Kitabu 50 greatest lessons from life ni kitabu kinachotoa ushauri muhimu wa kuweza kuishi maisha bora na yenye mafanikio. Kitabu hiki kimeandikwa kutokana na uzoefu wa maisha wa mwandishi wa kitabu hiki.
Yafuatayo ni mambo 20 niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Karibu pia ujifunze.
1. Hazina yako kubwa ya maisha ipo kwenye vitu hivi vitatu muhimu; kwanza uwezo wa kufanya kila wakati kuwa bora kwako. Pili; afya yako. tatu; hali yako ya ucheshi.
2. Ni vigumu sana kuwa imara kama afya yako ni mbovu. Ni vigumu sana kufanikiwa kama afya yako ni mbovu. Ukiwa na afya nzuri unacho kila unachohitaji. Ukiwa na afya mbovu maisha yako ni magumu.
3. Pumua taratibu kupitia pua zako. Mbinu hii itakuwezesha kutulia pale ambapo umekutana na changamoto kubwa. Unapokutana na changamoto, kabla hujafanya maamuzi, pumua kwanza, taratibu na kwa muda. Wakati unapumua mawazo hasi yataondoka kama sumu inayoondoka mwilini na akili yako itakuwa safi kufanya maamuzi.
4. Vitu vingi ambavyo watu huwa wanahofia huwa hata havitokei. Lakini bado hofu imekuwa inaharibu maisha ya watu wengi sana. Ione hofu kama sumu, usikubali ikufikie karibu. Chochote unachohofia mara nyingi sio kweli na pia huwezi kuathiri.
5. Mara zote kuwa chanya, unapokuwa chanya unakaribisha mawazo mengine chanya na hii itakuwezesha kutatua changamoto yoyote utakayokutana nayo. Jiamini wewe mwenyewe, na hakuna kitakachokushinda.
6. Kadiri unavyokwenda na maisha yako, utaendelea kugundua kwamba vitu haviko kama vinavyoonekana kwa nje. Endelea kupumua, utumie vizuri kila wakati unaopitia na furahia maisha ambayo unayo.
7. Watu wanaoongea kwa sauti sana na wanaobishana sana mara nyingi hawajiamini. Wanatengeneza hali fulani ya kutaka waonekane ni muhimu.
8. Hakuna mtu yeyote, hakuna ambaye anakujua wewe vizuri. Na wewe hakuna mtu yeyote ambaye unamjua kwa undani. Tunavyoona kwa watu ni vya juu tu, hatuwezi kujua kwa hakika ni nini kipo ndani yao. Kila mmoja kuna maeneo ambayo yuko imara na maeneo ambayo ana udhaifu. Usikimbilie kuhukumu, hukumu yoyote unayoitoa, unakosea, kwa sababu hujui kwa hakika.
9. Usikubali vitu vidogo vidogo vikuvuruge. Usikasirike kwa sababu umepiga simu halafu haikupokelewa. Au umesubirishwa sana, au hukualikwa kwenye sherehe fulani, au umewekwa mwishoni. Haya yote ni madogo sana ukilinganisha na maisha bora uliyonayo.
10. Watu wengi utakaokutana nao kwenye maisha yako ni wazuri na wenye moyo wa kusaidia. Pia utakutana na wachache ambao wana roho nzuri na wasio tayari kusaidia, wasamehe na achana nao. Usikubali hasira na machukizo vikae kwenye akili yako, achilia viende. Usikae na kinyongo, kitakuzeesha mapema. Na kadiri unavyokwenda na maisha yako jua kwamba kila mtu ana changamoto kubwa kuliko inavyoonekana kwenye uso wake.
11. Maisha ni mbio za muda mrefu(marathon) na sio mbio za muda mfupi(sprint). Usikimbie mbio hizo kwa pupa, utachoka haraka na kuishia njiani. Pangilia mwendo wako, ambao unajua utakuwezesha kumaliza mbio zako, kuna wakati utahitaji kubadili mwendo, fanya hivyo kwa mpangilio, utakutana na changamoto, zitatue vyema. Muhimu ni kuzifurahia mbio hizi, huku ukijua unakoelekea.
12. Hofu inanyonya nguvu zako sana. Ukishakuwa na hofu inakuwa vigumu kwako kuchukua hatua. Unapoondokana na hofu unapata nguvu kubwa sana ya kuweza kuchukua hatua kwenye maisha yako. unapoondokana na hofu, unajisikia vizuri kuhusu wewe, na wale wanaokuzunguka na changamoto yoyote inaonekana ni ndogo na inatatulika.
13. Kila mtu anapenda kushinda. Lakini hutashinda mara zote. Hakuna aliyewahi kushinda mara zote. Endelea kujiamini na furahia maisha. Kumbuka ni kama mchezo tu na kushindwa sio mwisho wa dunia. Iwe umeshinda au umeshindwa, endelea kufurahia maisha.
14. Kama kuna kitu ambacho unakitaka kweli basi kiendee, anza kukifanya. Acha kukiongelea, usiogope kushindwa. Kama utashindwa, jifunze na anza tena kufanya. Hivi ndivyo walivyofanikiwa sana wamekuwa wakifanya.
15. Wasaidie wengine ambao wanapitia nyakati ngumu. Wanaweza kuwa wanajisikia wapweke. Unapomsaidia mtu, unakuwa umepata rafiki wa maisha. Unapomtia mtu moyo na kumwona akikua na kufanikiwa inakupa kuridhika. Mara zote kuwa wa msaada pale unapoweza, hutajutia hili.
16. Unaweza kujifunza mambo mengi sana kwa kusikiliza tu. Lakini watu wengi sio wasikilizaji. Kila mtu anataka kuongea na kama haongei anasubiri zamu yake ya kuongea, hasikilizi kwa makini.. jifunze kusikiliza bila ya kukatisha, utashangazwa na jinsi utakavyojifunza vitu vingi kwa kusikiliza tu.
17. Usikubali muda wako umezwe na mikutano ambayo sio muhimu kwako. Unahitaji kuweza kutengeneza nafasi tupu kwenye maisha yako kwa ajili yako wewe mwenyewe. Angalia mambo yote ambayo unayafanya na sio muhimu sana, kisha acha kuyafanya.
18. Kwa sababu kila siku na kila unapokuwepo unajitangaza wewe mwenyewe, vaa vizuri, kuwa msafi na tembea kwa mwendo wa heshima. Kumbuka mtu anapokutana na wewe kwa mara ya kwanza anajitengenezea picha yako kwenye akili yake ndani ya sekunde tano za mwanzo. Hakikisha picha hii ni nzuri na itakayokuletea fursa nyingi zaidi.
19. Usijiumize sana, wewe ni binadamu na binadamu wanakosea. Huwezi kupatia kila mara, hakuna ambaye amewahi kufanya hivyo. Kuna fursa nyingine nyingi ambazo bado ziko mbele yako, usikatishwe tamaa na kosa moja ulilofanya.
20. Jitahidi usiwe mtu ambaye anatoa taarifa mbaya. Hata kama unatoa taarifa tu, watu hawapendi taarifa mbaya na hivyo wanamchukia hata anayeleta taarifa mbaya. Kuwa mtu wa kutoa taarifa nzuri, na hata kama unatoa mbaya basi zitoe kwa njia ambayo inaweza kuwa nzuri.
21. Kuwa makini sana na kile unachosema au kuandika. Teknolojia imeleta mabadiliko makubwa sana kwenye maisha ya sasa. Huwezi kujua ulichosema au kuandika kinaweza kutumika wapi. Watu wanaweza kukurekodi na kutumia kama ushahidi. Kuwa makini sana.
Hayo ni muhimu sana kati ya mengi niliyojifunza kwenye kitabu hiki. Naamini kuna mengi umejifunza hapo, anza kuyafanyia kazi mara moja.