Nashawishika na ninaamini kabisa, bila ya shaka yoyote kwamba wewe rafiki yangu kuna kitu unaweza kufanya. Kitu hiki ni tofauti kabisa na cha kipekee na kinaweza kufanya maisha ya wengine kuwa bora sana.

Iwe ni kupitia kazi unayofanya sasa, iwe ni kupitia biashara yako, iwe ni kupitia vipaji ulivyo navyo, kuna kitu unaweza kufanya, ambacho sio cha kawaida. Kinaweza kuwa kawaida kwako, ila kwa wengine ni kitu kikubwa sana, na kinaweza kubadili maisha yao kabisa.

Leo hii angalia ni mtu gani mmoja unaweza kumsaidia kwa chochote unachoweza kufanya. Chochote kile ambacho unaona kitakuwa msaada kwake kwa hali aliyonayo. Kisha angalia kama kimeweza kumsaidia kweli. Kama kimemsaidia basi angalia mwingine anayeweza kunufaika pia. Na kama hakijamsaidia angalia ni jinsi gani unaweza kuboresha zaidi.

Huo ni upande mmoja wa kuwasaidia wengine kwa kile ambacho tayari unacho, upande wa pili na ambao ni muhimu sana ni kwamba kwa njia hii unaanzisha biashara nzuri na kubwa. Na kama ilivyo kwamba biashara zenye mafanikio ni zile zinazotatua matatizo ya watu, kwa kuanza na mtazamo huu utakuwa na uhakika wa kutengeneza biashara nzuri ya baadaye.

Ni kipi ulichonacho, ambacho unaweza kukitoa kwa wengine na ukawasaidia kutatua matatizo yao? Fikiri leo na anza kuchukua hatua. Usijidanganye tena ya kwamba utaanza vizuri wiki ijayo, ni sasa au sio sasa. (soma makala ya ukurasa wa jana)

SOMA; WORLD CLASS; Dalili Saba Kwamba Tayari Wewe Una Mtizamo Chanya Utakaokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba kuna vitu ninavyojua ambavyo vinaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa wengine. Najua kwa kuanza kuvifanyia kazi naweza kuwasaidia wengine kuwa na maisha bora sana. Na wakati huo pia nitakuwa natengeneza biashara bora sana kwangu. Leo hii naanza kufanyia kazi vitu hivi kwa kuangalia mtu anayeweza kunufaika, na kuanza naye.

NENO LA LEO.

“Do not focus on money, instead focus on a problem that needs to be solved for the world..money will follow you as a bi-product.”
― Manoj Arora

Usifikirie kuhusu fedha tu, badala yake fikiria matatizo ambayo yanahitaji kutatuliwa kwenye dunia hii na yatatue… fedha zitafuata kama zao la kutatua matatizo hayo.

Leo hii angalia ni matatizo gani ya wengine unaweza kuyatatua kupitia kile unachofanya au unachojua. Kisha anza kuyatatua. LEO.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.