Mwaka mpya unapoanza watu wengi huwa na mipango mikubwa na mizuri sana. Lakini wengi huishia njiani katika kutekeleza mipango yao hii kutokana na baadhi ya makosa wanayofanya kipindi cha mwanzo wa mwaka kwenye kuweka mipango yao hiyo.

Mwaka huu 2016 bado ni mchanga kabisa, na ndio wakati ambao watu wengi wanaweka malengo. Huenda wewe moja ya malengo yako ni kuanza biashara mwaka huu. Labda umekuwa kwenye ajira muda mrefu na unafikiri unahitaji kuwa na biashara. Au umemaliza masomo, umetafuta ajira hupati na umeamua kuanza biashara. Kwa vyovyote vile, kama umeamua kuingia kwenye biashara nakupa hongera sana. Kwa sababu biashara yako ndio njia pekee ya kujitengenezea kipato kinachoendana na juhudi zako.

Lakini kutaka au kupanga tu kuingia kwenye biashara hakutoshi kukuwezesha wewe kufanikiwa kupitia biashara hiyo. Kuna mambo muhimu sana ambayo unatakiwa kuzingatia ili usije kuishia njiani. Kwa kuzingatia haya utajihakikishia kusimama kibiashara mwaka huu 2016.

1. Anza kidogo.

Huenda una ndoto za kuwa na biashara kubwa sana, huenda unapanga kufikia watu wengi na kutengeneza faida kubwa kwenye biashara yako. Pamoja na ndoto hizo kubwa na nzuri ni vyema ukaanza kidogo. Anza kidogo hasa kama bado huna uzoefu, kwa kuanza huku kidogo utajifunza vitu vingi kuhusu biashara ambavyo kwa sasa bado hujavijua.

Hata uwe umejipanga vizuri kiasi gani, biashara zina changamoto ambazo ni lazima utazipitia. Hivyo kama wewe ni mgeni kabisa kwenye biashara, ni vyema ukajifunza kupitia changamoto hizi unapoanza kidogo na unavyozidi kukomaa uendelee kukuza biashara yako. kwa kuanza kidogo hata ukipata hasara haitakuumiza sana kama ungetaka kuanza kwa ukubwa.

2. Anza na wazo lolote unaloweza kwa sasa.

Kuna watu wengi wanataka kuanza biashara lakini kinachowakwamisha ni wazo. Wengi wamekuwa wakifikiri labda kuna wazo moja wakishalipata tu basi biashara ni mafanikio. Lakini huo sio ukweli, kama tulivyoona hapo juu kila biashara ina changamoto zake. Na hivyo kufikiri kuna wazo litakuwa rahisi ni kujidanganya.

Kitu muhimu kuzingatia kwenye wazo la biashara ni kuangalia kitu gani unapenda kufanya, mahitaji ya watu ni nini na unawezaje kuwatimizia mahitaji hayo. Au unaweza kuangalia watu wana matatizo gani na ukawasaidia kutatua matatizo yao. Au pia unaweza kuangalia biashara zinazoendeshwa sasa, zinakosa nini ambacho watu wanahitaji na ukaja na suluhisho la hiko kinachokosekana. Mawazo ya biashara yapo mengi sana, ni wewe kuamua unachukua lipi na kulifanyia kazi.

3. Jitoe kweli kweli.

Kama unaingia kwenye biashara kujaribu naweza kukushauri uache tu mara moja, kujaribu hakutakufikisha mbali. Pale changamoto zitakapobisha hodi na kukukuta wewe unajaribu zitakusumbua sana.

Kama umeamua kuingia kwenye biashara ingia kweli, weka juhudi kuhakikisha unakuza biashara yako na chukulia hiko ndio chanzo chako kikuu cha kipato. Usiingie kwenye biashara na ukafanya kwa mazoea, weka jitihada sana, weka ubunifu na kila siku fikiria njia za kuboresha zaidi biashara yako.

4. Kuwa na malengo ya ukuaji wa biashara yako.

Kuna watu wengi ambao wameingia kwenye biashara miaka kumi iliyopita na mpaka leo bado wako pale pale. Yaani biashara zao zipo kiwango kile kile na hazijakua na kuweza kuwapa uhuru. Sababu kubwa ya hili ni mtu kuingia kwenye biashara bila ya kuwa na mpango wa ukuaji. Na biashara inapokolea anakuwa amemezwa kabisa na biashara kiasi cha kushindwa kujua anawezaje kukua zaidi.

Wewe usifanye kosa hili, kuwa kabisa na mpango wa ukuaji wa biashara yako. jua kabisa miaka mitano ya biashara yako utakuwa wapi na biashara itakuwa imekua kiasi gani. Ni lazima siku zijazo uwe na uhuru kupitia biashara yako. yote hayo unaanza kuyapanga sasa hivi.

5. Jifunze kila siku.

Kama umeamua kuingia kwenye biashara maana yake umejiandikisha kwenye shule ambayo hakuna kuhitimu. Umechagua njia ya kujifunza maisha yako yote. Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi sana, njia pekee ya wewe kuweza kwenda na kasi hii ya mabadiliko ni kujifunza kila siku. Soma vitabu vya biashara, soma makala kama hizi za biashara, hudhuria semina za biashara na mafunzo mengine muhimu ya kibiashara.

Kadiri unavyojifunza ndipo utajua mbinu bora zaidi za kukuza biashara yako ikiwepo kuwafikia wengi zaidi, kuongeza mtaji, kupata wasaidizi bora na mengine mazuri.

Kama umechagua mwaka 2016 kuanza biashara basi nakukaribisha sana na pia nakutakia kila la kheri. Amua hakuna chochote kitakachokurudisha nyuma na karibu tuendelee kujifunza kila mara.