Moja ya vitu vinavyotufanya tunaendelea kuwepo duniani kama binadamu ni kujali. Ndio tunajali sana kuhusu sisi wenyewe na hata wale wanaotuzunguka.

Tunapenda kuona tupo kwenye hali salama na hata wale wa karibu yetu pia tunapenda kuona wapo salama.

Lakini kujali huku pia kunakuja na hasara zake, kuna kujali ambapo kunakuumiza wewe mwenyewe au wale ambao wanakuzunguka.

Leo tutaangalia kujali ambapo kunawaumiza wale ambao ni wa karibu yetu.

Tuseme labda kuna mtu wako wa karibu, ndugu, mtoto, mwenza au rafiki na amekuja kwako ana mpango wa kufanya jambo fulani kubwa kwenye maisha yake. Na wewe kwa unavyomfahamu unaona kabisa hawezi. Hivyo kwa kuwa unamjali unamwambia ukweli, hiki unachotaka kufanya hutaweza au kitakushinda.

Umemwambia hilo kwa nia njema kabisa, kwa sababu unamjali, kwa sababu hutaki kumwona akipata shida au kuingia kwenye changamoto, unastahili hongera! Si ndio?

Japo unajali, lakini hapa umemuumiza sana huyu mtu. Umemuumiza kiasi kikubwa sana na hataweza kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yake. Na vile ulivyo mtu wa karibu kwa uliyemwambia, basi anaamini sana maneno yako.

Unawezaje kutumia kujali kwako kumsaidia mtu wa karibu yako?

Baada ya yeye kukuambia mpango mkubwa alionao, hebu taka kujua zaidi ni kiasi gani amejipanga. Mwambie akueleze vizuri ni jinsi gani atakavyosonga mbele kama mambo hayatakwenda kama alivyopanga. Na kulingana na majibu yake utajua amejipanga kiasi gani.

Na mwishoni, angalia ni jinsi gani inawezekana kwake, ni maeneo gani muhimu azingatie. Halafu mpe moyo afanye, mhamasishe asonge mbele hata kama atakutana na changamoto.

Lakini vipi akishindwa? Si nitaonekana sikumtahadharisha mapema?

Ndio atashindwa, tena mara nyingi tu. Hapana, hutaonekana kwamba hukumtahadharisha.

Na kushindwa huku ni faida kwake, kwa sababu atajifunza zaidi. Atakuwa mbali zaidi kuliko ambavyo angeacha kufanya kabisa. Na kama amejitoa kweli, ni rahisi kwake kutokea hapo kwenye kushindwa, kuliko kuanzia mwanzo kabisa.

Kujali kwako kusiwe kikwazo cha wengine kushindwa kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yako. bali kuwe hamasa ya watu kuchukua hatua zaidi.

SOMA; Unachotakiwa Kuelewa Pale Ndugu Zako Wa Karibu Wanapokukatisha Tamaa.

TAMKO LANGU;

Nimejua kwamba pamoja na kujali kwangu nimekuwa nawaumiza watu wa karibu yangu. Nimekuwa naona nawaokoa na matatizo makubwa ya mbeleni kumbe nawazuia kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yao ambazo zingeboresha zaidi maisha yao. Kuanzia sasa sitatumia tena kujali kwangu kuwa kikwazo kwa wengine, bali nitatumia kuwa hamasa kwa wengine kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yao.

NENO LA LEO.

Our duty is to encourage every one in his struggle to live up to his own highest idea, and strive at the same time to make the ideal as near as possible to the Truth.

Swami Vivekananda

Wajibu wetu ni kuwatia moyo wengine katika harakati zao za kuishi maisha bora kwao, na kukazana kufanya maisha hayo kuwa ya kweli kadiri inavyowezekana.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.