Mara nyingi huwa tunaing’ang’ania dunia, huwa tunajishika nayo tukiamini ndio itatupa kile ambacho tunataka.
Mara nyingi pia huwa tunafikiri tunaweza kuidhibiti dunia, kuifanya iende kama vile ambavyo sisi tunataka. Kutaka itupe kila ambacho tunataka.
Lakini yote haya tunayofikiri hayawezekani, na kuendelea kuyafanya ni kuipa dunia nafasi kubwa ya kukuumiza wewe. Kwa sababu mwisho wa siku huwezi kuipeleka dunia kama unavyotaka wewe na utaumia sana utakapokuja kugundua hilo baada ya kupoteza muda mwingi kujaribu.
Kwa kukazana kuifanya dunia ifanye vile unavyotaka, au kuidhibiti, wewe ndio utaishia kuumia na kupelekea kukata tamaa.
Ufanye nini?
Ipe dunia uhuru wa kufanya na kwenda vile ambavyo imekuwa inakwenda.
Using’ang’anie kutaka dunia iende au ifanye vile unavyotaka. Usifikiri kwamba unaweza kuidhibiti dunia.
Unapoipa dunia uhuru, na kujiondoa kwenye kutaka iende unavyotaka au kuidhibiti, unaipa dunia uhuru wa kukuwezesha wewe kuishi maisha yako bila ya kuyaharibu.
Elewa kuna vitu vingi sana ambavyo huwezi kuviathiri hapa duniani. Na pia elewa kila linalotokea, hata kama ni baya kwako lina sababu, na kwa kila unalopitia kuna fursa nzuri sana kwako.
Ipe dunia uhuru wa kwenda vile inavyotaka kwenda na yenyewe itakupa uhuru wa kuishi maisha unayotaka. Jaribu kuing’ang’ania dunia iende unavyotaka wewe na utakosa kabisa uhuru wa maisha yako, kwa kujikuta unaumia na kung’ang’ania vitu ambavyo haviwezekani. Shukuru kwa kila hali unayopitia hapa duniani.
SOMA; Usilalamike, Dunia Imekupa Kila Kitu, Ni Wewe Tu…
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kujaribu kuidhibiti dunia ni kujiharibia maisha yangu mwenyewe. Kuanzia sasa naipa dunia uhuru wa kwenda vile inavyotakiwa kwenda, na nitashukuru kwa kile ninachopata na kukitumia vizuri ili niweze kufika pale ninapotaka. Kung’ang’ania vitu ambavyo siwezi kuvidhibiti ni njia ya kujiumiza, sitofanya hivyo.
NENO LA LEO.
“Flow with whatever is happening and let your mind be free. Stay centered by accepting whatever you are doing. This is the ultimate.”
Chuang Tzu
Nenda na kile kinachotokea na ruhusu mawazo yako yawe huru. Kuwa mtulivu na kubali kile unachofanya. Huu ndio uhuru mkubwa kwako.
Usijaribu kuidhibiti dunia, kutaka iende unavyotaka wewe, utajiumiza sana.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.