Vitu hivyo vitatu vinakutosha kabisa kuweza kuishi maisha ya mafanikio makubwa sana, kama utaanza kuvipa uzito mara moja.

Kwa kuzingatia vitu hivi vitatu, utabadili kabisa mtizamo wako kuhusu maisha na utapata nguvu ya kujitoa zaidi ili uweze kupata matokeo makubwa zaidi.

Jukumu lako….

Kama kuna kitu chochote unachotaka kupata kwenye maisha yako, basi hilo ni jukumu lako wewe, na sio la mtu mwingine yeyote.

Unataka kupata kipato kikubwa ukilinganisha na unachopata sasa, hilo ni jukumu lako.

Unataka kufika ngazi za juu sana kuliko ulipo sasa, unataka kutoa huduma bora zaidi, hilo ni jukumu lako.

Unataka kuanza biashara, au kukuza biashara yako zaidi, unataka kuwafikia wateja wako, hilo ni jukumu lako.

Unataka kuwa na familia bora, unataka kuwa na mahusiano bora na wote wanaokuzunguka, hilo ni jukumu lako.

Unataka kuwa na maisha ya furaha na mafanikio, ni jukumu lako.

Matatizo yako….

Unataka maisha bora kweli, lakini hupo tayari kujitoa kweli kuyafikia kaisha yako, hilo ni tatizo lako.

Unaona kama unayopaswa kufanya ni mengi sana na wewe huwezi, unaona kama unayotakiwa kufanya ni ya kitoto sana, hayo ni matatizo yako.

Unatafuta njia za mkato za kufikia mafanikio unayotaka, unacheza bahati na sibu, unacheza kamari, unaiba, unadhulumu, unadanganya, na mwishowe unakuja kugundua kote ulikuwa unapoteza muda tu, hayo ni matatizo yako.

Baada ya kujaribu jaribu, bila ya kuweka juhudi hasa, na ukaona hupati, unakuja na taarifa za kujifurahisha wewe mwenyewe kwamba walioweza wamebahatika tu, au wamependelewa, au wametumia nguvu za ajabu, hayo ni matatizo yako.

Uzembe wako….

Umeanzisha biashara uliyokuwa unapanga kuanza kwa muda mrefu, umeajiri watu wa kusimamia biashara hiyo, wamekimbia na fedha au wamesababisha hasara kwenye biashara yako, huo ni uzembe wako.

Umekubaliana na rafiki yako, au ndugu yako, kwamba mfanye biashara pamoja, mmechanga mtaji, mmeanza biashara, katikati mwenzako kakugeuka, kaleta hasara na kakimbia na mtaji uliobaki, huo ni uzembe wako.

Umekuwa kwenye kazi muda mrefu, lakini hupandishwi cheo, wala huongezewi mshahara, na wakati wengine wanapashindwa kila siku, huo ni uzembe wako.

Mahusiano yako yamekuwa yanakusumbua, familia yako ni ugomvi kila siku, hakuna anayeelewana na wewe, huo ni uzembe wako.

Ni jukumu lako na hivyo chukua hatua.

Ni matatizo yako na hivyo badilika.

Ni uzembe wako hivyo kuwa makini wakati mwingine, usirudie makosa uliyofanya sasa.

Kama hii ni ngumu kwako jua mafanikio pia yatakuwa magumu kwako. Kama ni rahisi kwako jua mafanikio ni uhakika. Mafanikio yanakuja pale mtu unapochukua jukumu hilo na kuacha kutafuta sababu au mtu wa kulaumu.

SOMA; Dalili Saba Kwamba Tayari Wewe Una Mtizamo Chanya Utakaokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa.

TAMKO LANGU;

Ni jukumu langu kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yangu, kuishi maisha bora na ya furaha. Ni matatizo yangu pale ninapokuwa na mtazamo hasi au potofu unaonizuia kufikia mafanikio hayo makubwa. Na ni uzembe wangu pale ninapofanya makosa yanayonirudisha nyuma, na hivyo nahitaji kujifunza na kutokuyarudia tena.

NENO LA LEO.

“The moment you accept responsibility for EVERYTHING in your life is the moment you gain the power to change ANYTHING in your life.”

Pale unapokubali kwamba maisha yako ni jukumu lako, ndipo unapopata nguvu ya kubadili chochote kwenye maisha yako.

Mafanikio ni jukumu lako, mtazamo hasi ni tatizo lako, kushindwa ni uzembe wako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.