Kuna baadhi ya watu ambao kutokana na maisha waliyopitia wanaamini kufanikiwa sio muhimu kwenye maisha. Na hii pia inaathiriwa na maana ambayo wao wenyewe wameiweka kwenye mafanikio.
Naomba tukumbushane jambo moja muhimu, kufanikiwa ni jambo muhimu sana kwenye maisha yako, nasema tena ni jambo muhimu. Haijalishi maana ya mafanikio ni nini kwako, kama tu kufanikiwa ni kuwa bora kwenye maeneo ya maisha yako basi ni muhimu sana.
Na ni muhimu sio kwako tu, bali kwa wengine wengi ambao wanakuzunguka, na huu ndio msukumo mkubwa unaohitaji kwenye maisha yako.
Unapofanikiwa wewe unafungua milango kwa wengine wengi sana.
Kwanza kuna watu wataona kwamba inawezekana, na wao wataweka juhudi, na wao watafanikiwa pia. Huenda mwanzo walikuwa wanaambiwa kitu fulani hakiwezekani, na wao wakaamini. Ila watakapokuona wewe umeweza, itawapa hamasa ya wao kufanya pia.
Pili utatatua matatizo ya wengi. Kwa wewe kufanikiwa ni lazima kutokane na huduma fulani unayoitoa kwa watu wengine. Sasa kama utafanikiwa kwa njia hii ni dhahiri utaweza kutatua matatizo watu wengi zaidi.
Tatu utainua hali ya kila mtu. Tuseme labda upo kijijini, ambapo hakuna duka la bidhaa au huduma fulani. Wewe ukaanzisha duka, ukafanikiwa sana na kutatua matatizo ya wengi. Pale pia wengine watashawishika kuanzisha biashara nyingine ambazo bado hazijakuwepo kwenye kijiji hiko. Kwa njia hii utainua hali za watu wengi sana.
Narudia tena, fanikiwa, sio kwa sababu yako binafsi, ila kwa sababu kuna kundi kubwa la watu ambao watanufaika sana na mafanikio yako.
MUHIMU; Najua unaelewa ni mafanikio ya aina gani tunayozungumzia hapa, ni mafanikio ya wazi na sio ya kutumia mbinu ambazo sio halali.
SOMA; Mambo Matano Yatakayokuwezesha Kushirikiana Vizuri Na Watu Kwenye Kazi Na Kufikia Mafanikio Makubwa.
TAMKO LANGU;
Nimeamua kufanikiwa sio kwa sababu zangu binafsi tu, bali kwa sababu mafanikio yangu yatawasaidia watu wengi sana. Nimeshaamua sitarudi nyuma kwenye safari hii. Nimechagua hii kuwa safari ya maisha yangu.
NENO LA LEO.
Coming together is a beginning; keeping together is progress; working together is success.
Henry Ford
Kukutana pamoja ni mwanzo; kukaa pamoja ni maendeleo; kufanya kazi pamoja ni mafanikio.
Unapofanikiwa hunufaiki wewe tu, bali wengine pia wananufaika. Ni muhimu sana ufanikiwe.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.