Katika biashara zote, kuna maeneo ambayo ni muhimu sana, ambayo ndiyo yanafanya biashara iweze kusimama na kwenda. Na kuna maeneo mengine ambayo ni muhimu, lakini sio sana, kiasi kwamba hata yasipopewa nguvu kubwa biashara bado inakwenda vizuri. Sisemi kwamba usizingatie eneo fulani la biashara yako, bali ninachokwambia ni kwamba kuna maeneo yanahitaji nguvu zaidi ili biashara yako iweze kwenda vizuri.

Kama wewe ni mfanyabiashara makini najua tayari umeshaweka malengo yako ya kibiashara kwa mwaka huu 2016. Na kama hujaweka bado, unaweza kuweka sasa kwani bado mwaka ni mchanga, tupo kwenye mwezi wa kwanza bado. Unaweza kuyaweka malengo yako ya kibiashara na ukaanza kuyafanyia kazi mara moja.

Leo katika makala hii ya kona ya mjasiriamali, tunakwenda kuangalia maeneo matatu muhimu kwenye biashara yako, ambayo unahitaji kuongeza nguvu zaidi kwa mwaka huu 2016. Kwa kuweka nguvu maeneo haya biashara yako itakua na kuweza kutengeneza faida kubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali. Karibu twende pamoja kuangalia maeneo haya matatu na kama tayari una malengo uyasisitize haya na kama bado hujaweka malengo basi uanzie kwenye maeneo haya matatu.

Eneo la kwanza ni masoko.

Kitu kimoja ninachoweza kukuhakikishia kwamba kuna watu ambao wangefaa kuwa wateja wako, lakini hawajui kama biashara yako ipo. Wana shida ambazo wewe ungeweza kuzitatua, na wapo tayari kugharamia, lakini hawajui kama wewe upo na unafanya biashara inayoendana na wanachotaka. Sasa unawapataje hawa watu? Ni lazima taarifa zako ziwafikie. Na taarifa zako zinawafikiaje? Hapa ndipo eneo la masoko linapokuwa muhimu sana kwenye biashara yako.

Mwaka huu 2016 hakikisha unaweka nguvu kubwa kwenye eneo lako la masoko, andaa kampeni za kuitangaza biashara yako ili iwafikie watu wengi zaidi. Na sio lazima utumie gharama kubwa kuliko majibu utakayopata, unaweza kuanza na kampeni za kutengeneza vipeperushi na kuvitoa kwa watu wanaoweza kuwa wateja wako, kutumia mitandao ya kijamii, kutumia makundi ya kijamii ambapo unahusika. Popote unapokuwa kwa mwaka huu 2016 hakikisha watu wanaokuzunguka wanajua unafanya nini na unawezaje kuwasaidia kwa yale matatizo wanayopata yanayohusiana na kile unachofanya.

Pia watumie wateja ulionao sasa kukuletea wateja wengi zaidi. Washawishi na wahamasishe kuwaambia wengine wanaoweza kunufaika na biashara unayofanya. Na unaweza kuwapa motisha kwa kufanya hivyo. Weka juhudi kubwa kwenye masoko, na kadiri biashara yako inavyopata wateja wengi, ndivyo itakavyokuwa kubwa na kukuletea faida.

Eneo la pili ni mtaji au fedha.

Ni lazima kwa mwaka huu 2016 uweze kukuza mtaji wako zaidi, kama kweli unataka biashara yako ikue zaidi. Unakuzaje mtaji, hilo ndio muhimu unalotakiwa kulifanyia kazi na kuweka juhudi. Kikubwa ni kuhakikisha biashara yako inakuza mtaji, na hivyo kuweza kutoa huduma na mahitaji mengi zaidi na kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi.

Kuna njia nyingi unazoweza kutumia kuongeza mtaji wa biashara yako. unaweza kuanza kwa kurudisha sehemu kubwa ya faida unayopata kwenye mtaji. Hapa unahakikisha ile faida unayopata, sehemu kubwa inarudi kuongeza mtaji, na hivyo unapunguza utegemezi au matumizi kutoka kwenye biashara yako. Hii ni njia bora sana ya kukuza mtaji wako, ila pia inaweza kukuchukua muda mrefu kufikia lengo.

Njia nyingine unayoweza kutumia kukuza mtaji wako kwa mwaka huu 2016 ni kutafuta mtu au watu ambao unaweza kuingia nao ubia wa kibiashara kwa mwaka huu. Na ili uweze kupata mtu au watu hawa ni lazima biashara yako iwe inaeleweka vizuri kiasi kwamba ukimwelezea mtu anaona ni kitu kinachofaa kuwekezea.

Kama njia hizo mbili bado haziwezi kukupatia mtaji unaotaka kuongeza kwa mwaka huu 2016, basi unaweza kwenda kwenye njia ya tatu ambayo ni mkopo wa kibiashara. Siku hizi kuna taasisi nyingi ambazo zinatoa mikopo ya kibiashara, jua ni taasisi gani itakufaa wewe na malengo yako. unahitaji kuwa na biashara iliyosajiliwa na inayoendeshwa vizuri ili kuweza kupata mkopo. Hivyo kama bado hujaiweka vizuri biashara yako, kwa kuisajili na kuiendesha vizuri, anza kufanyia kazi hilo mapema sana ili ujiweke kwenye nafasi nzuri ya kupata mkopo.

Eneo la tatu ni kwenye wasaidizi wa biashara (wafanyakazi).

Hili ni eneo muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako. wafanyakazi wako ndio wateja wako wa kwanza kabisa kwenye biashara yako. wafanyakazi wako wanaweza kuvutia wateja zaidi waje, au wanaweza kufukuza wateja wako. Ni vyema kuhakikisha umeajiri watu wanaopenda kweli kufanya kile ambacho umewaajiri kufanya, na pia kuwapa motisha na hamasa ya kuweka juhudi zaidi kwenye kazi yako.

Pia hakikisha wafanyakazi wako wanapata mafunzo au semina ya kibiashara itakayowafanya kuongeza ufanisi wao, kujituma zaidi na kuongeza tija kwenye kazi zao na hivyo biashara yako kunufaika zaidi.

Maeneo haya matatu, wateja, mtaji na wafanyakazi yanahitaji uyafanyie kazi sana kwa mwaka huu 2016 maana haya ndiyo yanayobeba biashara yako. kutetereka kwa eneo moja kati ya hayo, kutaleta madhara makubwa sana kwenye biashara yako. usikubali mwaka huu 2016 uendelee kufanya mambo kama ambavyo ulikuwa umezoea kufanya, anza kuweka juhudi zaidi na utaona majibu bora zaidi. Nakutakia kila la kheri.