Unajua kwa nini watu wanaocheza kamari huishia kuwa na uteja? Wanaendelea kucheza licha ya kwamba wanapoteza fedha nyingi kuliko wanazopata? Ni kwa sababu ya uzoefu wao, huo ndio unaowapoteza zaidi.

Kama mtu akianza kucheza kamari na kila siku akawa analiwa tu fedha, hajawahi kupata hata siku moja, hataendelea kwa muda mrefu, ataacha. Lakini kama akicheza na siku moja akapata fedha kiasi, tayari anakuwa na uzoefu kwamba anaweza kupata fedha. Hivyo ataendelea kucheza hata kama analiwa fedha kwa sababu ana uzoefu wa kupata, hivyo ataamini japo kwa sasa analiwa ila baadae atakula na yeye, si tayari ana uzoefu?

Sasa hii haiishii kwa wacheza kamari tu, bali ni tabia yetu sisi binadamu wote.

Binadamu huwa tunapenda kutumia uzoefu wetu kuendelea kufanya au kutokufanya jambo. Kama tumewahi kufanya jambo fulani na tukipata majibu mazuri basi moja kwa moja tunahusisha tulichofanya na matokeo hayo mazuri. Na kwa njia hii tutaendelea kufanya jambo hilo tukiamini kupata tena mambo mazuri hata kama kwa sasa hatupati kile tulichotegemea kupata.

Wakati mwingine uzoefu wetu huu unatuzuia kuchukua hatua kwa sababu tu huko nyuma tulichukua hatua na kupata majibu ambayo hatukutarajia. Hivyo mpaka leo tunaamini kuchukua hatua fulani kunapelekea kupata hasara au kuumia.

Ufanye nini?

Kabla hujaendelea kufanya au kutokufanya kitu kutokana na uzoefu ulionao, simama na jiulize je uzoefu huu unahusiana moja kwa moja. Kupata majibu mazuri au mabaya kunaweza kusihusiane moja kwa moja na kile ulichofanya wewe. Inaweza kuwa matokeo yaligongana tu na kile ulichofanya, au mazingira fulani yalichangia ambayo kwa sasa hayapo. Au ilikuwa bahati tu na hivyo huwezi kurudia tena.

Tafakari kila ambacho umekuwa unafanya kwa mazoea ya matokeo uliyopata nyuma, na kama kwa sasa hupati matokeo yale uliyokuwa unapata au uliyowahi kupata licha ya kufanya ulivyokuwa unafanya, basi jua uzoefu wako unakurudisha nyuma, unakuzuia kusonga mbele zaidi.

Usikubali uzoefu wako uwe kikwazo kwako kupiga hatua, hoji kila mara na jaribu mambo mapya. Ulichopata jana sio lazima utapata leo au kesho, hata kama utafanya kile ulichofanya jana. Jiridhishe kabla ya kutegemea uzoefu ulionao.

SOMA; Swali moja muhimu sana ninalojiuliza kila siku asubuhi.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba uzoefu wangu unaweza kuwa kikwazo kwangu kufikia mafanikio makubwa. Sio lazima nilichofanya jana kikaleta matokeo fulani, na leo kitaniletea matokeo hayo pia. Nitaanza kuhoji kila uzoefu niliobeba ambao kwa sasa hauniletei yale matokeo niliyokuwa napata awali. Na nitaendelea kujaribu mambo mapya ili kuendelea kupata matokeo bora zaidi.

NENO LA LEO.

“Life is a succession of lessons which must be lived to be understood.”
― Ralph Waldo Emerson

Maisha ni muendelezo wa masomo ambayo lazima uyaishi ili uweze kuyaelewa.

Usikubali uzoefu wa nyuma ukuzuie wewe kufanikiwa zaidi leo na kesho. Jaribu mambo mapya kila wakati.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.