Ni hivi, juhudi unazohitaji kuweka ni sawa, iwe unataka kuwa na maisha bora au unataka kuwa na maisha ya hovyo.

Yaani unahitaji kuweka juhudi zile zile kwenye chochote utakachochagua, iwe ni kuwa na maisha bora au kuwa na maisha ya hovyo, iwe ni kuwa tajiri au kuwa masikini.

Kwa maneno mengine, juhudi unazohitaji kuweka ili uwe tajiri, ndio juhudi hizo hizo unazohitaji kuweka ili uwe masikini. Sema tu uelekeo wa juhudi ndio unabadilika.

Hii ina maana kwamba ili uwe na maisha bora, ili uweze kufikia mafanikio unayotazamia, unahitaji kuweka juhudi. Na pia ili uwe na maisha ya hovyo, ili ushindwe kufikia mafanikio unayotazamia, unahitaji pia kuweka juhudi.

Najua hii unaweza usielewe hasa kwa mara ya kwanza, kwa sababu unaweza kuona wanaotaka maisha bora wanaweka juhudi kubwa zaidi kuliko wale wanaopata maisha ya hovyo. Lakini ukweli ni kwamba wote wanaweka juhudi sawa, ila juhudi hizi zinatofautiana.

Kwa mfano, wakati mtu anayetaka kuwa na maisha bora akijifunza kwa kusoma vitabu, unafikiri yule anayekuwa na maisha ya hovyo anakuwa amepumzika? Hapana, anakuwa amekaa anaangalia tv, au anazunguka kwenye mitandao ya kijamii siku nzima, hii nayo ni juhudi.

Wakati anayefanikiwa akifikiria ni njia gani atumie ili kuongeza thamani ya kile anachofanya, akitafuta jinsi ya kwenda hatua ya ziada, anayeshindwa anakuwa anafikiria ni njia gani atumie kutoroka kazi yake, ni sababu gani atoe ili aonekane ilikuwa nje ya uwezo wake, hii nayo ni juhudi kubwa.

Wakati anayefanikiwa akiweka sehemu ya kipato chake pembeni na baadae kuwekeza, anayeshindwa anakazana kutumia kipato chake chote kwenye mambo ambayo sio muhimu, zote hizi ni juhudi.

Hivyo rafiki yangu kama umekuwa unafikiri hufanikiwi kwa sababu huweki juhudi, sio kweli, umekuwa unaweka juhudi, ila ni za upande wa pili. Uzuri ni kwamba unaweza kubadili juhudi hizo sasa na ukaanza kufurahia maisha ya mafanikio. Maisha ni yako na uchaguzi ni wako. Chagua kuweka juhudi ambazo zitakupeleka kwenye mafanikio.

SOMA; Malengo matano muhimu ya kibiashara ya kuweka kwa mwaka 2016.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba juhudi ninazohitaji kuweka ili kufanikiwa ni sawa na juhudi ninazohitaji kuweka ili kutokufanikiwa. Tofauti ni kwamba juhudi hizi zina uelekeo tofauti. Mimi nimechagua kuweka juhudi ambazo zitanipeleka kwenye maisha bora na yenye mafanikio. Sihitaji tena kupoteza muda wangu na nguvu zangu kwenye mambo ambayo sio muhimu kwangu.

NENO LA LEO.

“All the effort in the world won’t matter if you’re not inspired.”
― Chuck Palahniuk

Juhudi zote duniani hazitakusaidia kama hujahamasika.

Jua ni kitu gani hasa unachotaka na kisha weka juhudi kwenye kukipata kitu hiko. Usipojua unachotaka utaweka juhudi kwenye mambo yasiyo ya msingi.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.