Nilipokuwa nasoma sekondari, nilikuwa napenda sana somo la hesabu. Usijali kama ulikuwa hulipendi, leo nitakuelekeza kidogo sana, ili tuweze kwenda pamoja.

Wakati tupo kidato cha pili, mwalimu wetu wa hesabu alikuwa akitoa mitihani, alikuwa ana mtindo tofauti wa kusahihisha. Kwa somo la hesabu lilivyo, njia unayotumia kufikia jibu lako ina maksi zake na jibu pia lina maksi zake. Hivyo hata ukikosa jibu, bado utapata maksi kwenye njia uliyotumia.

Sasa huyu mwalimu wetu alikuwa anasahihisha jibu kwanza, kama umepata ndio anakupa maksi kwenye njia, kama umekosa jibu basi hahangaiki na njia. Tukamlalamikia kwamba kwa njia hiyo ya usahihishaji anawanyima watu maksi zao kwenye njia. Baada ya kutusikiliza alitupa kauli moja, NJIA YA KWELI INALETA MAJIBU YA KWELI, kama jibu hata halikaribiani na ukweli sina haja ya kuangalia njia, maana ni ya uongo.

Kwa kipindi kile sikumwelewa, ila kadiri ninavyokwenda na maisha naona ni jinsi gani ilivyo dhahiri kwenye maisha ya kila mmoja wetu. Njia ya kweli inaleta majibu ya kweli. Na tukienda mbele zaidi, njia ya kweli ni moja tu, lakini njia za uongo ni nyingi, na ndio maana zinawapoteza wengi.

Turudi darasani kidogo, kwa somo la hesabu.

2 + 5 X 6/3 = __(kabla hujaangalia jibu hapo chini, jaribu kufanya mwenyewe)

Yaani mbili, jumlisha tano, mara sita gawanya kwa tatu jibu ni?

Kuna njia moja tu ya kweli ya kupata jibu la kweli hapo, na kuna njia nyingi za uongo za kupata jibu la uongo.

Njia ya kweli ni MAGAZIJUTO, unaanza kufungua mabano, unagawanya, unazidisha, unajumlisha halafu unamaliza na kutoa. Kwa mtiririko huo unapata jibu sahihi ambalo hapo litakuwa 12. (wewe umepata ngapi?)

Kwa njia nyingine nyingi za uongo utapata majibu haya, 14, 9, 13 na mengine mengi, kulingana na njia ya uongo uliyotumia.

Sasa turudi kwenye funzo letu la leo, pole kama hesabu hiyo imekuwa ngumu kwako.

Katika maisha njia ya ukweli huwa ni moja, njia ya kufanikiwa huwa ni moja, lakini njia za kushindwa huwa ni nyingi sana. Na njia hizi huwachanganya wengi na kufikiri ni za kweli. Tena wanaweza kulalamika kabisa mbona wanafanya kila wanachotakiwa kufanya lakini hawapati matokeo waliyotegemea kupata? Kabla hujaendelea kulalamika kumbuka kwamba aliyepata jibu 14 kwenye hilo swali hapo juu ametumia njia ya kihesabu kabisa, lakini sio njia ya kweli.

Ni muhimu sana ujichunguze kama kweli uko kwenye njia ya kweli ambayo itakufikisha kwenye mafanikio unayotarajia, na weka juhudi sana kuhakikisha unapata yale matokeo unayotarajia kupata.

Na njia ya kweli inaanza na kile ambacho unapenda kukifanya, na ukakifanya kwa moyo mmoja, ukajituma sana, ukawa na nidhamu, ukawa mvumilivu, ukawa mwaminifu, ukawa mwadilifu na ukagoma kukata tamaa.

SOMA; Kama Maisha Ni Vita, Basi Huu Ndio Ukweli Unaotakiwa Kujua.

TAMKO LANGU;

Nimejifunza kwamba kabla sijalalamika kwa nini sipati majibu ninayotaka, ni muhimu nikachunguza kama njia ninayotumia ni njia ya kweli. Kwa sababu njia ya kweli inaleta majibu ya kweli, na njia ya kweli ni moja tu, ila za uongo ni nyingi na zinavutia sana. Nitaifuata njia ya kweli na kuhakikisha nakomaa nayo mpaka nipate kile ninachotaka.

NENO LA LEO.

Three things cannot be long hidden: the sun, the moon, and the truth.

Buddha

Kuna vitu vitatu ambavyo haviwezi kufichwa kwa muda mrefu; jua, mwezi na ukweli. Hata ukikazana kuvificha lazima itafika wakati na vitakuwa wazi.

Ujue ukweli kwako na ishi ukweli huo. Njia ya ukweli ni moja na inaleta majibu ya kweli. Njia za uongo ni nyingi na zinashawishi sana. Kuwa makini.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.