Habari za leo rafiki?
Naamini uko vizuri sana na unaendelea na harakati zako z akuboresha maisha yako zaidi. Najua mwaka 2016 ndio unaanza kukolea na nina hakika bado una ule moto wa malengo ambayo umejiwekea kwa mwaka huu 2016.
Kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho kuhusu maisha yako ni kwamba unataka kuwa na maisha bora, na unataka yawe bora zaidi ya yalivyo sasa. Hilo halina ubishi. Vitu vyote unavyofanya, viwe vizuri au vibaya, ni kwa lengo kuu moja, kuwa na maisha bora, maisha ya furaha na ya mafanikio.
Lakini kikubwa ambacho kinakuzuia wewe kufikia yale maisha bora unayotaka ni kukosa maarifa sahihi ya kukufikisha kwenye maisha hayo. Tunaishi kwenye dunia ambayo ina kelele nyingi sana, na sehemu kubwa ya kelele hizi hazina mchango wowote kwenye maisha yako. pia tunaishi kwenye jamii ambayo kila mtu anafanya kile ambacho wengine wanafanya, na hivyo hata wanapokamilisha kufanya, bado hawaoni maisha yao yamebadilika.
Hivyo kitu kingine ambacho nina uhakika nacho kuhusu wewe ni kwamba unahitaji kujifunza kitu, kila siku, narudia tena KILA SIKU ambacho kitakuwezesha wewe kuishi yale maisha ya furaha na mafanikio kwako. Kila siku mpaka utakapoiaga dunia unahitaji kujifunza kitu kipya ambacho kitakuwezesha kufanya mabadiliko kwenye utendaji wako, kwenye jinsi unavyoichukulia dunia, kwenye jinsi unavyotatua changamoto unazokutana nazo.
Na kwa bahati mbaya sana huwezi kupata sehemu hiyo ya kujifunza mambo hayo mazuri kila siku.

 
Tarehe moja mwezi wa kwanza mwaka 2015 nilianza kuandika KURASA 365 ZA MWAKA 2015. Lengo ilikuwa ni kuandika kitu kila siku kwenye siku 365 za mwaka ule 2015. Na ninashukuru sana kwa sababu lengo lile limetimia kwa asilimia 100. Na sio tu kutimia bali wengi wameniandikia ni kwa jinsi gani kurasa zile zimekuwa na msaada kwenye maisha yao, kazi na biashara zao.
Baada ya mafanikio yale makubwa ya KURASA 365 ZA MWAKA 2015, sasa nakukaribisha kwenye kitu kingine kikubwa zaidi na hiki ni KURASA ZA MAISHA.
Karibu kwenye KURASA ZA MAISHA.
Kurasa za maisha ni mwendelezo wa kurasa 365 za mwaka 2015. Katika kurasa za maisha, kama ilivyokuwa kwenye kurasa 365, tunachukulia maisha yako kama kitabu unachoandika na kila siku mpya ni ukurasa mpya, ambao wewe unaandika kitu, kutokana na yale ambayo unayafanya. Kwa kuchukulia maisha kama kurasa, tunaweza kuishi siku moja kwa ukamilifu na kuhakikisha siku hii inakuwa ni siku ya kumbukumbu kwenye maisha yetu. Hatutakubali tena kupoteza muda kwa sababu tunajua kila siku ina hesabu yake.
Kupitia KURASA ZA MAISHA, kila siku utapata makala nzuri na fupi ambayo itakupa maarifa, itakubadili mtazamo na itakuwezesha kutafakari zaidi kuhusu maisha yako. makala hizi kama utazisoma kila siku na kufanyia kazi yale unayojifunza, maisha yako hayawezi kubakia pale yalipo sasa.
Maboresho zaidi kwenye KURASA ZA MAISHA.
Kwenye makala hizi za kurasa za maisha, kuna maboresho zaidi ili kuhakikisha ya kwamba unapata maarifa kamili yatakayoyafanya maisha yako kwa ujumla kuwa bora zaidi. Na hivyo tutakuwa tunajifunza yale maeneo yote muhimu yanayokamilisha maisha yetu.
Maeneo hayo ni;
1. Fikra, hapa tutakuwa tunapata makala za kubadili fikra zetu na kuzifanya kuwa chanya.
2. Afya, hapa tutakuwa tunajifunza pia kuhusu afya zetu, maana ni msingi muhimu sana kwa maisha ya mafanikio.
3. Mahusiano, haya yanahusika sana kwenye maisha yetu, mahusiano na familia, ndugu, jamaa na marafiki na hata wale tunaofanya nao kazi au biashara.
4. Imani, pia tutakuwa tunapata makala za kutuwezesha kuboresha zaidi imani zetu.
5. Mafanikio, hapa tutayazungumzia mafanikio kwa ujumla, na mambo yote yanayohusiana na mafanikio.
Pia kutakuwa na mengine mengi sana ya kujifunza kuhusu maisha.
Jukumu lako wewe ni kuhakikisha kila siku asubuhi kabla hujaianza siku yako, unapita kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unasoma UKURASA wa siku husika na kutafakari unawezaje kuutumia kwenye maisha yako.
Hii ni njia bora sana ya kuianza siku yako, kwani utaianza na mtazamo chanya na kuwa na hamasa ya kuweka juhudi zaidi. Kuliko uianze siku na habari hasi, ambazo hazina mchango wowote kwenye maisha yako, ni vyema ukaianza siku yako na makala ya KURASA ZA MAISHA.
Nimejitoa kuhakikisha kila siku nakuletea makala hizi za kurasa, lengo langu ni kuweza kuandika kila siku, mpaka siku ninayoondoka hapa duniani. Nitajitahidi kuvuka changamoto yoyote itakayozuia hili, na sitakubali sababu yoyote inizuie kukuletea wewe makala za kurasa kila siku.
Karibu twende pamoja kwenye safari hii ya kuwa na maisha bora zaidi kila siku. Maana safari hii haina mwisho wala kilele, ni kitu cha kufanya kila siku kama bado unaishi.
Kila siku unapoamka asubuhi, ingia kwenye KISIMA CHA MAARIFA, www.kisimachamaarifa.co.tz na usome makala ya ukurasa wa siku husina, na hata makala za kurasa za nyuma na makala nyingine za KISIMA CHA MAARIFA.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
0717396253