Habari Msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu. Kwanza kabisa heri ya mwaka mpya, ni matumaini yangu umeuanza mwaka vizuri kabisa. Uchambuzi wetu wa kwanza kwa mwaka huu 2016 unaangazia maswala ya mahusiano. Hivyo basi tutachambua kitabu kizuri sana kinachoitwa The DNA of Relationships. Kitabu hiki kimeandikwa na mtaalamu wa maswala ya mahusiano Dr.Gary Smalley akishirikiana na waandishi wengine watatu, wawili kati yao ni watoto wake wa kuwazaa (Dr. Greg Smalley na Michael Smalley) na rafiki yake anayeitwa Dr. Robert S. Paul. Waandishi wote wana uzoefu wa kutosha kwenye maswala ya mahusiano na wamefanyika msaada mkubwa katika ndoa nyingi. 

 
Kitabu hiki kinaitwa DNA of Relationships, kwa nini kiitwe hivyo, kwanza tuone nini maana ya DNA (Deoxyribonucleic Acid), DNA kwa Kiswahili inajulikana kama VINASABA, ambapo vinasaba ni utambulisho wa kipekee wa kila kiumbe ambao unabeba taarifa muhimu na inayorithisha tabia au umbile fulani la mhusika. Vinasaba pia inaweza kuelezewa kama kitabu cha kumbukumbu kinachohusu maisha binafsi. Katika Kitabu hichi Cha DNA of Relationships kinachambua mambo ya msingi katika mahusiano, tena kwa misingi ya Neno La Mungu (Biblia) ndio maana kikaitwa vinasaba vya mahusiano.
Waandishi wanaelezea kwamba maisha ni mahusiano, na kila mmoja wetu alizaliwa ili kua kwenye mahusiano (Mahusiano ya kindugu, mahusiano ya kirafiki au mahusiano ya kindoa). Kitabu hiki kinazungumzia zaidi mahusiano ya kifamilia ( mwanaume, mwanamke na watoto). Kwa ujumla wake kitabu kinaweka misingi ya mahusiano, jinsi ya kuweza kukabiliana na changamoto za mahusiano na jinsi ya kuboresha mahusiano yako yaweze kunawiri kila kukicha. Maisha ni mahusiano, mengine ni maelezo tu. Mungu amekuumba kwa ajili ya mahusiano Hilo huwezi kulibadili.
Karibu tujifunze zaidi
1. Mahusiano sio jambo la hiari. Tangu tulipozaliwa tulikua na mahusiano na wazazi na ndugu wengine. Baadae tukaanza kuhusiana na watoto wengine. Tulivyoendelea kukua tukaanza kuwa na mahusiano shuleni, katika sehemu za kazi, na kujikuta tukitengeneza mahusiano na marafiki zetu wa karibu. Hatimaye watu hutengeneza mahusiano na wale wawapendao sana. Hii ina maana huwezi kuepuka mahusiano, lazima tu utahusiana.
2. Wakati mahusiano yanapokua magumu na yenye maumivu, hua tunapenda kuyakatisha mahusiano yale, na hata kujaribu kuyatupilia mbali kwa muda mahusiano yote. Lakini hujikuta tumerejea na kutafuta kujiunganisha tena. Japokuwa tunaweza kuchagua jinsi ya kushiriki kwenye mahusiano, hatuna uchaguzi kuhusu aidha kushiriki au kutoshiriki. Our only real choice is whether we will work to make our relationships healthy; whether we will do things that hinder or enhance them.
3. Kufanya uchaguzi hua ni kugumu maana kunahitaji badiliko, na badiliko hilo linaweza kua lenye kuogofya. Kutokuchagua kwenyewe ni uchaguzi. Unapoahirisha kufanya uchaguzi basi ujue unafanya uchaguzi. Usikubali kua mtumwa au mhanga wa wakati uliopita. You have to change. Even when the change is scary
4. Migogoro mingi katika mahusiano inasababishwa na mambo mawili ya msingi, kwanza kuhisi kwamba hupewi umuhimu wa kutosha au unaostahili ( hii ipo hasa kwa wanawake), pili ni kuhisi unataka kudhibitiwa au kutawaliwa (hii hasa iko kwa wanaume).
5. Yatazame mahusiano yako kwa lensi ya jicho la Kimungu. Ili mahusiano yako yawe na afya pata lensi ya Kimungu kuhusu mahusiano. Je Mwongozo wa Kimungu kuhusu mahusiano unasemaje? Jitazame kama Mungu anavyokutazama, Mtazame huyo mwenza wako kama Mungu anavyomtazama, pia yatazame mahusiano yenu kama Mungu anavyowatazama.
SOMA; Viungo Vikuu Vitatu(3) Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha.
6. Tatizo la nje mara chache sana hua linakua ndio tatizo halisi. Kwa maneno mengine kile kinachoonekana kua tatizo hua sio tatizo. Mfano kama mwenzako hua anapenda kufoka , tatizo sio kufoka. Ni kitu gani hicho kinachomfanya awe anafoka? Pengine anahisi hajapewa umuhimu unaostahili. Au pengine anaona hapewi heshima yake, au hapendwi inavyopaswa. Jitahidi kufahamu tatizo halisi ni lipi kisha ufanye kitu ili kutatua. Kutokufahamu tatizo halisi kutakuletea ugumu sana katika kutatua tatizo unaloliona kama tatizo.
7. Usitegemee mtu mwingine kua suluhisho lako. Unapofanya hivyo ni kuweka matarajio yako kwake na uwezekano wa kukatishwa tamaa ni mkubwa. Wewe ndiye suluhisho unalolitafuta. Don’t expect the other person to be your solution.
8. Kama bado unatarajia wengine wakufanye mwenye furaha basi ujue kwamba bado una utoto ndani yako, yaani bado hujakua, bila kujali una umri wa miaka mingapi. Waliokua tu ndio wanafahamu kwamba furaha ya kweli inatoka kwao binafsi na si kwa wengine. Furahia maisha yako, usisubiri ufurahishwe na wengine au na vitu.
9. Hakuna kilichopo nje ya Mungu kinachoweza kukuletea uzima, furaha na Amani. Ni utoto kudhani kwamba kitu fulani katika dunia hii kitakupatia utoshelevu na furaha ya kudumu. Mungu ndiye chanzo cha uzima/maisha, watu na vitu ni ziada tu.
10. Stress au msongo wa mawazo ni ombwe (gap) lililopo kati ya kile tunachotarajia kitokee na kile kinachotokea kiuhalisia. Kutegemeana na uzito wa matarajio yenyewe, tunaweza kuwa na stress kubwa au kidogo. Kwa kadiri matarajio yanapokua ya thamani ndivyo msongo wa mawazo unakua mkubwa pale unapotokea. Hebu jaribu kufikri watu wamepata hasara. Mtu wa kwanza awe na matarajio ya kutengeneza faida ya milioni 100 katika biashara yake halafu inatokea mambo yanakwenda kombo halafu haambulii hata shilingi mia. Mtu wa pili awe na matarajio ya kutengeneza faida ya laki moja halafu naye asipate hata mia. Je kati ya hao watu wawili nani atakua na msongo wa mawazo mkubwa?
11. Thamini utofauti uliopo kati yako na mwenzako. Watu wawili wanapokua kwenye mzozo, mara kadhaa huonyesha tofauti zao kama ndio tatizo. Lakini hilo sio kweli. Tofauti zenu ni Baraka kwenu, mnachopaswa kufanya ni kufahamu jinsi ya ku deal nazo na kuzifanya kua mtaji wa kusonga mbele. When we value our differences rather than make them the focus of our conflict, we create safety.
SOMA; Malengo Matano (5) Muhimu Kwako Kuweka Mwaka 2016 Ili Uwe Na Maisha Bora Sana.
12. Heshimu ukuta uliopo kati yako na mwenza wako. Watu wanapotendewa ndivyo sivyo hujenga ukuta kati yao na wale waliowatendea vibaya. Mfano kama umemtendea mwenza wako jambo baya, labda amegundua umemdanganya kwenye jambo fulani, atajenga ukuta au mpaka kati yake na wewe, hii ni kwa sababu anajihisi hayuko salama tena. Sasa wewe usifanye kosa kwa kutaka kulazimisha kuubomoa huo ukuta, yaani kwa kutaka kulazimisha kuleta ukaribu wa mwanzo, ukifanya hivyo utaharibu. Heshimu ukuta huo, kuheshimu ukuta huo ni kuonyesha kuwa unaheshimu hisia zake kwa wakati huo anapojihisi kukosa usalama. Unachopaswa kufanya ni kuomba msamaha na ujirekebishe, huku ukitengeneza mazingira ya kurudisha imani yake kwako ambapo huyo mwezako atajihisi salama tena, na kisha yeye ndiye atakayevunja ule ukuta mwenyewe. Create a safe environment in which the other person can gradually take down the wall.
13. Usiwe mwepesi wa kuhukumu. Badala ya kukimbilia kuhukumu, hebu jaribu kufikiri yale mambo mazuri ya huyo mwenzako. Usiwe mtu wa kuwaza mabaya tu kila wakati. Yaani unakuta mtu anawaza kwamba mwenzake atakua amemsaliti, bila kujua kuwaza hivyo ndiyo kunatengeneza kutokuaminiana na kunaweza kutengeneza mazingira ya kufanyika hivyo. Mume wako kachelewa jambo la kwanza sio kuwaza atakua kapitia kwa wanawake wengine. Ukiwaza hivyo jambo la kwanza akifika utaanza kumuuliza maswali ya kumshuku kwamba sio mwaminifu na hii inaweza kuleta mgogoro. Hebu elezea mazuri ya mwezako maana tunapoyaelezea mambo mazuri kuwahusu wenzetu (marafiki au mwenza) badala ya kuwahukumu, mahusiano yanakua katika nafasi nzuri ya kukua.
14. Jipende na kujitunza wewe binafsi kwanza. Watu hudhani kwamba kujitunza au kujipenda binafsi ni kitu kibaya. Kitu ambacho si kweli, Huwezi kuwajali wengine kama wewe mwenyewe hujijali, vivyo hivyo huwezi kuwapenda wengine kama hujipendi. It’s only when you allow your cup to be filled that you can fill the cup of others. If you have nothing in your cup, you can’t give anything away.
15. Mawasiliano ni kuelewa na si kuangalia ni nani yupo sahihi na nani hayupo sahihi. Inapotokea mmepishana mawazo, kabla ya kutaka ueleweke wewe kwanza, jitahidi umuelewe mwenzako kwanza, unapotaka wazo lako ndilo lieleweke kwa mwenzio, utakachoonyesha ni kwamba wewe upo tu ili kufanikisha ajenda yako, hivyo mwenzako atahisi kwamba hujali hisia zake. Mahusiano yako yatanawiri endapo utaweka kipaumbele katika kumuelewa mwezako kwanza.
16. Katika mahusiano mawasiliano yenye ufanisi (effective communication) ni kitu cha muhimu sana. Mawasiliano yenye ufanisi yanatokana na kule kusikiliza na kuongea kwa moyo wa dhati. Watu wanapojihisi wamesikilizwa kwa hisia vizuri, wanahisi kwamba wanajaliwa. Hii ni tofauti kabisa na kule kumsikiliza mtu kichwani tu, yaani kwa kuangalia tu maudhui ya yale maneno mwezako anayosema bila kuchimba au kuweka usikivu kwenye zile hisia zilizopo nyuma ya yale maneno. Mara nyingi hasa sisi wanaume, tunapokua tunawasikiliza wenza wetu, huwa tunasikiliza haraka haraka na kukimbilia kutafuta njia za kutatua hiyo changamoto, halafu tunakuta hata pamoja na kutatua changamoto hizo wenza wetu wanakua bado hawajapata kile walichokua wanakitaka. Wakati mwingine unapomsikiliza mwanamke wako na kuelewa hisia zilizopo nyuma ya maneno yake, inakua ni jibu tosha, tena anaweza yeye mwenyewe kutoa suluhisho. Lengo la mawasiliano yenye ufanisi ni kuelewa ujumbe wa hisia wa mzungumzaji na siyo yale maneno anayotoa. You have to ask yourself What is this person feeling? Listen beyond the words to the feelings.
SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Kijana Wa Kitanzania(kama una miaka kati 20 mpaka 30 soma hapa)
17. Mawasiliano fanisi (effective communication) yanakomboa muda. Unaweza kushangaa kwa nini pamoja na kutatua tatizo uliloelezewa na mke wako lakini bado anaendelea kuliongelea tena na tena. Kuna kitu bado kinakosa hapo, ni kwamba hisia zake hazijasikilizwa. Hii hufanya muda mwingi kutumika kujadili na kutatua suala dogo tu. Hua inashangaza kile kinachotokea pindi mwanamke anapohisi hisia zake zimeeleweka kwa kina. Inakua rahisi kwa yeye kuacha kulizungumzia suala lilelile maana hana sababu ya kufanya hivyo kwa sababu kiu yake imeshakatwa kwa kueleweka hisia zake. So learn to listen with your heart Put your problem-solving urges on hold for a while, and listen with your heart.
18. Adui wako siyo huyo mwenzako. Adui wa nafsi zetu na mahusiano yetu anataka kuharibu mahusiano yako yenye afya. Na cha kwanza ni kutaka uchukulie kwamba huyo mwenzako ndio adui na ndio tatizo. Kama akifanikiwa kukufanya hivyo tayari anakua ameshinda. Never forget that your true enemy is not the other person.
19. Ushindi mzuri katika mahusiano ni kutafuta suluhisho ambalo wote wawili mnalifurahia. Neno la Mungu linasema kuna njia ionekanayo ni njema machoni pa mtu lakini ni njia ya upotevuni. Wakati mwingine kwa kujaribu kusisitiza kuhusu njia zetu katika kutatua jambo, tunaishia kuua mahusiano yetu ya kufurahia. Kwa hiyo unapaswa kuelewa kwamba, japokuwa kuna njia inaonekana ni sahihi kwako inaweza isiwe mbadala mzuri wa kutatua changamoto na pengine siyo mbadala pekee uliopo, zipo njia mbadala kadhaa. Kwa hiyo usijifungie mwenyewe kwenye mtazamo wako pekee jinsi unavyoona wewe tu hata kama unataka kushinda hiyo hoja. Kumbuka mpo kwenye timu moja, hivyo kushinda haina maana njia yako tu ndio itumike. Remember, you’re part of a team. Winning is finding and implementing a solution that both people can feel good about.
20. Huwezi kumlazimisha mwenzako abadilike. Mtu pekee unayeweza kumbadilisha ni wewe. Mabadiliko yanaanza na Yule anayetaka mabadiliko. Wajibu pekee ulionao ni kujibadilisha wewe. Wakati mwingine unaweza kwenda mbele za Mungu kumuomba ambadilishe mwenza wako, ulishawahi kujiuliza swali Je kama Mungu anachotaka ni akubadilishe wewe? Allow God to change you, then leave the rest up to him.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com