Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Are You Fully Charged?

Habari ndugu msomaji wa Makala ya uchambuzi wa vitabu. Karibu sana kwenye wiki nyingine ya uchambuzi wa vitabu. Wiki hii tunajifunza kutoka kwenye kitabu kinachoitwa Are you Fully Charged? (Je umejaa chaji?) kilichoandikwa na ndugu Tom Rath. Kitabu hiki kinatoa mafunzo mazuri ya jinsi mtu anaweza kuishi maisha bora kwenye kila nyanja bila kuathiri mahusiano yake na wale awapendao, na bila kuharibu afya yake. Mwandishi anafananisha maisha na kazi kama betri ya kuchaji, kwamba mtu atafurahia maisha na kazi yake kama maisha na kazi yatakua na chaji iliyojaa. Anafundisha kwamba kuna vitu katika maisha tunavyofanya vinapunguza chaji na kuna vitu vingine vinatuongezea chaji. Pia tofauti kabisa na watu wengi wanavyoamini kwamba kufanikiwa ni kujitesa, kutokulala, kutokula au kutokufurahia maisha na wengine, kitabu hiki kinafundisha kwamba mafanikio yanapimika katika sehemu kuu tatu, kutengeneza maana kwenye kile unachofanya , kuwa na mahusiano bora na wengine, na kuwa mwenye nguvu (afya bora). Mwandishi ameeleza mambo mengi mazuri sana, yaliyofanywa kitafiti na sio kama aonavyo yeye, bali utafiti ndio unaongea zaidi kwenye kitabu hiki.

 
Karibu sana tujifunze wote.
1. Tengeneza maana kwa ushindi mdogo. Jiulize ni kitu gani hicho utakachofanya leo kilete utofauti? Hata kama ni kidogo. Utofauti mdogo mdogo ndio unapelekea utofauti mkubwa, hivyo hivyo ushindi mdogo mdogo ukikusanyika kwa pamoja ndio unaleta ushindi mkubwa. Usipuuzie jambo dogo ukadhani hata ukilifanikisha litakua halina utofauti mkubwa, hapana si kweli. Hakikisha kila unachofanya hata kama ni kidogo unakifanya vizuri ili kuleta maana. Maana inaletwa kwa kuunganisha viushindi vidogovidogo na kisha kua ushindi mkubwa. Small wins generate meaningful progress
2. Acha kutafuta furaha, tafuta maana. Utafutaji wa maana ndio unaofanya maisha yawe ya thamani na sio utafutaji wa furaha. Watu wanaotumia muda mwingi katika maisha kujitafutia furaha yao binafsi, hua hawaipati. Furaha pasipo maana ni sawa na maisha yenye ubinafsi. People leading meaningful lives get a lot of joy from giving to others.
3. Fanya vitu kutokaa na msukumo wa ndani au hamasiko la ndani (intrinsic motivation) kuliko hamasiko la nje. Msukumo wa nje huwa sio endelevu, hivyo ukiutegemea na wewe hutadumu. Hamasiko la ndani hua ni la mtu binafsi. Hamsiko la ndani ndio linalompa mtu nguvu ya kufanya zaidi na zaidi hata anapokutana na vikwazo. Mfano kama unafanya biashara, hamasiko la nje linaweza kua kutengeneza faida kubwa, na hamasiko la ndani likawa kuwafanya wateja wawe wenye furaha au kutoa suluhisho la tatizo linalowakabili wateja.
4. Tafsiri ya KAZI kwa siku hizi na zijazo inabidi kupata maana mpya. Kazi inapaswa kua kusudi na sio sehemu. Kazi ni kuweza kutendea kazi kipaji chako na kuweza kuzalisha thamani. Huwezi kufurahia kazi yako kama hujui hiyo kazi inaleta maana gani, je kazi unayofanya inaendana na kusudi lako la kuwepo hapa duniani? Wale wanaodhani kazi ni sehemu fulani, au kampuni fulani, huishia kuhama kazi moja hadi nyingine bila kupata utoshelevu.
5. Tafuta wito mkuu zaidi ya fedha. Lengo kuu la kufanya kazi linapokua ni fedha hutaridhika hata ulipwe kiasi gani. Utafiti unaonyesha kwamba wafanyakazi wanaoweka fedha kama kipaumbele huishia kua na msongo wa mawazo kwenye kazi moja hadi nyingine. Utatafuta kazi inayolipa zaidi hata kama kazi yenyewe haiendani na kusudi au ndoto zako. Hivyo unadhani kwamba utafurahia maisha ukilipwa hizo fedha nyingi, ila mwisho wa siku unajikuta huna furaha ya kudumu. Kutengeneza kipato cha milioni 50 kwa mwaka huonekana hakitoshi kama marafiki zako wanatengeneza zaidi ya milioni 100 kwa mwaka. Ndio maana unashauriwa kutafuta wito mkuu kuliko fedha. Maana Furaha hailetwi na fedha nyingi, furaha ya kudumu inaletwa kwa kutumikia kusudi lako ambalo ni kuu kuliko fedha, na kutengeneza maana katika kile unachofanya pia kuyapa maisha ya wengine maana na furaha. Someone else will always have a bigger house or a better car. It is a race you will never win.
SOMA; Mbinu za kuongeza ufanisi wako kwenye biashara ili kuongeza faida.
6. Fedha inaweza kuua maana. Lengo linapokua ni fedha, ni rahisi kuweka maslahi yako mbele zaidi ya maslahi ya kundi. Hata kama una nia nzuri, inapotokea ukawa unalipwa ili kufanya kazi ili uwazidi wenzako, lazima kutaleta mgawanyiko wewe na wenzako. Motisha wa kifedha usipoangaliwa vizuri husababisha mahusiano na wafanyakazi wenzako kuharibika. Hii ndio maana ugomvi mwingi maofisini hua kati ya wafanya kazi wanaozidiana mishahara. Wale wenye mishahara midogo hutengeneza chuki dhidi ya wale wenye mishahara mikubwa. Au wenye mishahara mikubwa hutengeneza dharau dhidi ya wale wenye mishahara midogo.
7. Unatengeneza maana pale uwezo wako na vile unayovipenda vinapokutana na mahitaji ya dunia. Kufahamu vipaji vyako na kuwa na ustahimilivu na kile upendacho katika maisha ni muhimu, lakini hilo halitoshi maana hilo ni nusu tu katika mlinganyo (equation) wa supply and demand. Kitu ambacho kinaweza kua cha muhimu zaidi ni kufahamu dunia inahitaji nini kutoka kwako na jinsi gani unavyoweza kutumia vipaji na uwezo wako katika kuzalisha kile unachopaswa kutoa kwa dunia.
8. Maneno chanya yanapotumika aidha kwa kuongea au kwa kuandika ni kama gundi inayoshikilia mahusiano pamoja. Katika mazungumzo yako ya kimaandishi au kuongea hakikisha yanatawaliwa na maneno chanya zaidi, ili kuweza kustawisha mahusiano yako na wengine. Utafiti unaonyesha kwamba maneno hasi yana nguvu mara nne zaidi ya maneno chanya. Hii ina maana unapotoa neno moja hasi kwa mwenzako yatahitajika maneno chanya manne ili kumrudisha katika hali ya mwanzo.
9. Tafiti nyingi zinaonyesha kwamba motisha usio wa kifedha (nonfinancial incentives) kama vile kutambulika (recognition), usikivu (attention), heshima na wajibu vinaweza kuwa na ufanisi zaidi ya motisha wa kifedha. Kama unataka kuhamasisha watu wafanye kazi kubwa wape motisha ambao utanufaisha timu yote na motisha huo usiwe wa kifedha.
10. Katika zama hizi za leo kuna taarifa nyingi zisizokuwa na mwisho, pia kuna vizuizi vingi visivyoisha, ni rahisi kutumia muda mwingi katika mabishano na majibizano. Ni rahisi sana kukosa umakini katika kazi kwa sababu ya simu au habari kwenye radio, tv, magazeti n.k. Matakwa ya wengine yanayokuja kwako lazima yatatumia sehemu ya muda wako wa siku. Mfano wapo watu watataka kuchati na wewe, kukupigia simu muongee, wapo watakaotaka mtoke wote n.k. Ila baada ya miaka kadhaa ijayo (5 au 10) vitu utakavyokua unajivunia havitatokana na matokeo ya kufuata matakwa ya wengine. Kitu kitakachojalisha katika maisha yako ya baadaye ni kile ulichoanzisha leo na sio ulichoanzishiwa. Usiishi maisha yako kwa kuwa mtu wa kujibu tu (responding) badala yake kuwa mtu wa kuanzisha vitu ambavyo baadaye utakua unajivunia.
11. Hata pale unapokua huna zuri la kusema kwa wengine usionyeshe dharau au kupuuzia. Kuwapuuzia wengine kunawaudhi kuliko hata mrejesho hasi.
SOMA; Kilimo Bora cha Nyanya; Maandalizi Ya Mbegu, Shamba Na Upandaji Wa Miche.
12. Unapokosolewa na wengine ina maana kwamba wana kufuatilia na wanakupa usikivu (attention), maana isingekua hivyo wasingekua wanapata cha kukukosoa. Haina haja ya kutumia muda wako mwingi kuumia kwa nini umekosolewa, maana ni bora kukosolewa kuliko kuupuziwa.
13. Ikiwa utaendelea kusubiri jamii iendelee kukupa tafsiri ya furaha kwa ajili yako, utaingia kwenye mbio ambazo hutakua na nafasi hata moja ya kushinda. Tafuta tafsiri (definition) sahihi ya furaha yako.
14. Watu hupenda kuzungumza kujihusu wao. Utafiti unaonyesha kwamba asilimia 40 ya hotuba na mazungumzo yote ya siku nzima yanahusu mazungumzo ambayo watu wakiwaeleza wenzao vitu wanavyofikiri na wanavyohisi. Hii ni kwa sababu kila mtu anataka kuonekana wa muhimu zaidi. Ukitaka kuboresha mahusiano yako na wengine pindi unapokua kwenye mazungumzo usiwe mtu wa kuongelea mambo yako, wafanye wengine wazungumze kujihusu wao, maana wanapozungumza wanajihisi ni wa muhimu. Watu wako tayari hata kuacha fedha ili tu wazungumze kujihusu wao.
15. Epuka kufurahia mwenyewe maisha. Unapofurahia maisha na wengine unatengeneza kumbukumbu nzuri itakayodumu kwa muda mrefu lakini pia utajisikia vizuri zaidi. Utafiti unaonyesha kwamba watu wengi husimulia kumbukumbu nzuri za nyuma kua ni zile nyakati walizofurahia na wengine, kama vile sherehe za harusi, sikukuu za Christmas, likizo za pamoja, walipoenda matembezi ya pamoja na wawapendao (kwenda out) n.k Mfano tukio moja liwe nini wewe binafsi umeenda kuogelea mwenyewe katika hotel ya kifahari, na tukio lingine uwe umeenda na marafiki zako uwapendao kwenda kuogelea kwenye hotel hiyohiyo. Je ni tukio lipi litakua rahisi kulikumbuka? Bila ubishi tukio la pili ulilokua na marafiki ndilo utakalofurahia na kulikumbuka muda mrefu zaidi.
16. Shauku ya kuwasaidia wengine ni sehemu inayokufanya kuwa binadamu. Unapokosa shauku hiyo basi ujue utu wako una uwalakini. Watu wengi hufikiri wameumbwa ili wawe watu wa kusaidiwa tu. Tafiti pia zinaonyesha kwamba asilimia kubwa ya watu wanaopata utoshelevu ni wale watoaji kuliko wale wapokeaji. Anza leo kusaidia wengine, hata wale wasiokua na uwezo wa kukulipa chochote. You are much better at helping yourself if you are also helping another person with a similar problem.
SOMA; Tabia Tano(5) Za Wafanyakazi Ambao Ni Sumu Kwenye Eneo La Kazi Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
17. Weka afya yako kua kipaumbele cha kwanza. Mafanikio yeyote utakayotafuta huku afya yako ikiharibika hutayafurahia. Kabla hujafikiria mafanikio yeyote kama ya fedha na mali anza na mafanikio ya afya kwanza. Wapo watu wengi hupata mafanikio ya kifedha na mali na cha ajabu hutumia mafanikio hayo kuharibu afya zao, maana huanza kulewa sana, kuvuta sigara au madawa ya kulevya, kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi na watu wengi n.k. Vitu hivyo hupelekea kudhoofisha afya na kisha kufupisha maisha yao. Tafiti tena zinaonyesha watu wengi wanaowasaidia wengine, hudhani hao wanaowasaidia ni wa muhimu kuliko wao wenyewe, ndio maana hujikuta hawajali afya zao wenyewe. Wale unaowasaidia utawasaidia vizuri endapo utaweza kujisaidia wewe kwanza kua na afya bora ili uwe na uwezo wa kuendelea kuwasaidia. Kwa wale waliwahi kupanda ndege, ukiwa kwenye ndege kuna wale wahudumu wanaotoa maelekezo kwenye ndege, huwa wanatoa maelekezo kwamba endapo patatokea upungufu wa hewa ya oksijeni ndani ya ndege kuna kifaa cha kuvaa puani ili kupata oksijeni, lakini wanakwambia kama uko na mtoto wako (hata ndugu au rafiki), anza kujihudumia wewe kwanza kuvaa kifaa hicho ndipo umsaidie mwanao kumvalisha. Maana endapo ukakimbilia kumhudumia mwanao kwanza ikatokea kabla hujamaliza kumhudumia ukazidiwa na kupoteza maisha ni kwamba hata Yule mwanao utampoteza, hivyo mtakua mmepotea wawili. Ila ukianza wewe kujihudumia ni rahisi kumhudumia na mwanao maana utakua tayari wewe uko salama.
18. Ili uwe mwenye nguvu, unahitaji kula vizuri, mazoezi pamoja na kulala vizuri. Katika ulaji tunaposema ulaji mzuri wa chakula haina maana kula vyakula tunavyotaka bali vyakula vilivyo sahihi. Vyakula tunavyokula vina ushawishi wa moja kwa moja kwenye afya zetu. Kula vizuri ni rahisi kama utaanza na vyakula sahihi. Unaweza kuanza na vitu vya msingi kama vile kuepuka vyakula vya kukaanga kwa mafuta, achana na vitu vilivyoongezewa sukari kama soda, pipi n.k, punguza kula vyakula vilivyokobolewa. Kula mbogamboga na matunda kwa wingi. Hakikisha unakua na nidhamu ya hali ya juu katika ulaji wa chakula. Unaweza kuanza na msingi huo wakati ukijifunza vitu vingine zaidi kuhusu ulaji bora wenye afya.
19. Kuchelewa kulala kunapunguza mafanikio badala ya kuongeza. Tulipokua tunakua tuliamini kwamba kukesha ukifanya kazi ndio njia ya uhakika kufanikiwa, kumbe si kweli. Wataalamu wanasema kwamba mtu ili awe na afya njema anapaswa kulala masaa 7 hadi 8. Na kwa kila saa unalopunguza katika kulala ujue unapunguza pia saa moja ya kufanikiwa. Kama unalala masaa 5 ina maana umepunguza masaa 2 ya kulala, hivyohivyo umepunguza masaa mawili ya kufanikiwa. Kama ulikua ufanikiwe kesho saa 4 asubuhi, utafanikiwa saa 6 mchana na kwa kadri unavyoendelea kupunguza masaa ya kulala ndivyo unavyozidi kupeleka mbele masaa ya kufanikiwa kwako. Utafiti unaonyesha kwamba mtu anapokosa usingizi kutosha kunaleta athari mbaya katika afya yake, utendaji kazi wake, na pia kunapunguza uwezo wa kufikiri.
20. Siku za kufanya mambo yenye kuleta utofauti zina ukomo. Hivyo basi usipo tumia muda vizuri kwa kufanya vitu vyenye kuleta maana, uwezekano wa kuja kujutia baadaye ni mkubwa sana. Kila mtu anayo fursa ya kuamua jinsi gani atumie muda wake. Usipotumia muda wa sasa vizuri, baadaye utakuja kugundua kwamba hukutekeleza zile ndoto zako, ulizokua nazo miaka mingi iliyopita. Anza sasa kwa kutengeneza maana, wekeza katika kuimarisha mahusiano yako, hakikisha unayo nguvu unayohitaji kuwa vizuri. Ukiweza kufanya vitu hivyo vitatu katika muunganiko ndiyo ufafanuzi wa kuwa mwenye chaji iliyojaa pia utakua na uwezo wa kuwachajisha wale wanaokuzunguka.
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

One thought on “Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Are You Fully Charged?

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: