Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Tumekutana tena hapa kwa ajili ya kushirikishana maarifa ambayo yatatuwezesha kujenga falsafa mpya ya maisha yetu. Na kupitia falsafa hii tuweze kuishi maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Katika makala ya leo ya falsafa tutaangalia jinsi ya kuishi maisha yenye maana kubwa kwetu na kwa wale wanaotuzunguka.

Ili maisha yetu yawe bora sana, ili tuweze kuyafurahia maisha yetu na ili tuweze kufikia mafanikio makubwa na yatakayodumu, ni lazima maisha yetu na kile ambacho tunafanya viwe na maana kubwa kwetu sisi wenyewe na hata kwa dunia kwa ujumla.

Maana ya maisha yetu inatokana na ule mchango ambao tunautoa kwenye maisha ya wengine. Inatokana na jinsi ambavyo wengine wananufaika kwa uwepo wetu au kwa kile ambacho tunafanya. Ni kwa njia hii tunahamasika kuweka juhudi zaidi ili kuendelea kuwanufaisha wengine na hivyo kufanikiwa zaidi.

Maisha ya maana hayatokani na sisi kuangalia ni jinsi gani tutanufaika tu, hayatokani na kuhakikisha tunapata faida kwenye kila jambo, tena kubwa na ya haraka. Maisha ya maana pia hayatokani na kufikiria fedha tu wakati wote. Japo fedha ni muhimu sana, lakini zinapokuwa ndio kitu pekee unachofikiria kwenye kile unachofanya, unapoteza maana kubwa ya maisha yako.

Kwenye makala hii tutajadili mambo kumi muhimu ya kuanza kufanya ili uweze kujenga na kuishi maisha ambayo yana maana kubwa kwako na kwa wanaokuzunguka pia.

1. Jua ni lipi dhumuni lako kubwa kwenye maisha.

Ni lazima uwe na dhumuni kubwa sana kwenye maisha yako, dhumuni ambalo ni kubwa kuliko fedha, kuliko kuonekana na wengine na kuliko sifa unazopata kutokana na kile unachofanya. Dhumuni hili kubwa ndio kitu kinachokusukuma kuishi maisha mema, kufanya kile ambacho unafanya, ukijua ya kwamba kuna watu wengi wananufaika na wewe kufanya hivyo.

Kama umeshalijua dhumuni hili kubwa la maisha yako hongera sana na lifanyie kazi kila siku. Kama bado hujalijua endelea kutafuta, na anza kwa kufikiri ni jinsi gani unapenda dunia iwe bora zaidi na upi mchango wako kwenye dunia kuwa bora. Kisha fanyia kazi pale ambapo unaona panakufaa zaidi.

2. Fanya kile ambacho unakipenda.

Kwanza maisha yetu ni mafupi sana ukilinganisha na wakati ambao dunia imekuwepo. Pili kuna vitu vingi sana tunavyoshawishiwa kufanya ukilinganisha na muda wetu mfupi tulionao. Ni vigumu sana kuwa na maisha yenye maana kama utakuwa unajaribu kufanya kila kitu, au unafanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya.

Fanya kile kitu ambacho unapenda kweli kukifanya. Ishi yale maisha ambayo wewe unayafurahia, ambayo yanakuwezesha wewe kutoa mchango mkubwa kwa wengine. Na kazana na maisha hayo huku ukifanyia kazi ile dhamira yako kubwa kwenye maisha. Kuishi maisha ambayo huyapendi, au kufanya kitu ambacho hukipendi, kutakuzuia wewe kuweza kutoa kilicho bora kwa wengine.

3. Jua ni mambo gani muhimu kwenye maisha na shughuli zako.

Pamoja na kujua dhamira kubwa ya maisha yako, na kujua kile ambacho unapenda kufanya, bado huwezi kufanya kila kitu kinachohusiana na maeneo hayo. Unahitaji kujua yale maeneo muhimu sana ambayo wewe ukiweka nguvu zako unapata matokeo mazuri na makubwa.

Jua ni maeneo gani muhimu sana kwenye maisha yako, kazi au biashara yako na kisha yape muda wa kutosha. Okoa muda unaopoteza sasa kwenye mambo ambayo sio muhimu sana kwako na hayana mchango kwako kufikia ile dhamira kubwa ya maisha yako. muda ni rasilimali adimu, unavyoweza kuitumia vizuri ndivyo unavyopata matokeo mazuri.

4. Tengeneza falsafa fupi ua maisha yako.

Hii itatokana na kile ambacho unakiamini sana kwenye maisha yako, kile ambacho upo tayari kukisimamia hata kama dunia nzima inakwenda kinyume. Kwa kuwa na falsafa ambayo unaisimamia kutafanya maisha yako yawe na maana kubwa kwako na hata wale wanaokuzunguka.

Kwa kukosa falsafa ambapo maisha yako yanasimama , utajikuta unapelekwa kama bendera na kila anayekuja na ushawishi wake. Lakini unapokuwa na falsafa unayoisimamia, utajiuliza mara mbili kabla hujakubaliana na ushawishi wa mtu yeyote, na hii itakuepusha kutapeliwa na kudanganywa.

5. Weka watu mbele zaidi ya vitu.

Kwa jambo lolote unalifanya, kwa maisha yoyote unayoishi, kila mara jiulize ni kwa namna gani wengine wananufaika na hiki ninachofanya. Weka kipaumbele kwa watu, kama ni biashara jiulize wateja wako wananufaikaje, kama ni kazi jiulize mwajiri na yule anayetegemea huduma unayotoa ananufaikaje. Kwa njia hii utaona fursa nyingi zaidi za kuwasaidia watu na hivyo kuyafikia mafanikio makubwa.

Kwa kuweka kipaumbele kwenye watu, inafanya maisha yako kuwa na maana kubwa.

6. Tafuta upande chanya mara zote.

Kadiri unavyokwenda na maisha yako, utakutana na mambo mengi na changamoto nyingi pia. Kwenye kila jambo utakalokutana nalo, liwe zuri au baya kiasi gani, kila jambo lina pande mbili. Kuna upande chanya wa jambo na kuna upande hasi wa jambo. Upande upi unakubali ukuathiri hilo ni chaguo lako mwenyewe.

Kama unataka kuwa na maisha yenye maana kwako na kwa wengine pia, chagua kuwa upande chanya kwenye kila jambo ambalo unafanya. Chagua kuangalia ni jinsi gani unaweza kutumia hali unayopitia kuboresha maisha yako na ya wanaokuzunguka. Hata kama unapitia wakati mgumu kiasi gani, kuna mambo chanya unaweza kutoka nayo hapo na yakabadili amisha yako na ya wengine pia.

7. Dhibiti mawazo yako.

Kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako, kinaanza na mawazo yako. hofu zote ulizonazo, hazipo sehemu nyingine yoyote bali kwenye mawazo yako. na hata kukata tamaa hakuanzii sehemu nyingine bali kwenye mawazo yako. ukishindwa kudhibiti mawazo yako, yatakuhangaisha sana, yatakuletea kila hali ya kutisha na kukatisha tamaa. Ni jukumu lako kudhibiti mawazo yako, na kuhakikisha yanafikiria kile ambacho wewe pekee ndio unakitaka.

Njia za kudhibiti mawazo yako ni pamoja na kufikiria upande chanya wa jambo, kutajuhudi na hata kuweka malengo ambayo utakuwa unayapitia kila siku.

8. Tafuta ushindi mdogo mdogo kila siku.

Pamoja na kwamba una dhamira ya kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako, lakini mambo haya makubwa hayatokei mara moja, bali ni zao la mambo madogo madogo unayofanya kila siku. Kwa bahati mbaya sana mambo hayo madogo madogo ndio yanaongoza kwa kuahirishwa kufanywa.

Ili kuondokana na tabia hiii ya kuahirisha mambo madogo madogo na hivyo kujizuia kuishi maisha yenye maana kwako, weka malengo ya kila siku na yafanyie kazi. Kama ukiyafikia kwa siku hiyo huu unakuwa ushindi wako mkubwa. Kwa kufanya kama ushindi mdogo mdogo wa kila siku inakusukuma kuweka juhudi hata kama hujisikii kufanya.

9. Rahisisha maisha yako.

Kadiri unavyofanya maisha yako kuwa rahisi, kwa kuhitaji vile vitu ambavyo ni muhimu tu kwako, ndivyo unavyopata nafasi ya kufanya mambo makubwa na yanayoleta maana kwenye maisha yako na ya wengine. Ifanye siku yako kuwa rahisi kuishi, kwa kuwa na majukumu muhimu ambayo unajua ni nini unakwenda kufanya. Pia usikubali vitu vikumiliki wewe, bali wewe ndiyo uvimiliki. Peleka muda wako kwenye vile vitu ambavyo ni muhimu, na acha kuupoteza kwenye vitu ambavyo vinapita tu.

10. Toa kwa wanaohitaji.

Maana kubwa ya maisha inakuja kwa kutoa na sio kwa kupokea. Na uzuri wa kutoa ni kwamba lazima utapokea, hii ni sheria ya dunia, haijawahi kuvunjwa. Unapokea sawa sawa na unavyotoa. Hivyo ili kujenga na kuishi maisha yenye maana kwako na wanaokuzunguka, angalia ni vitu gani unaweza kutoa kwa wengine na vikaboresha maisha yako.

Na kutoa sio lazima iwe fedha, inaweza kuwa utaalamu wako ambao utasaidia wengine kuwa na maisha bora, inaweza kuwa muda wako wa kukaa ana watu wanaohitaji kupata muda na kusikilizwa na vingine vingi.

Kuishi maisha yenye maana ni uamuzi wako na ni kitu ambacho unahitaji kufanyia kazi, haitokei kama ajali. Amua sasa kuweka maana kubwa kwenye maisha yako na kwa kile ambacho unafanya, na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako kwa kuwa na furaha na mafanikio pia.

Nakutakia kila la kheri kwenye kujenga na kuishi maisha yenye maana kubwa.

TUPO PAMOJA.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.