Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha The Start-Up Of You.

Habari ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu, ni matumaini yangu unaendelea vizuri. Katika wiki hii ya kumalizia mwaka huu 2015 tunakuletea uchambuzi wa kitabu cha The Start-up of You, kitabu hiki kimeandikwa na waandishi wawili amabo ni Reid Hoffman na Ben Casnocha. Bwana Reid Hoffman ndio mwanzilishi mwenza (co-founder) na CEO wa mtandao maarufu wa wanataaluma wa LinkedIn. Kitabu hiki kinazungumzia uboreshaji binafsi wa kila mtu anaopaswa kufanya ili aweze kuishi kijasiriamali. Kitabu kinafundisha kwamba kila mtu ni mjasiriamali na msingi mkuu wa ujasiriamali ni kuumba/kutengeneza na kuboresha, hivyo basi kabla ya kufikiri kuanzisha biashara, jianzishe wewe kwanza, jiboreshe wewe kwanza, jitengeneze wewe kwanza. Utakapokua bora kama wewe ni mwajiriwa utakua thamani kubwa kwenye soko la ajira, na hata kama unataka kuanzisha biashara kama umeshakua bora, utaongeza thamani kubwa sana kwenye biashara yako. Kwa maana biashara haiwezi kua bora kuzidi mimiliki wa biashara hiyo. 

 
Karibu tujifunze mengine.
1. Kama wewe ni mwajiriwa tambua kwamba Jukumu la kujiboresha ni la kwako, na sio la mwajiri wako. Iwe unataka kuwa na ujuzi mpya, ili kufanya vizuri kazi uliyoajiriwa, ni jukumu lako sasa kujifunza ujuzi huo, sio kusubiri hadi upelekwe mafunzo (training) na mwajiri wako. Mfano umegundua ili kazi yako iwe na ufanisi unahitaji kua na ujuzi wa kompyuta, weka mkakati hata wa kwenda kupata mafunzo wakati wa jioni unapotoka kazini. Fanya uwekezaji binafsi (invest in yourself) kwa kujifunza na kuongeza ujuzi wako. Kampuni nyingi haziko tayari kuwekeza sana kwa mwajiriwa maana wanajua, hutafanya kazi hapo miaka yote. Wanajua muda wowote unaweza kuondoka. Hata zile kampuni chache zinazopeleka waajiriwa wake kwenye mafunzo, huingia nao mikataba, kwamba huyo mfanyakazi afanye kazi kwenye hiyo kampuni baada ya miaka kadhaa bila kuondoka. Hii ni kumhakikishia mwajiri kwamba anafaidika na uwekezaji aliofanya kwa mwajiriwa. Ila unapofanya uwekezaji binafsi kwa kujifunza ujuzi mpya na kuongeza uwezo wako wautendaji wako, unakua na faida kubwa zaidi, unaongeza thamani yako, pia unakua huru kwenda popote pale fursa zinapotokea, hata ukibaki kwenye hiyo kampuni ni rahisi kupanda nafasi za juu.
SOMA; Upotoshaji Mkubwa Unaofanywa Kwenye Elimu Ya Ujasiriamali.
2. Kuna Pengo au Ombwe (gap) kubwa linaloongezeka kati ya wanaofahamu kanuni mpya za kazi na wenye ujuzi mpya wa uchumi wa dunia na wale wanaoshikilia mambo ya kizamani, wanafikiri kizamani. Kundi la kwanza ni lile linaloamini katika njia mpya, na ujuzi mpya, kundi hili linaweza kupenya kirahisi kwenye uchumi wa dunia, na wanaweza kuendana na mabadiliko. Kundi la pili ni lile linaloshikilia mambo ya zamani, au unaweza kuwaita wahafidhina, watu wasiopenda mabadiliko, wameridhika na hali waliyonayo. Kundi hili huachwa nyuma sana, maana uchumi mpya wa dunia ya kileo unahitaji ujuzi mpya, moja kwa moja hujikuta wamebaguliwa na soko, na kuonekana hawahitajiki. Mwisho wa siku wao hubaki kuwakosoa wale wanaoendana na mabadiliko na kujifunza njia mpya. Usikubaili kua mhafidhina, utaachwa tu.
3. Nguvu ya kuboresha maisha yetu ipo mikononi mwetu. Unao Uwezo wa kujiboresha na kuboresha ulimwengu unaokuzunguka. Ukiwa bora, vitu na watu wanaokuzunguka nao wanakua bora. Mchakato huu unaanza na wewe.
4. Jiweke kwenye tasnia inayokua kwa kasi maana ndiko kunakua na fursa nyingi. Kama wewe ni mwajiriwa, using’ang’anie kile tu unachokifanya sasa au kile ulichosomea tu, jifunze vitu vipya, hata visivyokua na uhusiano na kazi ya sasa, kama vitu hivyo vinakuwezesha kuingia kwenye tasnia inayokua kwa kasi. Mfano tasnia ya teknolojia na habari kwa sasa inakua kwa kasi, na fursa nyingi zinazaliwa huko, sasa kama wewe unafanya kazi za uhasibu au kilimo, usibakie hapo tu, weka mpango wa kujifunza kuhusu tasnia hiyo inayokua, ukijifunza kila siku kwa saa 1, baada ya miaka 3 utakua mtaalamu aliyebobea katika hilo eneo. Tumia mpango wa ABZ. Mpango A ni uboreshaji wa ujuzi ulio nao sasa, unaohusiana na kile unachokifanya sasa. Mpango B, ni mpango wa kujifunza ujuzi wa vitu ambavyo vinatofautiana kidogo na mpango A japo kuna uhusiano fulani, mpango B unakusaidia pale mpango A unaposhindwa kufanya kazi au pale unapotaka kuhamia mpango B pengine fursa huko ni nzuri kuliko kwenye mpango A. Mpango Z ni mpango wa tofauti kabisa, pale ambapo mipango yote miwili imefeli sasa unakwenda kwenye Mpango Z. Mfano mpango A unaweza kua ni Ajira yako, mpango B ni biashara, Mpango Z ukawa ni kuingia kwenye Siasa. Mfano mwingine, Mpango A unaweza kua ni kuboresha utaalamu wako wa uhasibu, mpango B ukawa kujifunza ukaguzi wa mahesbau (auditing). Mpango Z ukawa ni kufanya kilimo.
5. Safari ya kujiboresha haina mwisho. Kampuni zilizofanikiwa sana hua hazina mwisho wa kujiboresha, yani kwao uboreshaji ni mchakato endelevu. Mfano kampuni ya kubwa na maarufu ya uuzwaji wa vitabu Amazon, wao wanasema kila siku kwao ni kama Siku ya kwanza (Day 1), yaani kila siku kwao ndio uboreshaji unaanza. Kampuni hii ina mafanikio makubwa sana hata mmiliki wake Bwana Jeff Bezos ni moja wa matajiri wakubwa wa dunia, kwa sasa anashika nafasi ya 15 kwenye orodha ya watu tajiri duniani, hii ni kwa mujibu wa jarida la Forbes la 2015. Huu ni moja tu ya mifano kibao, ya biashara na watu wanaojiboresha kila kukicha. Uboreshaji wa maisha yako unapaswa kua endelevu, uboreshaji wa biashara yako vivyo hivyo unapaswa kua endelevu. Usikubali kubweteka na mafanikio uliyonayo leo ukaacha kujiboresha. Usipojiboresha unaachwa nyuma, maana dunia inabadilika kila kukicha. Ukuaji wako unategemea kujiboresha kwako, usipokua ina maana unadumaa au unakufa. If you’re not growing, you’re contracting. If you’re not moving forward, you’re moving backward
6. Inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni moja (1,000,000) wanaweza kufanya kazi yako unayofanya. Ukiachilia hilo, wapo watu wengi wanaotamani hiyo kazi yako. Je ni kipi kinachokufanya uwe wa kipekee kutoka kwenye hilo kundi kubwa la watu? Kumbuka kila kitu kinachotamaniwa lazima kuwe na ushindani. Na huwezi kuwa wa kipekee kama huna sifaa zinazokutofautisha na wengine, mojawapo ikiwa ni ubora unaokua kila siku. Fahamu upekee wako ni upi, kisha anza kuuendeleza zaidi ili uonekane.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
7. Kuwa bora kuliko ushidani au washindani ni jambo la msingi la kila mjasiriamali. Kila sekta makumpuni kadhaa yanashindania kupata kila dola ya mteja. Mfano kama wateja wanatumia elfu moja (1,000) kwa siku kwa ajili ya mawasiliano, makampuni yote ya simu yanashindania kuipata hiyo elfu moja ya mteja. Hivyo hivyo kwenye sekta nyingine. Kama bidha au huduma unayotoa, haina utofauti wa wazi na bidhaa au huduma za washindani wako, hakikisha unafanya kitu. Unless it’s first, only, faster, better, or cheaper—it’s not going to command anyone’s attention. Good entrepreneurs build and brand products that are differentiated from the competition.
8. Lengo ambalo linaweza kufanikishwa kwa hatua moja tu hua linakosa hamasa au maana. Mfano wewe ni mfanyakazi na una mshahara wa laki tano (500,000) kwa mwezi halafu unajiwekea lengo la kununua baisikeli moja ya 150,000/= kwa mwaka, linakua halina mashiko maana hata ndani ya mwezi mmoja unaweza kununua. Lengo lenye maana na lenye hamasa ni lile linalohitaji kupitia hatua kadhaa, ambazo zitahitaji commitment ya hali ya juu. Unapoweka malengo usiweke malengo ambayo hata ukiyafanikisha panakua hakuna utofauti na ulivyokua mwanzo au panakua na tofauti ndogo. Weka malengo ambayo ukiyafanikisha panakua na tofauti ya wazi kabisa ya kabla na baada ya kufanikisha malengo. A goal that can be achieved in a single step is probably not very meaningful—or ambitious.
9. Masoko yasiyokuwepo hayajali wewe ni mwerevu (smart) kiasi gani. Hivyo hviyvo haijalishi jinsi gani umekua ukifanya kazi kwa bidii, au jinsi gani unavyopenda unachokifanya. Kama hakuna atakayekulipa kwa huduma unazotoa katika soko la ajira, itakua ni kazi ngumu sana. Hii ina maanisha kama unachokifanya, au ujuzi ulionao hauna soko, basi ujue haijalishi uko nondo kiasi gani kwenye hiyo fan,i thamani yako haitaonekana. Markets that don’t exist don’t care how smart you are.
10. Kabla ya kulalamika uongezewe mshahara kuna swali muhimu kwa kila mwajiriwa anapaswa kujiuliza. Je ni thamani gani unayoongeza katika kazi yako? Ikitokea umeacha ghafla kwenda kazini, ni nini hicho unadhani hakitafanyika kutokana na wewe kukosekana? Hapo ndipo unapoongeza thamani, ila kama hakuna utofauti, na kama wengine wanaweza kuziba pengo lako hata lisionekane, basi ujue thamani yako ni ndogo sana. Ili uweze kua na sauti kwenye kazi yako lazima uwe na thamani kubwa unayoongeza kwenye hiyo kampuni. Ukiwa wa muhimu kwenye kazi yako hata linapokuja swala la kuongezwa mshahara unaweza kua na sauti. Hivyo usipoteze muda kudai nyongeza ya mshahara wakati thamani yako ni ndogo, ongeza thamani yako, kwa kujifunza vitu vipya vinavyoweza kuongeza ufanisi wako wa kazi na kufanya upewe majukumu muhimu ya kampuni.
11. Njia rahisi ya kutambua vitu unavyowezakufanya vizuri (your strengths) angalia vile vitu watu wanapenda kukusifia au kukupongeza navyo, japo inaweza isiwe ni vyote, lakini asilimia kubwa ya vile vitu watu wanakusifia navyo mara kwa mara ujue ndio uwezo wako ulipo, na yamkini mafanikio yako asilimia kubwa yatatokana na uendelezaji wa vitu hivyo. Kama wewe ni mwajiriwa angalia ni vitu gani mwajiri wako au bosi wako unayeripoti kwake anapenda kukusifia na kujivunia kwamba unafanya vizuri. Unaweza pia kumuuliza kwa nia ya kutaka kujiboresha zaidi. Think about the things people frequently compliment you on—those may be your strengths
12. Njia ya haraka ya wewe kubadilika, ni kuambatana na watu ambao tayari wako vile unavyotaka kua. Ni rahisi kuiga tabia na imani za marafiki zetu tunaokua nao mara kwa mara. Kama inavyojulikana kwamba wewe ulivyo ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Kwa msingi huo kama unataka kua mtu wa kufanya mambo makubwa lazima uzungukwe na watu angalau watano wanaofanya mambo makubwa. Utajikuta automatic na wewe unaiga hizo tabia bila gharama kubwa. Tofauti na kuzungukwa na watu wavivu alafu unataka kua mtu wa bidii, unajifunza sana kuhusu kufanya kazi kwa bidii lakini muda mwingi umezungwa na wavivu, itakuwia ngumu sana kubadilika. If your friends are the types of people who get stuff done, chances are you’ll be that way, too
SOMA; Njia TATU Za Kufanya Moto Wa Ujasiriamali Uendelee Kuwaka Kwenye Nafsi Yako…
13. Kila mtu anaaina mbili za asset (mali) za kukusaidia kwenye taaluma yako ya kazi. Aina ya kwanza ni mali zisizoshikika (soft asset), hivi ni vile vitu ambavyo huwezi kuviuza moja kwa moja kupata pesa. Vitu hivyo vina mchango usioshikika (intangible contributors) katika mafanikio yako. Mali hizo ni kama maarifa uliyonayo, taarifa zilizopo kwenye ubongo wako, connection ulizonazo za watu mbalimbali na imani uliyojijengea kwao, ujuzi mbalimbali ulionao, heshima yako na jina ulilojijengea kwenye jamii. Hizo ni baadhi ya mali zisizoshikika (soft asset). Kwa upande wa mali zinazoshikika (hard assets) ni vile vitu unavyoweza kuviorodhesha kama vitu unavyomiliki, mfano fedha taslimu ulizonazo kwenye pochi au zilizopo benki, vitu kama kompyuta, nyumba n.k
14. Katika aina hizi mbili za mali, yenye thamani zaidi ni zile zisizoshikika(soft assets) hizi ndizozinazopelekea kufanikiwa zaidi kwa kuongeza thamani yako. Aina hii hakuna mtu anaeweza kuja kukupokonya, yani mali hizi zipo ndani yako. Unapokutana na changamoto ambazo wengine wanaziona ni ngumu, lakini wewe unaziona ni rahisi, basi tambua unamiliki soft assets zenye thamani. Kitu kitakaochokutengananisha na wengine sio komputa nzuri unayomiliki au fedha ulizonazo benki, bali ni thamani ya hizi mali zisizoshikika kama ujuzi mbalimbali, connection yako na watu wenye thamani, taarifa sahihi ulizo nazo, uwezo wako wa kufanya mambo makubwa wengine wasiyoweza kufanya. Ukiweza kufanikiwa katika kuzipata mali hizi ni dhahiri kwamba lazima ukuaji wako utakwenda hatua nyingine kila wakati. Utaweza kufanya mambo makubwa wengine wasiyoweza na utatambulika na wanaokuzunguka. Often it’s when you come in contact with challenges other people find hard but you find easy that you know you’re in possession of a valuable soft asset.
15. Katika kujenga mahusianao mazuri na mtu mwingineinategemea misingi miwili. Kwanza kuona ulimwengu kwa jicho la huyo mwenzako. Yaani kuweza kuona anavyoona yeye. Katika hili hakuna anayefahamu vizuri kama mjarisiamali mwenye ujuzi, kwa maana mjasiriamali anatambua fika ili aweze kufanya vizuri lazima awe na uwezo wa kuuona ulimwengu kama wateja wanavyoona. Wajasiriamali wanafanikiwa pale wanapozalisha vitu ambavyo wateja wako tayari kununua. Hii inamaanisha kuelewa vizuri nini kinaendelea kwenye vichwa vya wateja, kufahamu wateja wanatamani nini na sio kujiangalia wewe unataka nini.
16. Msingi wa pili au hitaji la pili katika kujenga mahusiano mazuri na watu wengine, ni kufikiri kuhusu jinsi unavyoweza kusaidia au kushirikiana na huyo mwenzako badala ya kufikiri kuhusu nini utapata kutoka kwake. Kwa bahati mbaya hii imekua ni hulka ya watu wengi, pale unapotaka kuanzaisha uhusiano na mtu fulani, au urafiki au hata ushirika wa kibishara na mtu mwingine, kitu cha kwanza kufikiri ni jinsi gani wewe utanufaika kutoka kwake. Bahati mbaya hata katika mazungumzo ya awali unaonyesha wazi kuna kitu wewe unategemea unufaike zaidi. Hii dhana hupelekea biashara nyingi sana zisifanikiwe maana unaonekana ni mtu wa maslahi binafi zaidi bila kujali mwenzako yeye atanufaikaje. Ukitaka ufanikiwe mweke mwezako mbele, fikiria ni thamani gani utaiongeza katika huo uhusiano, huyo mwenzako atanaufaikaje kwanza na wewe.
17. Mifumo yetu ya elimu inatufundisha kukariri taarifa au facts zilizohifadhiwa kwenye vitabu na kisha kuzitumia wakati wa kujibia mtihani. Falsafa hii inatazama elimu kama mali isiyohamishika wala kubadilika (fixed asset) kwamba unajifunza kisha unakua nayo hiyo elimu milele. Lakini kama msomi wa kisasa huwezi kupata elimu kwa mtindo huu, maana elimu haisimami sehemu moja (the knowledge you need is not static) bali inabadilika kila siku. Katika ulimwengu wa kazi kila siku ni siku ya mtihani, maana kila siku inakuja na changamoto mpya zisizotabirika. Stockpiling facts won’t get you anywhere. What will get you somewhere is being able to access the information you need, when you need it.
SOMA; Sababu Kumi(10) Kwa Nini Uendelee Kubaki Kwenye Ajira Kwa Muda Kabla Ya Kujitosa Moja Kwa Moja Kwenye Ujasiriamali.
18. Unapokua huna uchaguzi mwingine zaidi ya kupambana, unapambana kisawasawa tena kwa bidii. Hivyo hivyo Unapokua huna rasilimali unazitengeneza. Kukosa rasilimali fulani hakupaswi kumzuia mtu kutimiza ndoto zake. When you have no choice but to create, you create.
19. Usipovikabili vihatarishi (risks), vihatarishi vitakukabili wewe. Usidhani kwa kuacha kufanya vitu vikubwa ndo utakua umeepuka vihatarishi, la hasha ni utakua umesogeza mbele tu tena vihatarishi hivyo vitakua vibaya zaidi. Mfano mtu anaogopa kuanza biashara kwa kuona ina risk kubwa, anaamua kuishia kwenye kutafuta kazi zenye usalama zaidi (job security), bila kujua kwamba hiyo kazi huwezi kudumu nayo na kurithisha watoto wako pindi umeondoka hapa ulimwenguni. Utatumika kwenye hiyo kazi, ila ikitokea umepata ulemavu au umeshindwa kufanya hiyo kazi kutokana labda na umri kwenda, mwajiri wako hatakuonea huruma, atakachofanya ni kutafuta mrithi wako. Kisha utalipwa mafao yako alafu habari ndo imeishia hapo. Jiulize hayo mafao unakwenda kufanyia nini? Hapa wengi ndio wanakufa mapema kwa presha na kisukari kwasababu ya mawazo mengi. Maana ukicheki huna ujuzi wowote wa biashara, na ile hela ya mafao inaendelea kuyoyoma, kila biashara ukijaribu inafeli. Kwanini usife mapema. Wenzako walioanza biashara enzi hizo leo hii ni matajiri na wanauwezo wa kumilikisha watoto wao biashara zao. Hebu na wewe jaribu kummilikisha mwanao hiyo kazi yako ya ajira uone kama itawezekana. Remember: If you don’t find risk, risk will find you
20. Kila mtu amezaliwa mjasiriamali, ijapokua hii haimpi kila mtu dhamana ya kuishi kama mjasiriamali. Pia kuzaliwa mjasiriamali haimaanishi kila mtu anatakiwa aanzishe kampuni, la hasha, tunaposema tumezaliwa wajasiriamli, ni kwasababu shauku ya kuumba au kutengeneza (create) ipo ndani ya kila mmoja wetu, na kuumba au kutengeneza ndio msingi wa ujasiriamali. Ili tabia hizo za kijasiriamali ziweze kujidhiirisha zinahitaji kuendelezwa na kulelewa. You can take control of your life and apply entrepreneurial skills to whatever work you do
Asanteni sana
Nikutakie heri na mafanikio tele katika mwaka 2016
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

One thought on “Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha The Start-Up Of You.

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: