Kusema uongo na kutokutoa taarifa yote ni vitu viwili tofauti kabisa.

Na japo ni muhimu sana kusema ukweli, haimaanishi ni lazima utoe taarifa yote.

Kuna wakati unahitaji kutoa taarifa kiasi na sehemu nyingine ya taarifa ukaiacha. Hapa hudanganyi, bali unatoa ile taarifa inayomtosha mtu kwa wakati fulani na kuacha nyingine ambayo sio muhimu au wakati wake bado wa kuitoa.

Mara zote sema ukweli, ila sio lazima utoe taarifa yote kwa kila mtu. Kulingana na mazingira uliyonayo kwa wakati huo, unaweza kutoa sehemu ya taarifa na nyingine ukaiacha na kuja kutoa baadae wakati ambapo mazingira yanaruhusu.

Hapa hujadanganya, umekuwa mkweli na umezingatia hali halisi na huhitaji kutengeneza uongo juu ya uongo ili kuendelea kuaminika.

Na kutoa sehemu ya taarifa haimaanishi kusema nusu ya ukweli, bali ni kusema ukweli kama ulivyo, ila kuna baadhi ya taarifa huhitaji kuitoa katika wakati huo.

SOMA; Kama Maisha Ni Vita, Basi Huu Ndio Ukweli Unaotakiwa Kujua.

TAMKO LANGU;

Japokuwa nahitaji kuwa mkweli mara zote, haimaanishi nahitaji kutoa taarifa yote kila wakati. Kuna wakati ambapo nahitaji kutoa sehemu ya taarifa kulingana na mazingira yaliyopo. Nalizingatia hilo na kamwe sitosema uongo.

NENO LA LEO.

The Truth which has made us free will in the end make us glad, also. ~ Felix Adler

Ukweli ambao umetuweka huru, mwishoni utatufanya tuwe na furaha.

Mara zote sema ukweli, japo sio lazima kutoa taarifa kamili, ila usidanganye. Ni rahisi kusimamia ukweli kuliko uongo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.