Wakati unasoma hapa kuna mambo mengi sana yanayoendelea duniani, zaidi ya mambo milioni.
Na katika mambo hayo kuna ambayo ni mazuri na kuna ambayo ni mabaya.
Kutokana na mambo hayo, wewe mwenyewe unaweza kuchagua kuiona dunia kuwa nzuri au kuwa mbaya.
Kwa kufikiria zaidi yale mambo mabaya yanayotokea, utaiona dunia kuwa sehemu mbaya sana. Utaogopa sana dunia na utaona maisha hayana maana.
Kwa kufikiri zaidi yale mambo mazuri yanayotokea, utaiona dunia kuwa sehemu nzuri sana. Utaipenda dunia na utakuwa na hamasa ya kuendelea na maisha yako hapa duniani.
Yote hii inaanza na wewe, ni wapi umeelekeza mawazo yako zaidi.
Na hili pia linakuja kwenye maisha yako ya kila siku. Kuna mambo mengi yanayokutokea, baadhi mazuri na baadhi mabaya.
Kama utayafikiria yale mabaya tu utaona maisha yako ni ya hovyo na hayana maana kuishi. Utakata tamaa na kushindwa kusonga mbele zaidi.
Kama utayafikiria yale mazuri utayaona maisha yako ni bora na kuyafurahia kuishi. Hapa utakuwa na hamasa ya kuendelea kuyaboresha zaidi.
Tena, inaanzia kwako, kwa wapi unapopeleka mawazo yako, kuzuri au kubaya.
Na sio kwamba unajifanya mabaya hayapo, yapo na unajua yapo lakini wewe unafikiri zaidi kwa yale mazuri.
SOMA; Kwa Kuwa Bado Upo Hai, Mambo Mazuri Yatatokea Kama Utafanya Hivi…
TAMKO LANGU;
Nimejifunza kwamba ubaya na uzuri wa dunia unaanza na mimi mwenyewe, kwa yale mawazo ambayo naruhusu yatawale akili yangu. Kama nitafikiri yale mazuri nitaiona dunia kuwa sehemu nzuri. Kama nitafikiri yale mabaya nitaiona dunia kuwa mbaya. Kuanzia leo nimechagua kufikiri zaidi yale mazuri kwenye maisha yangu na kwenye dunia kwa ujumla.
NENO LA LEO.
Live life to the fullest, and focus on the positive.
Matt Cameron
Ishi maisha yako kwa ukamilifu, na fikiri zaidi yale chanya.
Kama utafikiri yale mabaya tu, utaona maisha ni mabaya. Kama utafikiri yale yaliyo mazuri utaona maisha ni mzuri.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.