Kila mmoja wetu anapitia hali hii katika kipindi fulani kwenye maisha yake, wapo wanaopata mgogoro huu kwa muda mfupi, wapo wanaoishi na mgogoro huu maisha yao yote.

Huu ni mgogoro kati yako wewe na nafsi yako.

Huu ni mgogoro mkubwa sana, ambao unaleta hasira kubwa kwako.

Hivyo mapema utakapousuluhisha, ndivyo itakuwa rahisi kwako kuwa na maisha bora.

Na kama utashindwa kuusuluhisha, kila siku utakuwa na hasira na maisha yako na hata upate nini, bado utaona maisha yako sio bora.

Mgogoro huu unatokana na nini?

Chanzo cha mgogoro huu ni tofauti yako wewe na jamii inayokuzunguka. Wewe una picha fulani ya maisha bora kwako. Unajua ni vitu gani muhimu kwako kufanya ili uyafurahie maisha yako. na jamii nayo ina picha fulani ya mtu kama wewe, inajua ni kitu gani unatakiwa kufanya ili uonekane ni mtu wa kawaida, kinyume na hapo utaonekana wa ajabu katika jamii.

Sasa kwenye kutaka kuishi maisha yako au maisha ya jamii ndipo mgogoro mkubwa sana unaibuka ndani yako. mgogoro huu unaleta hasira kubwa sana kwa sababu mara nyingi utakuwa unavutiwa kufanya vile jamii inavyokutegemea, na wakati huo sio kitu bora kwako.

Kutatua au kutokutatua mgogoro huu.

Wapo watu ambao wanatatua mgogoro huu mapema sana kwenye maisha yao kwa kuamua kwenda na yale maisha ya ndoto zao, bila ya kujali jamii inawachukuliaje. Hawa huwa na maisha bora na ya mafanikio, na baadae jamii inawakubali sana.

Wao watu ambao wanashindwa kutatua mgogoro huu kwa maisha yao yote, na hivyo kuwa wanafanya vile jamii inavyowategemea wafanye, na huku ndani ya mioyo yao wakijua kabisa ya kwamba wanachofanya sio sahihi kwao. Watu hawa huenda na hali hii maisha yao yote na japo kwa nje wanaweza kuonekana wako vizuri, kwa ndani kuna mgogoro mkubwa sana. Watu hawa hawafikii mafanikio makubwa kwao binafsi, na hata jamii haiwaoni kuwa wa kipekee.

Tatua mgogoro huu leo.

Je wewe upo upande gani? Ulishatatua mgogoro huu au bado unakusumbua?

Kama ulishatatua hongera sana na endelea kuweka juhudi kwenye yale maisha ambayo umeyachagua wewe mwenyewe.

Kama bado hujautatua utatue leo, kwa kuamua kuishi yale maisha ambayo ni muhimu kwako, bila ya kujali wengine wanaishije au wanasemaje. Hili litakuletea faraja kubwa sana na hata utakapokutana na changamoto, ambazo lazima zije, utazikabili kwa furaha na sio hasira.

SOMA; Matatizo Yote Kwenye Maisha Yako Yanatokana Na Kitu Hiki.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kuna mgogoro mkubwa unaoendelea ndani ya nafasi yangu. Mgogoro huu ni kati ya maisha ya ndoto yangu na maisha ya ndoto ya jamii inayonizunguka. Mgogoro huu unatokana na jamii kunilazimisha kuishi maisha ya ndoto yao, na wakati huo mimi nataka kuishi maisha ya ndoto yangu. Leo namaliza mgogoro huu kwa kuchagua kuishi maisha ya ndoto yangu.

NENO LA LEO.

Nothing is given to man on earth – struggle is built into the nature of life, and conflict is possible – the hero is the man who lets no obstacle prevent him from pursuing the values he has chosen.

 Andrew Bernstein

Hakuna kitu ambacho mtu anapewa kirahisi hapa duniani, mapambano ndio asili ya maisha, na mgogoro haukosekani. Shujaa ni yule mtu ambaye haruhusu chochote kimzuie yeye kufanya kile ambacho ni muhimu kwake.

Je wewe ni shujaa?

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.