Bado tupo kwenye mwanzo wa mwaka na kipindi hiki ndipo watu wengi sana wanaweka malengo na mipango ya kuanza biashara au kukuza biashara zao zaidi. Katika kipindi hiki watu wengi wanauliza mawazo bora ya biashara ambayo wanaweza kufanya na wakapata faida nzuri na mafanikio pia.

Wazo la biashara ni sehemu muhimu sana kwenye mafanikio ya biashara yoyote. Lakini pia hakuna wazo bora la biashara kwa kila mtu, wazo ambalo linaweza kuwa bora sana kwa wengine, kwako linaweza lisiwe bora. Ndio maana watu wengi wanaoiga biashara hujikuta katika wakati mgumu kwa sababu waliona wengine wanafaidika lakini wao hawafaidiki.

Ubora wa wazo la biashara unategemea na mtu mwenyewe na ndio maana ni muhimu sana kila mtu kupima kama kweli wazo lake la biashara ni bora. Zoezi hili ni lazima lifanywe na mfanyabiashara mwenyewe maana yeye ndiye anayeongoza biashara yake. Katika makala hii ya leo tutaangalia njia tano za kupima kama wazo lako la biashara ni bora kwako.

  1. Je wazo lako la biashara linatatua tatizo gani?

Mafanikio ya biashara yoyote yanatokana na kutatua matatizo ya watu, au kutimiza mahitaji yao. Njia ya kwanza kabisa ya kupima wazo lako ni kujiuliza ni tatizo gani unataka kutatua, au ni hitaji gani ambalo watu hawajapatiwa. Ni lazima wazo lako liongeze thamani kwenye maisha ya watu wengine, iwe kwa kuwatatulia matatizo au kuwapatia kile ambacho wanakosa.

Wazo bora la biashara ni lile ambalo linatatua tatizo ambalo linasumbua sana na linawasumbua wengi. Kadiri watu wanavyohitaji kitu sana, ndivyo thamani yake inakuwa kubwa pia.

  1. Je watu wapo tayari kulipia kile unachotoa?

Unaweza kuwa na wazo zuri sana la kutatua matatizo ya watu, au kuwapatia kile ambacho wanakihitaji sana, lakini watu wakawa hawapo tayari kulipia gharama unazotoza. Hivyo kabla hujasema kwamba una wazo bora la biashara ni vyema ukajiridhisha kama watu wapo tayari kulipa gharama ili kupata huduma au bidhaa unayotoa wewe.

Unaweza kuona sehemu hakuna magari kwa ajili ya usafiri wa umma, na ukaona kweli kwamba watu wanahitaji usafiri. Wewe ukapeleka usafiri pale na ukakuta watu wanaona gharama unayotoza ni kubwa sana bora waendelee kutembea na miguu.

Kwa biashara yoyote unayofanya au kutaka kufanya, angalia uwezo wa watu na hata utayari wao wa kulipia gharama utakazotoza.

  1. Je kuna wateja wa kutosha kuweza kukidhi gharama zako na kupata faida?

Unaweza kuwa na wazo la biashara ambalo linatatua matatizo ya watu, na ukaona kweli kuna watu wapo tayari kulipia gharama za kupata huduma au bidhaa yako, ila tatizo likaja kwamba watu hao ni wachache sana kiasi kwamba hawatoshi kufanya manunuzi ya kutosha kufidia gharama zako zote na kubaki na faida.

Ni muhimu kujua ukubwa wa soko la biashara yako na kuona kama ukubwa huo utakuwezesha kufidia gharama zako na hatimaye wewe kubaki na faida. Tofauti na hapo utashindwa kuendesha biashara yako.

  1. Je ni kitu ambacho unakipenda, au kupenda kufanya?

Sehemu nyingine muhimu ambapo mafanikio ya biashara yoyote yanatokea ni mapenzi binafsi ya mfanyabiashara mwenyewe. Kama unafanya biashara ambayo inatokana na kitu unachopenda kweli, au unachopenda kufanya, utakuwa tayari kupambana hata pale unapokutana na changamoto. Pia utakuwa na shauku kubwa na hivyo kutafuta njia za kuiboresha zaidi. Na utakuwa na ubunifu zaidi.

Jiulize kama wazo lako la biashara linatokana na kitu ambacho unapenda kufanya au unakipenda. Kama unapenda kweli, una nafasi kubwa sana ya kufanikiwa, maana wewe hutachukulia tu kama kazi au biashara, bali utachukulia kama sehemu ya maisha yako.

  1. Je unaweza kumwelezea yeyote kwa njia rahisi na akakuelewa?

Njia nyingine muhimu ya kujua wazo bora la biashara ni urahisi wake kwenye kueleweka na wengine. Kama bibi yako ambaye hakupata nafasi ya kusoma, akikuuliza unafanya biashara gani mjukuu wangu, je unaweza kumweleza kwa lugha rahisi na akakuelewa? Kama jibu ni ndio basi hilo ni wazo bora kwako la biashara, na kama linaendana na hayo mengine hapo juu basi anza kulifanyia kazi. Kama huwezi kumweleza bibi yako akaelewa, basi kwa bahati mbaya sana hata wewe bado hujalielewa wazo lako la biashara. Na kama hujalielewa utawezaje kufanikiwa?

Hakikisha unalielewa vizuri wazo lako la biashara na biashara ile unayofanya, kiasi kwamba hata mtu gani akikuuliza unafanya biashara gani basi uweze kumwambia kwa urahisi. Unaweza kukutana na mdau anayeweza kuisaidia biashara yako na akakupa dakika tano za kujieleza, kama hazikutoshi utakosa msaada muhimu kwa biashara yako. ni muhimu kuielewa na kuweza kuielezea biashara yako kwa wengine.

Kama kila mwaka umekuwa unasema utaanza biashara lakini huanzi, usiendeleze hilo mwaka huu 2016. Anza kuweka kwenye matendo ile mipango yako yote, na kama utakwama ndio utajifunza zaidi. Kama bado hujapata mwanga wa wapi uanzie kwenye biashara tuwasiliane. Kila la kheri.