Kwa usalama wako binafsi, zungukwa na watu wenye busara, watu ambao mnafikiri sawa, watu ambao mnakwenda mbali zaidi ya pale mlipo sasa. Na watu ambao wanaboresha kile wanachofanya na maisha yao kila siku.
Kwa kuzungukwa na watu wa aina hii inakuwa ahueni kwako kuchukua hatua na kuendelea kuweka juhudi, hata pale unapokutana na changamoto au vikwazo.
Lakini kama utakaidi hili, na kuendelea kuzungukwa na watu ambao hawana mbele wala nyuma, watu waliokata tamaa na maisha yao, na watu ambao hawafikirii kwenda mbali zaidi ya walipo sasa, itakuwa vigumu sana kwako kupiga hatua. Kila utakachojaribu kufanya utaona hakiwezekani kutokana na ushahidi wa uongo utakaopokea kutoka kwa watu hawa.
Tumeshaambiana tena na tena ya kwamba vile ulivyo ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka, wale ambao unatumia muda mwingi kuwa nao. Hivyo unaweza kujua utaendelea kuwa na maisha gani kwa kuangalia maisha ya wale ambao wanakuzunguka, huwezi kwenda mbali zaidi yao, ndivyo ilivyo.
Njia pekee ya kwenda mbali zaidi ya ulipo sasa ni kuangalia wale walioko mbali, au wanaoenda mbali, na kuzungukwa nao. Ila kuendelea kuzungukwa na wanaokuzunguka sasa, ambao wamekuzunguka kwa muda mrefu, utaendelea kupata matokeo unayopata sasa.
SOMA; Nguvu Kubwa Inayokurudisha Nyuma Na Jinsi Ya Kuishinda.
TAMKO LANGU;
Kwa usalama wangu binafsi, nimeamua kuzungukwa na watu ambao wanajua wanakokwenda na maisha yao, wale ambao wanataka kuwa bora zaidi. Nimejua ya kwamba kuzungukwa na watu wasiojua wanakokwenda, waliokata tamaa na maisha yao ni shimo kubwa kwa mafanikio yangu.
NENO LA LEO.
Surround yourself with only people who are going to lift you higher.
Oprah Winfrey
Zungukwa na watu ambao wanakusukuma kwenda juu zaidi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.