Mfanyabiashara mkubwa unayemuona leo, hakuanzia hapo, alianza chini kabisa, kwa kupata hasara lakini leo unamwona ana biashara kubwa.
Mwanamuziki mashuhuri unayemuona leo, hakuanzia hapo alipo, alianza chini kabisa, nyimbo zake za kwanza watu hawakuzisikiliza.
Mwandishi mashuhuri unayemuona leo hakuanzia hapo, ukipewa andiko lake la kwanza usome unaweza kuona ni mtu ambaye hajui anachofanya.
Lakini watu hawa wamekuwa bora sana leo, baada ya muda kwenda.
Hii inatokana na kwamba waliamua kutokuwa wazuri, walikubali kwamba wao hawako vizuri na hivyo kufanyia kazi kile walichotaka mpaka watakapokuwa wazuri. Na wakawa wazuri, na kila mtu akapenda kile wanachofanya.
Ufanye nini?
Chochote kile unachotaka kuanza kufanya, najua mwanzo huu wa mwaka kuna vingi unataka kuanza kufanya, kubali kwamba wewe sio mzuri kwenye vitu hivyo. Na fanyia kazi hilo ukijua ya kwamba kadiri unavyoweka juhudi ndivyo utakavyokuwa mzuri.
Unapokubali kwamba wewe sio mzuri, hata unapokutana na changamoto kubwa na ikapelekea kushindwa, hutakata tamaa kwa sababu unajua hukuwa mzuri na changamoto hiyo ni sehemu ya darasa unalohitaji ili kukua zaidi.
Amua leo na kubali kwamba hauko vizuri kwenye chochote unachoanza kufanya, na weka juhudi kuhakikisha kwamba unakuwa mzuri sana kwenye eneo hilo.
Kumbuka dunia haitakuvumilia kwa muda mrefu kama hutakuwa mazuri, hivyo weka juhudi kubwa kuhakikisha unakuwa mzuri kadiri siku zinavyozidi kwenda.
SOMA; Mambo Kumi Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Matumizi Yako Ya Fedha Ili kuweza Kufiki Uhuru Wa Kifedha.
TAMKO LANGU;
Nimekubali kwamba kile ninachokwenda kuanza kufanya sipo vizuri, na hivyo najitoa kuhakikisha kadiri siku zinavyokwenda nakuwa vizuri sana. Sitarudishwa nyuma na changamoto yoyote kwa sababu najua changamoto ni sehemu nzuri sana ya mimi kujifunza.
NENO LA LEO.
Every Pro was once an amateur. Every expert was once a beginner. So dream big. And start now.
Kila mtaalamu alianza bila ya kujua. Kila aliyebobea alianzia chini kabisa. Hivyo kuwa na ndoto kubwa. Na anza kuzifanyia kazi sasa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.