Si Kila Anayekukosoa Hapendi Unachofanya, Jifunze Kupitia Mrejesho Hasi.

Habari mpenzi msomaji wa amka Mtanzania. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vyema na hasa katika siku hizi za mwanzo wa mwaka 2016. Nina imani ulipata nafasi ya kufanya tathmini ya mwaka 2015 , ukijifanyia tathmini kuona ni namna gani ulifanikisha yale malengo yako basi kama yalienda vizuri utakuwa na kila sababu ya kufurahia na kuzidi kujipanga kwa ajili ya hatua kubwa zaidi mwaka huu 2016, kwako wewe ambaye mambo hayajaenda kama vile ulitamani yawe, iwe ni changamoto kwako kukaa chini na kuangalia kwa nini ulishindwa kuyatimiza, pengine ni vyema kuangalia kama hayo malengo uliyoyapanga yanapimika? Tafuta kujua na kuelewa kwa nini hayakutimia, ili uweze kushughulikia kile kilisababisha ushindwe kufikia malengo yako mwaka wa 2015, lakini katika yote usikate tamaa bado unayo nafasi ya kurekebisha na kuanza vizuri na mambo yakawa vizuri kabisa.
SOMA; Mambo Kumi (10) Muhimu Ya Kufanya Ili Mwaka 2016 Uwe Bora Sana Kwako.

 
Ndugu zangu leo napenda kuzungumza na wale wenzangu na mimi ambao wanapenda kuambiwa tu maneno ya kufurahisha au habari wanazozipenda, zinazowafurahisha masikioni mwao tu, kuna baadhi ya watu iwe ni kwenye biashara yake au hata pale kazini ulipoajiriwa anataka aambiwe tu anafanya vizuri, au kama ni kule kwenye biashara asifiwe tu kila wakati, yule mama ntilie anataka asikie tu kuwa chakula ni kitamu sana, fundi cherehani anataka aambiwe tu asante umenishonea nguo vizuri sana, ndugu zangu naelewa kuwa kikawaida kila mtu anapenda kusifiwa au kuambiwa maneno ya kumtia moyo maana yanamfanya mtu ajisikie vizuri zaidi na sipo kinyume na hilo kabisa.
Lakini kwa mtu mwenye ndoto za kufika mbali, kama kweli unataka kufanikiwa kwenye kile unakifanya ni lazima uwe tayari kukutana na watu wa aina mbalimbali wenye mitazamo mbalimbali, maana tambua kuwa kila mtu anaweza kuona kitu kile kile kwa utofati, mwingine ataona chakula kitamu, mwingine atasema kibaya, huyu atasema chumvi inatosha na huyu atasema imezidi, hivyo ni wajibu wako wewe kuweza kuelewa aina ya watu unawahudumia ili iwe rahisi hata pale wanapotoa maoni hasi uweze kuyachukulia vyema na kukaa chini na kuyafanyia tathmini , baadhi ya watu hawapendi mtu amwambie kitu hasi, kwa mfano nimekuja dukani kwako kununua bidhaa na labda imeisha muda wake wa kutumia unataka nisikuambie na niichukue tu, nikikuambia ni shida sana, unaona kama nakuharibia au najidai najua sana n.k, 
Kuna mwingine ukimwambia tu labda chakula cha leo si kizuri kama cha jana au leo chumvi mmezidisha badala ya kukushukuru kwa kuwa mwaminifu na kumpa ule mrejesho wa huduma yake kwa siku hiyo, mtu mwingine atakuona kama adui usiyemtakia mema na mwingine anaweza kukukasirikia kabisa, anaacha kushughulika na yale maoni umempatia, yeye anashughulika na mtoa maoni, ni kama kushughulikia kisichohusika, kutoka nje ya msitari, nimekuambia chakula ni kibaya inabidi uangalie namna ya kuboresha ili usiweze kupoteza wateja wako.
SOMA; Kama Wewe Ni Mjasiriamali, Acha Kabisa Kuogopa Mambo Haya.
Lakini kwa mtu mwenye maono ya kufika mbali lazima awe tayari kupokea mrejesho kutoka kwa walaji wa bidhaa zake, na mrejesho waweza kuwa hasi au chanya hamna namna ya kuzuia hilo, lakini wakati mwingine mtu wa kukupa mrejesho chanya kila wakati naye si mwema sana, si mzuri sana maana anaweza kukufanya ukaridhika, ukajisahau ukaona kila kitu kipo sawa hivyo ukabweteka na kuacha kufikiria kufanya vizuri zaidi ya hapo, lakini huyu mwenye mrejesho hasi ukiuchukulia vizuri itakusaidia maana utaweza kufanyia kazi mrejesho wake kwa kupima na kuona yale yanayorekebishika na kuyarekebisha ili kuweza kuhakikisha kuwa haupotezi wateja wako na wengine wanazidi kumiminika kila leo na mwisho wa siku lazima utafanikiwa, wanaotukosoa kuna wakati wanatusaidia sana tu hata zaidi ya wanaotusifia muda wote, kumbuka mwingine anaogopa kukukosoa kwa kuwa utakasirika, anaogopa kukukosoa ili msipoteze urafiki, japo rafiki wa kweli anatakiwa aseme ukweli tu hata kama ni mchungu.
Ndugu yangu wakati wowote kwenye shughuli zako kuwa tayari pia kupokea mrejesho hasi na usimwangalie mtoa mrejesho basi simama na kile amesema, kipime na ukiona ipo sehemu ya kuweka sawa fanya hivyo, ni kwa faida yako wewe na kile unafanya.
Makala imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255755350772

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: