Moja ya vitu ambavyo wewe kama rafiki yangu nakusihi sana uache ni kujidanganya.
Ndiyo umekuwa unajidanganya sana, huenda unajidanganya ukijua au mara nyingi unakuwa hujui, ila umekuwa unajidanganya sana. Na hilo limekuwa linakugharimu kwa kiasi kikubwa sana, na kukuzuia kufikia mafanikio.
Kuna mambo ambayo umekuwa unataka na kuamini unatakiwa kuyapata ila kwa bahati mbaya sana hayajawahi kutokea kabisa duniani.
Unataka uanze biashara leo, wateja wajipange kugombania biashara yako, upate faida kubwa sana na biashara ikue haraka haraka kama uyoga.
Unataka uanze kazi leo, na kwa haraka sana upandishwe vyeo, upate mshahara mkubwa, uwe na majumba na magari.
Unataka maisha yaende kama vile ambavyo ungependa yaende kwenye akili yako, na kama chochote kitakwenda tofauti na unavyotaka unaona dunia haipo sawa.
Ukweli ni kwamba una haki kabisa ya kuwa na ndoto kubwa sana, una haki ya kupata mafanikio makubwa, lakini unachotakiwa kujua ni kwamba mambo hayatakuja kirahisi kama unavyofikiria. Utakutana na changamoto nyingi sana, ambazo zitakufikisha kwenye hatua ya kukata tamaa na kuacha. Hapo ndipo kwenye kipimo muhimu sana kama kweli umejipanga kupata au unafanya tu kwa kujaribu.
Ni muhimu ujue kuanzia mwanzo kabisa, japo utaingia kwenye biashara ukiwa umejipanga, japo una wazo bora kabisa la biashara, bado mambo hayatakwenda kirahisi, ni lazima utakutana na changamoto, nyingine hata hukuzitegemea.
Hakuna maisha ya mteremko, na kama kuna ambao unaona wana maisha ya mteremko na hivyo kukuhamasisha sana, hujawaua vizuri wanapitia nini au hapo awali walipitia nini.
Jiandae kwa hali ngumu, na hii itakupa nguvu ya kupambana na kukuzuia kukata tamaa. Kama utaendelea na mawazo yako ya kujidanganya kwamba mambo yatakuwa rahisi na kupata unachotaka, unajiandaa kushindwa na kukata tamaa kabisa.
SOMA; Umuhimu wa changamoto kwenye maisha yako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba maisha niliyokuwa nafikiria sio uhalisia, nimekuwa najidanganya kwa kutokukubali mapema kwamba mambo sio rahisi kama ninavyofikiria. Kuanzia sasa nitajiandaa kwa hali ngumu kwa jambo lolote ninalokwenda kufanya, hii itanisaidia kupambana na changamoto nitakazo kutana nazo na pia kunizuia nisikate tamaa.
NENO LA LEO.
Success is never owned, it’s rented. And the rent is due everyday.
Mafanikio hayamilikiwi, bali yanakodishwa. Na kodi yake inalipwa kila siku.
Hakuna njia ambayo ni rahisi kufikia mafanikio, kila siku unahitaji kupambana, kila siku unahitaji kuvuka changamoto ndio ufikie mafanikio unayotaka. NI KILA SIKU.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.