Maneno ya ukweli hayabembelezi…

Na maneno yanayobembeleza sio ya kweli…

Hivyo ni wajibu kwako kuchagua, unataka kutoa maneno ya kubembeleza au unataka kutoa maneno ya kweli?

Ukitoa maneno ya kweli, watu hawatapendezwa, na wanaweza kukuchukia, ila ni kwa muda tu. Baadaye wataelewa, kwa sababu ukweli huwa haujifichi kwa muda mrefu. Baada ya muda utafahamika na wewe utakuwa umesaidia.

Ukitoa maneno ya kubembeleza, watu watafurahia na wanaweza kukupenda, ila ni kwa muda tu. Baadaye ukweli utafahamika, na hapa watu watakuchukia kwa sababu hukuwaambia ukweli tangu mwanzo, huenda wangechukua hatua mapema, na mambo yasingekuwa mabaya.

Japo hufanyi ili kupendwa au kuchukiwa na watu, japo huhitaji kujali kama ni nani anakupenda au kukuchukia, mara zote sema ukweli, hata kama ni mchungu kiasi gani, hakuna kilicho bora zaidi ya ukweli.

Mara zote sema ukweli.

SOMA; Mambo 15 Ya Kung’ang’ania Bila Ya Kujali Watu Wanasema Nini.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba maneno ya ukweli hayabembelezi na maneno yanayobembeleza sio ya ukweli. Kuanzia sasa nimeamua kusema ukweli mara zote, najua hii haitawapendeza wengi, lakini baadaye watanielewa.

NENO LA LEO.

“If you are busy pleasing everyone, you are not being true to yourself”
― Jocelyn Murray

Kama upo bize kuwafurahisha wengine, hauwi mkweli kwako wewe mwenyewe.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.