Maumivu hayakwepeki…
Umepata hasara kwenye biashara…
Nyumba yako imeungua….
Mtu wako wa karibu amefariki…
Ulichotegemea hujakipata…
Hii ni kwa sababu kuna mambo mengi ambayo hatuwezi kuyaathiri, na hivyo hatuwezi kukwepa maumivu. Yaani maumivu yapo na yanatujia mara kwa mara.
Mateso ni kuchagua, tofauti na maamuzi, wewe ndio unaamua uteseke au la.
Ndio maumivu yanaleta mateso, lakini mateso haya ni maamuzi yako wewe mwenyewe.
Na mateso haya yanatokana na ufahari wako na ubinafsi pia.
Pale unapoona kinachotokea kwako hakistahili, kwa nini wewe na kwa nini pamoja na kukazana mabaya yanakutokea wewe.
Unachagua wewe mwenyewe kuteseka, na kadiri unavyoendelea kufikiri kwa ufahari wako na ubinafsi wako ndivyo unavyozidi kujitesa.
Ufanyeje ili usiteseke?
Jua kila kinachotokea ni sehemu ya maisha yako, iwe kibaya au kizuri. Pia jua kwamba unavyofurahia kizuri kuna wakati utakutana na kibaya. Na pale kibaya kinapotokea, usione ni bahati mbaya kwako.
Pia acha kukweza ufahari wako, usitake mambo yako yawe mazuri ili watu waone mambo yako ni mazuri. Hili pia litakutesa sana.
Kuacha ubinafsi pia kutakusaidia kuepuka mateso unayojisababishia mwenyewe. Kwa sababu unapokuwa mbinafsi unajifikiria wewe tu, lakini unapowafikiria wengine utaona maumivu unayopitia wewe ni sehemu ya kawaida ya maisha.
SOMA; FEDHA; Tatizo Sio Fedha, Tatizo Ni Wewe.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba maumivu ni lazima na ni sehemu ya maisha, ila mateso ni kuchagua mwenyewe. Kuanzia sasa nimeamua kutokuteseka tena. Na nitafanya hivyo kwa kuweka pembeni ufahari wangu na pia kuacha ubinafsi.
NENO LA LEO.
“Pain is inevitable. Suffering is optional.”
― Haruki Murakami
Maumivu hayakwepeki. Mateso ni kuchagua.
Usikubali kuteseka kwa jambo lolote lile, wewe ni zaidi ya maumivu unayokutana nayo. Usichague kuteseka.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.