanyia kazi. Kwa maono hayo watu wanaweza kuyapokea na kujitoa kuyafanyia kazi au wakayapinga kabisa. Yote hii inategemea na jinsi unavyowasiliana na watu hao.
5. Unapoongea na watu, waambie kile unachoamini kinawezekana. Maono yako, matumaini yako, na imani yako kwa siku za mbeleni juu ya taasisi ambayo upo. Zungumzia yale yajayo vyema na watu watapata nguvu ya kuyafanyia kazi. Lakini ikawa wewe kama kiongozi huna uhakika, utazidi kuwachanganya wale wanaokufuata na kukosa imani kwako.
6. Wewe kama kiongozi kumbuka pia ni binadamu. Na kila binadamu anapitia magumu na pia anafanya makosa. Wafanye wale unaowaongoza wakuone wewe kama binadamu, na kwa njia hii watakuwa na wewe karibu zaidi. Ongea nao kwa kuwashirikisha safari ya maisha yako, changamoto unazopitia na makosa unayofanya, kwa njia hii watu watakuwa pamoja na wewe na watakusaidia kufanikiwa zaidi.
7. Kazi ya wewe kuwa kiongozi bora sio rahisi, kazi ya wewe kuwa na mawasiliano bora sio rahisi, ina changamoto zake na hivyo jiandae vyema. Jitoe kufanyia kazi kila siku kuhusu mawasiliano na kadiri siku zinavyokwenda utazidi kuwa bora. Kufanya mawasiliano ya mara kwa mara ni njia bora ya wewe kuboresha mawasiliano yako. usiseme umetingwa sana kufanya mawasiliano, bali hakikisha mawasiliano ni sehemu ya siku yako.
8. Moja ya njia za kuwa na mawasiliano bora ni kutoa hadithi. Unapopata nafasi ya kuzungumza na watu, kwanza tafuta hadithi inayoendana na kile unachokwenda kuzungumza nao. Watu wanapenda sana hadithi, na hivyo kuwaeleza hadithi nzuri kutawafanya wapokee vizuri kile unachowaambia. Na kumbuka kuhadithiana ni asili ya binadamu, tangu zamani watu wamekuwa wakipeana hadithi na kujifunza sana kupitia hadithi hizo. Kuwa mtu wa hadithi na watu watapenda kukusikiliza, na kuchukua hatua pia.
9. Unapozungumza, zungumza kile kweli ambacho unakiamini na unaweza kukisimamia. Hata kama una msukumo kiasi gani, usijaribu kudanganya au kupindisha ukweli, au kusema kitu ambacho huamini ili mradi tu kuwaridhisha wengine. Ukiwa mtu wa aina hii watu watakugundua na hawataweza kukuamini tena. Sema kile unachokiamini hata kama hakiwapendezi wengi, na wale wanaokuelewa watakuamini zaidi na zaidi. Unapowadanganya watu mara moja, huanza kujiuliza kama yale yote waliyokuwa wanaamini kuhusu wewe zamani ni kweli au pia ulikuwa unadanganya. Usiingie kwenye mtego huo, sema ukweli mara zote.
10. Ili kuweza kuwa na mawasiliano bora, kujiandaa ndio msingi wenyewe. Unahitaji kujiandaa, halafu ujiandae na ujiandae tena. Kama unakwenda kutoa hotuba, hakikisha unaisoma hotuba hiyo ukiwa peke yako, irudie mara nyingi uwezavyo. Kama unakwenda kufanya presentation ya kitu, fanya mazoezi mengi kama ndio unawasilisha kitu kile, rudia mara nyingi mpaka uone umeelewa kila hatua ya kile unachokwenda kuongea mbele ya wengine. Usichukulie ni kazi rahisi, maana unavyozungumza mbele ya watu ndio fursa kubwa ya wewe kwenda mbele zaidi. Itumie vizuri kwa kutoa kilicho bora.
11. Unapojiandaa kwenda kuongea mbele ya watu, andaa mazungumzo yako kwa mtiririko huu.
Kwanza; kuwa na wazo kuu ambalo unakwenda kuzungumza mbele ya watu hao. Ni kitu gani ambacho unataka mtu aondoke nacho kwenye mazungumzo hayo.
Pili; andaa pointi tatu za kutetea au kuelezea wazo lako kuu. Hapa ndipo unapowashawishi watu kwa nini wakubaliane na wazo hilo au kwa nini wachukue hatua.
Tatu; jiandae kwa swali ambalo mtu anaweza kuuliza kutokana na mazungumzo yako. fikiria maswali ambayo yanaweza kuulizwa na jiandae kwa majibu.
Nne; hadithi inayoendana na mazungumzo yako, ambayo itawavutia watu na kuwafanya waelewe vizuri kile unachokwenda kuzungumza.
Tano; andaa vielelezo muhimu kama picha, takwimu, na kadhalika. Kwa kujiandaa hivi mazungumzo yako yatakuwa bora sana.
12. Muonekano wako mbele ya watu ni kielelezo tosha. Kabla hata hujafungua mdomo wako kuongea, watu tayari wameshajua ni mtu wa aina gani. Jinsi unavyosimama, jinsi unavyotembea, na jinsi ulivyovaa inatosha kupeleka ujumbe kwa watu kuhusu wewe. Hivyo kuwa makini sana na mwonekano wako mbele ya wengine, kama unataka kuwa na mawasiliano bora.
13. Unaposimama mbele ya watu kwa ajili ya kuongea, jiamini na miliki jukwaa. Usitembee tembee sana maana hii inaonesha kwamba una hofu. Usiongee haraka sana wala taratibu sana. Unahitaji kuonekana kwamba una kitu muhimu cha kusema na upo tayari kukisema. Kadiri unavyojiamini mbele za watu na wao ndivyo wanavyokuamini na kuamini kile unachowaambia.
14. Chagua maneno yako vizuri. Kwa ujumbe mmoja unaweza kuwa na mapokeo tofauti kama utachagua maneno tofauti ya kutumia. Tumia muda wako kuchagua maneno mazuri ambayo yatafikisha ujumbe kwa watu ambao utawahamasisha kuchukua hatua. Hata kama unawapa habari mbaya, basi chagua maneno ambayo hayatawavunja watu moyo moja kwa moja. Hii ni mbinu muhimu sana ya mawasiliano na yenye ushawishi mkubwa.
15. Unapokuwa kwenye kipindi cha maswali na majibu, yaani wewe kama kiongozi unaulizwa maswali na watu kwenye kikao au na waandishi wa habari, basi tumia sheria hizi nne za maswali na majibu.
Kwanza; kuwa mtulivu, hata kama swali lililoulizwa ni la kukuumiza au kukukashifu, tulia, usioneshe kupaniki.
Pili; kuwa mwaminifu, sema ukweli hata kama sio kitu ambacho watu wanafurahia. Unaposema ukweli huhitaji kukumbika mara kwa mara ili kuendelea kuficha, na kazi yako itakuwa rahisi.
Tatu; kuwa unapatikana, inabidi iwe rahisi kwa watu kukifikia na kukuuliza maswali ambayo yanawatatiza.
Nne; kuwa na akili huru, usifikirie tu ya kwamba mtu anakuuliza swali ili kukukomoa, badala yake fikiria kwa kina zaidi, ni nini hasa kinachoendelea, au swali hilo limebeba fursa gani. Kwa hatua hizi nne utaweza kujibu maswali vizuri na kuwa na mawasiliano bora.
16. Unapoulizwa swali kamwe usiseme huna maoni, yaani NO COMMENT, kwa kiongozi kutoa kauli kama hiyo ni kuwaonesha watu kwamba hujali. Ni bora kusema kwamba huwezi kuzungumzia jambo hilo kutokana na sababu fulani, ambazo utawaambia kwa ufupi. Pia usitake kudanganya ili tu kuondokana na swali. Kumbuka watu wapo tayari kukusamehe pale unapokosea, ila unapowadanganya, hawatakusamehe kamwe, na hata wakikusamehe hawatakuamini tena.
17. Unapoongoza mikutano, unahitaji kuwa makini sana ili watu waweze kuondoka wakiwa na hamasa ya kwenda kufanyia kazi vile mlivyokubaliana. Kwanza kabisa tatizo kubwa la mikutano mingi ni kuchelewa kuanza, kuchelewa kuisha na hapo katikati kupoteza muda mwingi. Hakikisha unaandaa ajenda za mkutano, kuanza kwa muda na kumaliza kwa muda. Hii itawafanya watu wafurahie mikutano na kufanyia kazi yale mnayoazimia.
18. Unapoibuka ubishani kwenye mkutano wewe kama kiongozi unahitaji kwenda nao vizuri, kwanza usikataze ubishani, ila hakikisha unakuwa ni ubishani chanya, ambapo watu wanatoka na kitu cha kufanyia kazi. Usiwe ubishani hasi ambapo watu fulani wanajiona wao ni bora na wengine hawafai. Tafuta kitu ambacho kinawaunganisha wanaobishana pamoja na wahamasishe wakifanyie kazi. Kwa njia hii utapata mawazo mengi na mazuri.
19. Jifunze kuwasikiliza wengine na njia bora sana ya kufanya hivyo ni kuwa mdadisi. Mtu anapoongea wewe kuwa mdadisi, taka kujua zaidi kuhusiana na yeye mwenyewe na kile anachoongea. Uliza maswali yanayoanza na KWA NINI… ILIKUWAJE… kwa njia hii watu watapata nafasi ya kujieleza zaidi. Siri kubwa sana unayotakiwa kujua hapa ni hii, hakuna kitui ambacho watu wanapenda kama kusikilizwa. Unapoacha kila kitu na ukamsikiliza mtu, atavutiwa na wewe sana. Viongozi wote wenye mafanikio ni wasikilizaji wazuri. Anza na wewe kuwa msikilizaji. Na huwezi kusikiliza mtu huku unafanya vitu vingine kama kujibu ujumbe kwenye simu.
20. Kitu kimoja muhimu sana kuzingatia kwenye mawasiliano yako ni hiki, ongea taratibu, ongea kwa sauti ndogo na ongea maneno machache. Ongea taratibu, sio sana ila kwa kasi ambayo mtu anaweza kukuelewa, usiongee kama unakimbizwa. Ongea kwa sauti ndogo ila sio sana, bali ile ambayo mtu anakusikia vizuri, usipike kelele. Na ongea maneno machache, sio sana bali yale yanayomtosha mtu kukuelewa, usiongee maneno mengi mpaka watu wasahau yale ya msingi. Halafu baada ya hapo nyamaza. Kwa njia hii utafikisha ujumbe wako vizuri sana na anayekusikiliza atahamasika kuchukua hatua.
Hayo ndio mambo 20 niliyokuandalia kutoka kwenye kitabu SPEAK LIKE CEO, naamini kuna ambayo umejifunza hapa, kikubwa ni wewe uyafanyie kazi, na haijalishi upo kwenye ngazi gani sasa, mawasiliano mazuri yatakupeleka mbele zaidi. Anza sasa kufanyia kazi mbinu hizi nzuri ulizojifunza hapa.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.