Kitabu ARE YOU FULL CHARGED ni kitabu kinachotupa mbinu za kuweza kuongeza uzalishaji kwenye kazi zetu na kuwa na maisha bora pia. Kwa sasa tunaishi kwenye dunia yenye kelele nyingi na ni vigumu sana kufanikisha kile ambacho mtu unataka kwenye maisha. Kwa kujijua wewe mwenyewe vizuri, na kujua ni kitu gani hasa unachotaka, inakuwa rahisi kwako kukifanyia kazi na kukipata.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu sana niliyojifunza kwenye kitabu hiki kizuri.
1. Unahitaji vitu vitatu muhimu kwenye siku yako ili uweze kuifanya kuwa bora sana. Kitu cha kwanza ni kufanya kitu ambacho kina maana kubwa kwako, kitu ambacho kinakusukuma kufanya sio kwa sababu tu utapata fedha, bali kwa sababu kina maana kubwa kwako. Kitu cha pili ni kuzungukwa na watu ambao ni chanya kuliko wale ambao ni hasi. Watu hawa chanya wanakufanya uone inawezekana na hivyo kukusukuma zaidi, hasi wanakurudisha nyuma. Kitu cha tatu ni uwe na nguvu, nguvu ya mwili na akili ndio vinakuwezesha wewe kupata chochote unachotaka.
2. Fanya kitu chenye maana kubwa kwako au tafuta maana kubwa kwenye kile unachofanya. Maana kubwa ni ile sababu ukiacha fedha, inayokusukuma wewe kufanya kazi au biashara. Kama huna sababu hii kubwa zaidi ya fedha, basi itakuwa vigumu sana kwako kuweka juhudi, hasa pale unapokutana na changamoto, na lazima utakutana nazo.
3. Usisubiri mpaka upate ushindi mkubwa ndio ufurahie na kupata hamasa ya kufanya zaidi. Bali tengeneza ushindi mdogo mdogo kwenye kazi yako na maisha yako kila siku. Fanya kitu kidogo kidogo kitakachoboresha ile huduma unayotoa kwa wateja wako. Na vitu hivi vidogo vidogo ndio vinaleta ushindi mkubwa baadae.
4. Watu wanaoweka lengo lao kubwa kwenye maisha ni kutafuta furaha mara nyingi huwa hawaipati. Kukimbiza furaha ni sawa na kukimbiza kipepeo, utaona kama umekaribia lakini unahitaji kuendelea kukimbiza zaidi. Furaha haitafutwi, furaha ni zao la wewe kuwa na maisha bora, maisha yale yenye maana kwako, kwa kufanya vile vitu ambavyo unapenda kufanya na kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine. Acha kukimbiza furaha na anza kutengeneza maana kubwa kwenye maisha yako na ya wengine pia.
5. Furaha yako kwenye maisha pia inatokana na wewe kuweka pembeni furaha yako kwa muda kwa ajili ya wengine. Kila dakika unayoweka furaha yako pembeni kwa ajili ya watu wengine, unajenga familia bora sana, taasisi bora na hata jamii bora. Pale unapojali wengine na sio kujijali wewe tu, unatengeneza nafasi kubwa zaidi kwako kufikia mafanikio makubwa.
6. Kuna hamasa mbili zinazowasukuma watu kufanya kazi, au biashara. Kwanza ni hamasa kutoka nje, hii ni ile hamasa ambayo mtu anaipata kutokana na wengine wanamwonaje, au kwa motisha anazopewa na vitu vingine vinavyotokana na watu wengine. Pili ni hamasa kutoka ndani, hapa ni pale mtu anaposukumwa na sababu kubwa zilizopo ndani yake kufanya kazi au biashara hiyo. Hapa mtu anafanya kwa sababu ni kitu ambacho yuko tayari kufanya na haijalishi wengine wanasemaje au wanachukuliaje, yeye anajua ni muhimu na anafanya.
7. Kazi yenye maana na kazi inayomletea mtu mafanikio makubwa, ni ile ambayo inaendeshwa na hamasa kutoka ndani ya mtu mwenyewe. Hii ni ile hamasa inayomsukuma mtu kufanya kitu kwa sababu ni kitu muhimu sana kwake. Mwonekano kwa wengine au kupata fedha sio vitu vinavyomsukuma sana, japo vinakuja kama matokeo. Kwa kusukumwa na hamasa kutoka ndani, hakuna kinachoweza kukuzuia kufikia mafanikio makubwa. Maana hata unapokutana na changamoto, ni vigumu kukata tamaa.
8. Kazi yenye maana, na maisha yenye maana hayatokei tu, bali yanatengenezwa. Na hitaji moja muhimu la kutengeneza kazi na maisha yenye maana kwako ni kushikiza kile unachofanya na dhumuni lako kubwa kwenye maisha. Jiulize kile unachofanya kina mchango gani kwa wengine. Jiulize ni jinsi gani maisha ya wengine yanakuwa bora sana kupitia kazi au biashara ambayo unaifanya. Na pia jiulize kama ukiacha kufanya leo, dunia itakosa nini ambacho inakipata sasa. Kwa maswali haya utaona i mchango gani muhimu unaoutoa kwa dunia na hivyo kuona maana kubwa ya kazi yako na biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla.
9. Kazi yako halisi sio kile unachofanya kila siku, bali lile dhumuni lako kubwa kwenye maisha. Unachofanyia kazi ni ile picha kubwa unayoiona ya maisha yako, ile picha kubwa unayoiona ya wale unaowahudumia wakiwa na maisha bora. Hivyo kama huoni picha yoyote kubwa zaidi ya fedha, kazi yako haitakupa msukumo mkubwa na utaona ni kitu kisicho muhimu sana.
10. Kufanya kazi kwa lengo la kupata fedha tu ni sawa na kushiriki kwenye rushwa au utumwa. Kama mtu anakulipa wewe ili ufanye kile ambacho yeye anataka ufanye, na wakati wewe unapendelea kufanya kitu kingine tofauti, hii sio hali sawa kabisa kwako. Ni utumwa wa hali ya juu sana kama unafanya kitu ambacho hukipendi na hakina maana kwako ila unaendelea kufanya kwa sababu unalipwa. Unahitaji kutafuta uhuru wako kwa kutafuta maana kwenye kile unachokifanya au kufanya kile ambacho kina maana kwako.
11. Motisha ambao sio wa kifedha unawahamasisha watu kufanya kazi zaidi kuliko motisha ambao ni wa kifedha. Motisha usio wa kifedha ni kama kutambuliwa, kuheshimiwa, kuongezewa majukumu muhimu, na hata kukubalika kwamba mtu amefanya vizuri. Motisha hizi humfanya mtu aone kazi yake ni njema sana na hivyo kuweka juhudi zaidi. Motisha za kifedha humfanya mtu aone kinachomsukuma ni kupata fedha zaidi na hivyo kufika hatua ambayo hawezi kujisukuma tena kwa sababu hata fedha inayoongezeka haina maana kubwa tena.
12. Kufikia uhuru wa kifedha ni jambo muhimu sana ili kuwa na maisha bora. Kwa sababu kufikiria kuhusu fedha muda wote kunakufanya mtu uwe na hofu kubwa ya maisha na kutokuwa na uhakika. Lakini unapokuwa na uhuru wa kifedha unakuwa huru kufanya yale mambo ambayo ni muhimu kwako na yana maana kubwa kwenye maisha yako. wakati unaelekea kwenye uhuru wa kifedha, fedha isiwe ndio sababu yako kuu ya kufanya kile unachofanya, kuwa na hamasa ya ndani na hii itakuwezesha wewe kupata fedha unazotaka.
13. Kadiri unavyofikiria wengine wananufaikaje na kazi au biashara yako ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kuziona fursa zaidi za kuwahudumia zaidi. Na hii itakuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa. Kama utakuwa unaangalia fedha tu, unaweza kukosa nafasi ya kuziona fursa muhimu kutokana na mahitaji ya watu wanaohusika na kile unachofanya.
14. Kutengeneza kazi au biashara yenye maana kubwa sana kwako vitu vitatu muhimu vinahitaji kukutana pamoja. Cha kwanza ni nguvu zako au uimara wako, hapa ni kujua ni maeneo gani ambayo uko imara au uko vizuri sana. Cha pili ni mapenzi yako binafsi, hapa ni kuangalia ni kitu gani unapendelea sana kufanya au kufuatilia. Na cha tatu ni hitaji la dunia. Hapa ni pale watu wanapohitaji sana kile ambacho unafanya ili waweze kuwa na maisha bora. Ukiweza kuvifikisha vitu hivyo vitatu pamoja, hakuna kitakachokuzuia wewe kufanikiwa kwenye maisha yako. hivyo ni muhimu sana kujua vipaji ulivyonavyo nakuangalia ni jinsi gani dunia inaweza kunufaika navyo.
15. Kuweka maana kubwa kwenye kazi au biashara yako angalia ni jinsi gani vipaji vyako, elimu yako, uzoefu wako, utaalamu wako na utofauti wako unaweza kuwa na manufaa kwa watu wengine. Ni kitu gani kinakutofautisha wewe na watu wengine? Ni kitu gani upo tayari kuacha furaha ya muda mfupi, kukubali kuteseka lakini baadae ukanufaika sana? Kijue kitu hiki na kitumie kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Kwa njia hii utafikia mafanikio makubwa sana.
16. Kuna kitu ambacho wewe unaweza kukifanya kwa ubora zaidi ya watu wengine wote duniani. Umezaliwa na vipaji vya kipekee sana kwako, na wengine wana vipaji vyao tofauti. Utofauti huu wa vipaji ndio unatofautisha watu wote na hivyo mafanikio yako huwezi kuyalinganisha na mtu mwingine yeyote. Kwa sababu kuna vitu wewe unaweza kufanya zaidi ya wengine na kuna vitu wengine wanaweza kufanya zaidi ya unavyoweza kufanya wewe, jua kile unachoweza kufanya vizuri sana na weka nguvu zako zote hapo. Usikazane kufanyia kazi yale madhaifu yako, fanyia kazi yale maeneo ambayo uko vizuri, hayo ndiyo yanakupeleka wewe kwenye mafanikio.
17. Huwezi kuwa vizuri kwenye kila kitu na kila eneo. Kama unakazana maisha yako yote uwe vizuri kwenye kila kitu, unapoteza muda wako na hutaweza kuwa vizuri kwenye kitu chochote. Chagua yale maeneo ambayo uko vizuri, yale unayopenda kufanya na weka nguvu zako hapo. Chagua kuwa bora sana kwenye maeneo machache ambayo yatakufikisha kwenye mafanikio makubwa.
18. Hakikisha siku yoyote haiishi bila ya wewe kufanya kitu ambacho ni muhimu sana kwako. Siku inapopita ni kwamba imepotea moja kwa moja, huwezi kuitengeneza tena kwenye maisha yako. ukizembea siku moja ikapita, utashangaa siku kadhaa zimepita na hufanyii kazi yale ambayo ni muhimu kwako. Mara unashangaa miaka kumi imepita na maisha yako yako pale pale na ukiangalia nyuma kuna fursa nyingi sana ambazo umezipoteza. Hakikisha kila siku unaipa uzito wake na utaona fursa nyingi za kufikia mafanikio makubwa.
19. Hakikisha ndoto unayofanyia kazi kwenye maisha ni ndoto yako halisi. Watu wengi wanakimbiza ndoto ambazo sio ndoto zao halisi, japo wanaweza kujiaminisha hivyo. Mara nyingi watu hushawishiwa na yale mazingira yanayowazunguka. Mara nyingi utakuta watoto wa walimu nao wanakuwa walimu, au watoto wa madaktari nao wanakuwa madaktari. Wapo ambao wanakuwa wamependa kweli, ila wengi wanakuwa wameingia kwa msukumo kutoka kwa wazazi au watu wa karibu. Kwa namna hii watakosa ule msukumo wa ndani ambao ni muhimu kuwafikisha kwenye mafanikio makubwa.
20. Tunaishi kwenye dunia ambayo kuna taarifa nyingi sana na zote zinagombania muda wako. Simu yako inaweza kuwa usumbufu mkubwa sana kwako. Mawasiliano ya kawaida ya simu, email, mitandao ya kijamii, vyote hivi vinakazana kupata muda wako. Kama utaruhusu usumbufu huu uchukue muda wako, hutaweza kufanya jambo lolote la maana kwako. Hakikisha unatenga muda maalumu wa kupitia mambo ya simu yako, muda mwingine uweke kwenye ile kazi ambayo ni muhimu zaidi kwako. Dhibiti mawasiliano yako yote, usikubali mawasiliano yakuendeshe wewe, bali wewe ndio uyaendeshe.
21. Sema hapana kwa usumbufu ambao unachukua muda wako. Unahitaji kuweka nguvu zako nyingi kwenye kile unachofanya na sio kwenye kelele zinazokuzunguka. Kuweka simu yako wazi ambapo kila ujumbe wa kwenye mtandao unakufikia, hutaweza kupata utulivu wa kuweka juhudi kwenye kazi zako. Zima mtandao kwa muda unaotaka kufanya kazi inayohitaji utulivu mkubwa. Pia unaweza kuweka simu yako kwenye hali ya kutokuwa na mlio, hii itakupa wewe nafasi ya kufanya kazi zako kwa utulivu mkubwa.
Mafanikio yako kwenye kazi, biashara na hata maisha yanategemea na jinsi ambavyo unayachukulia maisha yako na kile unachokifanya pia. Kwa kujua kile ambacho unahitaji kwenye maisha yako, vipaji vyako, dunia inachotaka na kuwa na matumizi mazuri ya muda na nguvu zako ni njia ya uhakika ya kuwa na maisha bora na yenye mafanikio. Hakikisha maisha yako yanakuwa na maana kubwa zaidi tu ya kuzisukuma siku na kupata fedha.
Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi haya uliyojifunza.
TUPO PAMOJA.