Katika maisha ya malezi ya mtoto kujifunza hapa duniani mzazi ndio Mwalimu wa kwanza katika elimu ya malezi ya mtoto nyumbani, shuleni na kadhalika.
Wazazi wengi huwa wakishampeleka mtoto shule basi wanasahau na kuwaachia majukumu yote walimu shuleni bila kujua mzazi ndio mwalimu wa kwanza na siyo mwalimu wa shuleni. Walimu wanabebeshwa majukumu juu ya malezi ya watoto na hiyo siyo kazi ya walimu bali ni ya mzazi. Wanafunzi wanakosa mwongozo bora nyumbani ndio maana inapelekea baadhi ya wanafunzi kufanya vibaya katika masomo yao. Wazazi wengine wanadiriki kufunga safari mpaka shule na kumshtaki mtoto wake kwa mwalimu eti mwalimu naomba nisaidie huyu mimi ameshanishinda katika malezi. Matatizo mengine ya malezi wasababishi wa kwanza ni wazazi na wala usihangaike kumtafuta mchawi katika malezi ya kumlea mtoto wako.
Ili mtoto wako awe vizuri kitaaluma mzazi anza kumpa mtoto wako elimu ya kujitambua na kumjengea mtazamo chanya, mabadiliko yanaanza nyumbani na hisani huanza nyumbani kama wasemavyo Waswahili. Inatakiwa kuwepo na mnyororo wa watu ili mtoto au wanafunzi wako waweze kufaulu vema katika masomo yao. Watu watatu katika mnyororo huo ni mzazi, mwanafunzi na mwalimu. Bila kufuata mnyororo huu mwanafunzi lazima apotee na ukiangalia siku hizi wanafunzi wamezungukwa na dunia yenye watu wenye kelele nyingi na bila kuwa makini na kelele hizi za dunia mwanafunzi lazima atapoteza dira. Mitandao ya kijamii iko mingi wanafunzi wako mashuleni lakini wameshajazwa kelele za dunia anashindwa abebe lipi.
Kwa hiyo, kuna takiwa kuwepo na ushirikiano wa hali juu kati ya mzazi, mwanafunzi na mwalimu ili kupata elimu bora na matokeo mazuri juu ya mwanafunzi, kumwachia majukumu yote mwalimu ndio chanzo cha kuporomoka kwa maadili ya wanafunzi. Katika zama hizi za taarifa usimfiche mtoto mwambie ukweli juu ya mambo yote, mpe elimu ya jinsia bila kuficha kwani utamsaidia sana kuendelea kuficha ni kuficha ugonjwa na matokeo yake kifo kitakuumbua.
Mambo muhimu ya kuzingatia kwa mzazi ili kuwa mwalimu mzuri wa mwanao;
1. Mpongeze Anapofanya Vizuri;
Mtoto ana haki ya kupongezwa pale anapofanya vizuri katika masomo au mambo mengine. Hakuna binadamu asiyependa kupongezwa pale anapofanya vizuri. Kumpongeza mtoto kunampatia faraja, kujiamini , kupata hamasa ya kufanya vema tena na kuweka juhudi kubwa ili kufikia kiwango cha juu kabisa. Kupongezwa kwa mwanafunzi kunampatia nguvu mara dufu ya kuendelea kuwa mshindi. Lakini wazazi wengine wamekuwa tofauti kabisa hajui hata kumpongeza mtoto wala hata kumpa zawadi ili kumchochea mtoto katika bidii yake bali mtoto anaachwa nyuma kama vile maisha ya bata na watoto wake bata huwa anatangulia mbele yeye na kuwaacha watoto nyuma hii siyo nzuri kabisa katika kumjenga mtoto kisaikolojia.
SOMA; Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Malezi Ya Watoto Ili Kuwaandaa Kufikia Mafanikio.
2. Mpe Nafasi Akosee;
Mtoto anapokosea ndio anajifunza na kupotea njia ndio kujua njia. Usiwe mkali sana kwa mtoto anapokosea muoneshe dira ili aweze kufika salama kwenye safari yake. Swali lolote kama ulishawahi kuulizwa na ukakosea ukiulizwa mara ya pili huwezi kukosa kwanza utafanya kwa umakini kwa sababu baada ya kushindwa mara ya kwanza utajifunza kwa bidii ili ulijue likijitokeza tena mbele yako huwezi kulikosa. Kukosea ni sehemu ya kujifunza.
3. Mpe Nafasi Ya Kujaribu;
Mtoto anatakiwa afundishwe kufanya maamuzi akiwa angali mdogo. watu wengi ni wakubwa mpaka leo hii lakini wanashindwa kufanya maamuzi wamezoea kufanyiwa maamuzi katika maisha yao mpaka wanakua wakubwa. Mpe nafasi mtoto ajaribu kwani kujaribu siyo kushindwa. Ukimlea mtoto na kumzoesha afanye maamuzi binafsi achague itamsaidia mbeleni kuwa shujaa na siyo hodari.
4. Kuwa Rafiki Wake Wa Karibu;
Mzazi unapaswa kua rafiki wa karibu wa mtoto wako. Kuna mambo mengine mtoto hawezi kukuambia wewe kama mzazi kama usipojenga urafiki wa karibu. Muda mwingine unavua uzazi na unakua rafiki wa mtoto wako hapo utamjenga vizuri sana, kisaikolojia atajisikia huru kukuambia mambo muhimu yanayomsibu. Lakini ukiwa mzazi kauzu hucheki na watoto wako unamtengenezea mazingira mabaya ya kutokua na uhuru na wewe na kuogopa pia.
5. Kuwa Mdadisi Juu Ya Mtoto Wako;
Baada ya kumjengea mazingira mazuri ya kuwa karibu naye utapata nafasi ya kumdadisi mwanao anapenda nini na yuko vizuri katika eneo gani. Hapa ndio njia pekee ya kugundua mwanao au mtoto wako ana kipaji gani. Baada ya kugundua kipaji cha mtoto sasa hapo ndio fursa kwako wewe kama mzazi kukuza na kuendeleza kipaji cha mtoto wako. Ukiwa mzazi wa aina hii hakika utapata matokeo mazuri sana ya mtoto ndani na nje.
SOMA; Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Malezi Ya Watoto Ili Kuwaandaa Kufikia Mafanikio.
6. Mtengenezee Sehemu Ya Kuhifadhi Kumbukumbu Zake;
Watoto wanatakiwa watengenezewe sehemu nzuri ya kuhifadhi kumbukumbu muhimu kama vile faili au mafaili ili aweze kuweka taarifa zake muhimu. Kuna wazazi wengine hawajui hata umuhimu wa kumtafutia cheti cha kuzaliwa mtoto wake. Unaweza kumuuliza mzazi mtoto wake kazaliwa mwaka gani tarehe na mwezi hajui hili jambo la aibu sana. Cheti cha kuzaliwa ni muhimu sana kwa mtoto wako. Cheti cha kuzaliwa hifadhi katika faili lake maalumu na nyaraka nyingine muhimu na mitihani yake yote kuanzia darasa la awali mwekee katika faili lake itamjengea nidhamu nzuri katika maisha yake.
Hivyo basi, mzazi anatakiwa kumjengea mtoto uwezo wa kujiamini, kumtengenezea mazingira bora ya sasa na ya baadaye muda mwingine mbadilishie mazingira mtoto mpeleke sehemu ambazo anaweza kubadilisha mawazo, kujifunza mambo mbalimbali. Mazingira mapya yanamfanya mtoto ajisike vizuri na kuhisi anapendwa. Upendo ni silaha nzuri katika malezi ya mtoto wako.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com