Wazungu wanasema MIND YOUR OWN BUSINESS, yaani jali shughuli zako mwenyewe.

Lakini wengi tumekuwa tunajali sana kuhusu shughuli za wengine, hasa pale ambapo tunahisi zinahusiana na sisi.

Na tumekuwa tunaingilia kazi za wengine, na hili limekuwa linaturudisha nyuma sana.

Mfano wa kazi za wengine ambazo tumekuwa tunaingilia;

Kuna watu wanaitwa wakosoaji, hawa kazi yao ni kukosoa tu. Kwa lolote ambalo utafanya hawakosi kitu cha kukosoa. Ukitoa msaada kimya kimya watasema mbona hatumwonagi akitoa msaada. Ukitoa msaada na kutoa taarifa watasema msaada wa kweli hautakiwi kujionesha. Elewa hii ni kazi ya watu na hivyo usijisumbue kwa nini watu wakosoe kila kitu.

Kuna watu ambao wana chuki, na kazi yao ni kuchukia kila kitu au kila mtu ambaye anaonekana kwenda juu kuliko wao. Watu hawa watakuchukua tu bila sababu yoyote. Hujawahi kuwafanyia jambo lolote baya lakini wanakuchukia tu. Hawa ni wale ambao wakisikia umepata matatizo wanasema safi sana. Acha watu hao wafanye kazi yao, na wewe kazana kufanya kazi zako.

Kuna watu ambao ni wakatishaji tamaa. Watu hawa wao walishakata tamaa zamani sana na wanahakikisha kila anayewazunguka naye anakata tamaa. Hivyo watakazana kila kona kukukatisha tamaa. Wewe achana nao mara moja, usiingilie kazi yao, usitake kubishana nao kwamba inawezekana, wao wameshachagua hiyo ndiyo kazi yao, wewe songa mbele.

Kwa nini usiingilie kazi hizi za wengine?

1. Kwa sababu kwa kufanya hivyo unapoteza muda wako, ambao ungeutumia vizuri kupata kile ambacho unataka kwenye maisha yako.

2. Huwezi kuwabadili watu wa aina hii, wameshachagua wanachotaka kufanya na hivyo hata kama utawaonesha ni vibaya kiasi gani wanavyofanya, hawawezi kukuelewa. Hivyo okoa muda wako na utumie kufanya vitu ambavyo ni muhimu kwako.

MUHIMU; Kama na wewe upo kwenye moja ya makundi hayo ya kazi, chukua hatua ambayo ni stahili kwa maisha yako.

SOMA; Kama Unayapigania Mafanikio, Watu Watakuchukia, Usiumizwe na Hilo.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kuna watu ambao ni kazi yao kabisa kuhakikisha wengine hawasongi mbele. Na njia ya kusonga mbele pale ambapo umezungukwa na watu hawa ni kutokuingilia kazi zao. Nitatumia muda wangu vizuri kuhakikisha napata kile kilicho bora, huku nikiacha hao wakiendelea na mambo yao mengine.

NENO LA LEO.

Haters keep on hating, cause somebody’s gotta do it.

Chris Brown

Wenye chuki wataendelea kuchukia kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao.

Usipoteze muda wako kujaribu kuingilia kazi hizo za watu. Badala yake wekeza nguvu na muda wako kwenye kuwa bora zaidi. Acha wengine wafanye mambo yao.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.