Unapokutana na changamoto kwenye maisha yako, changamoto kubwa ambayo inakuhitaji kufanya maamuzi muhimu, hufanyi maamuzi hayo wewe. Badala yake unatafuta ushauri kwa wengine, na wengine wanakupa ushauri, na kwa sababu wewe hujakaa chini na kuitafakari changamoto hiyo kwa kina, unaona ushauri uliopewa ni bora na kuuchukua kama ulivyo na kufanyia kazi.

Unafanyia kazi ushauri ule na kama majibu yanakuja vizuri basi unafurahia na kuona umechukua maamuzi bora. Ila kama majibu hayatakuja vizuri sasa, hapa ndio mambo yanapoanza, unalaumu ya kwamba umeshauriwa vibaya.

Ukweli ni kwamba umekuwa unakimbia kufanya maamuzi ya msingi wewe mwenyewe ili upate mtu wa kulaumu. Na hapo nafsi yako haitaumia sana kwa sababu utafikiria hata hivyo siyo mimi niliyeamua nifanye hivi, nilishauriwa na watu hawa ambao ni wataalamu sana au ni wazoefu kwenye eneo hili.

Changamoto moja kuhusu ushauri ni kwamba hakuna ushauri mmoja unaowafaa watu wote. Kuna ushauri unaoendana na mtu husika katika tukio husika na wakati husika. Hivyo licha ya kuhitaji ushauri kutoka kwa wengine, bado wewe mwenyewe ndiye unahitaji kufanya maamuzi ya mwisho. Na ukishafanya maamuzi hayo unaweka majukumu yote juu yako, kama mambo yatakwenda vizuri poa, kama hayatakwenda vizuri ni wewe mwenyewe umesababisha.

Sisemi usiombe ushauri kwa wengine, omba sana, ila jua mwisho wa siku wewe ndiye utakayefanya maamuzi. Usimeze ushauri kama unavyoupata, hata kama unatoka kwa mtu gani. Wewe ndiye mtaalamu na mzoefu sana kwenye maisha yako kuliko mtu mwingine yeyote.

Acha kutafuta watu w akulaumu, ukikosea hata kama utalaumu watu wangapi, bado itabaki ni wewe umekosea. Pokea ushauri, ufikiri kwa kina, kulingana na changamoto unayopitia, na hali uliyonayo sasa, fanya maamuzi yanayoendana na wewe na ambayo utakuwa tayari kuyasimamia hata iweje. Fanyia kazi maamuzi yako, na pokea matokeo kwa mikono miwili, yawe mazuri au mabaya.

SOMA; Mambo 21 muhimu ya kiufanya kila siku ili kuwa na maisha yenye mafanikio.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba nimekuwa naomba sana ushauri na kukwepa kufanya maamuzi yangu mwenyewe ili nipate watu wa kulaumu. Kuanzia sasa sitamlaumu tena mtu yeyote ambaye amewahi kunishauri. Na hata nipokee ushauri kutoka kwa nani, ni jukumu langu kutafakari ushauri ninaopokea na changamoto ninayopitia, kisha kufanya maamuzi ambayo nitakuwa tayari kuyasimamia.

NENO LA LEO.

“You can get discouraged many times, but you are not a failure until you begin to blame somebody else and stop trying.”
― John Burroughs

Unaweza kukatishwa tamaa mara nyingi, lakini hujashindwa bado, mpaka pale utakapoanza kulaumu wengine na kuacha kujaribu tena.

Hatima ya maisha yako ipo mikononi mwako, usilaumu mtu mwingine yeyote, fikiri kwa kina na fanya maamuzi utakayoyasimamia.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.