Katika maisha yako, kuna maeneo ambayo una nguvu ya kufanya kitu au kuleta mabadiliko, na kuna maeneo ambayo huna nguvu kabisa.

Kama jinsi ambavyo tunajua, maana tumekuwa tunajifunza sana hapa, hasa kupitia FALSAFA MPYA YA MAISHA, kila kinachotokea kwenye maisha yako kina kisababishi. Hakuna kitu kinachotokea kwa bahati mbaya, kila kinachotokea kimesababishwa.

Hivyo kwenye kila kisababisho kwenye maisha, kuna matokeo yake. Matokeo unayopata leo yametokana na vitu ulivyofanya/ ulivyosababisha siku zilizopita. Hakuna kinachotokea kwako leo kwa bahati mbaya au nzuri, uliwahi kusababisha kwa namna moja au nyingine siku zilizopita.

Kama biashara yako unapata hasara leo, siku za nyuma kuna wakati hukuweka umakini kwenye biashara yako. kama kazi yako inakusumbua leo, siku za nyuma kuna wakati ulizembea kwenye kazi yako. na kama unapata matokeo mazuri maana yake ulifanya mazuri huko nyuma.

Sasa changamoto kubwa inaanzia hapa, watu wengi wanakazana kubadili matokeo. Na ndio maana tunajifunza hapa leo.

Unaweza kubadili unachofanya/ kisababishi lakini huwezi kubadili matokeo, huwezi kabisa, usijidanganye tena kwa hilo. Kama umezembea kwenye biashara yako, subiri matokeo yake yanakuja, na badala ya kukazana na matokeo hayo, ni vyema ukakazana kubadili kile ambacho unafanya.

Kama uliwahi kuwa mwizi huko nyuma, matokeo ya wizi wako yanakuja, huwezi kuyabadili. Ila unaweza kubadili matokeo ya siku zijazo kwa kuacha kuiba sasa. Lakini kuacha kuiba leo hakutazuia yale matokeo ya ulipoiba nyuma kutotokea. Ni lazima yatatokea kwa sababu huwezi kuidanganya dunia, na deni lolote ni lazima utalipa.

Usihangaike na kubadili matokeo, huna nguvu hiyo, hangaika na kubadili kile unachofanya, hangaika na kubadili tabia yako, hangaika na kubadili mawazo na mtizamo wako na hangaika na kubadili imani yako. hivi vina mchango mkubwa kwa hatua unazochukua.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Huwezi Kuidanganya Dunia, Acha Kujidanganya.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba naweza kubadili kile ninachofanya mimi, lakini siwezi kubadili matokeo. Nikishafanya kitu, matokeo ni lazima yatakuja, yanayoendana na kile ambacho nimefanya. Njia pekee ya mimi kupata matokeo bora ni kuanza kufanya kile ambacho ni bora. Kuanzia sasa nimeamua kufanya kile ambacho ni bora ili kutengeneza matokeo bora sana ya baadaye. Najua siwezi kuidanganya dunia, na kila deni nililosababisha nitahitajika kulilipa.

NENO LA LEO.

While we are free to choose our actions, we are not free to choose the consequences of our actions. – Stephen R. Covey

Tuna uhuru mkubwa wa kuchagua matendo yetu, lakini hatuna uhuru wa kuchagua matokeo ya matendo yetu.

Ukishafanya kitu, subiri matokeo, na usihangaike kubadili matokeo, bali hangaika kubadili kile unachofanya. Ukifanya mazuri unapata matokeo mazuri.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.