Moja ya vitu vinavyowarudisha watu wengi nyuma ni kulazimika kufanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya.

Na ni bora ingekuwa ni vitu vya kawaida tu, hapa unakuta unafanya vitu ambavyo ni kinyume na vile unavyoamini, kwa kifupi ni vitu ambavyo sio vizuri.

Kama kitu ni kibaya, na unajua ndani ya nafsi yako ni kibaya, kukifanya kutakusumbua sana, na kukuzuia wewe kusonga mbele. Hapo haijalishi ni watu wangapi ambao wanakifanya. Kinachojali hasa ni kwamba wewe umefanya, na umefanya ukiwa unajua kabisa ya kwamba sio kitu kizuri umefanya.

Kuweza kuishi maisha ambayo ni bora kwako, utakayoyafurahia na yenye mafanikio, sio kazi ndogo. Na ukubwa wa kazi hii unaanzia kwa wale wanaotuzunguka, wale tunaokuwa nao muda mwingi. Wana ushawishi mkubwa kwetu na wakati mwingine tunalazimika kufanya hata ambayo hatukupenda kufanya.

Ni lazima uweze kujua kipi ni sahihi kwako kufanya na kipi sio sahihi, na uhakikishe unasimamia mambo hayo mawili bila ya kujali upo kwenye mazingira gani.

Kama kitu ni kibaya, na wewe unajua ni kibaya, hata kama dunia nzima inafanya kitu hiko, wewe usikifanye. Hii ni kuhimu sana kwa mafanikio yako binafsi na maisha bora yenye furaha.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutumia Akili Yako Vizuri Na Ikakuletea Kila Unachotaka

TAMKO LANGU;

Ninajua ni kipi sahihi kwangu kufanya na kipi sio sahihi. Najua pia ni rahisi kushawishika kufanya kile ambacho sio sahihi kwa sababu tu kila mtu anakifanya. Kuanzia sasa nimeamua kama kitu sio sahihi kwangu kufanya, sitakifanya, hata kama kinafanywa na dunia nzima. Najua kusimamia kile ninachoamini ndio msingi mkuu wa mafanikio yangu na maisha yangu bora.

NENO LA LEO.

Right is right, even if everyone is against it, and wrong is wrong, even if everyone is for it.

William Penn

Ukweli utabaki kuwa ukweli, hata kama kila mtu anaupinga, na uongo utabaki kuwa uongo hata kama kila mtu anaukubali.

Jua kipi ni sahihi kwako na kifanye, kile ambacho sio sahihi usifanye, hata kama kila mtu anafanya.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.