SIWEZI, kama yalivyo maneno mengine mengi ambayo watu hupenda kutumia hasa katika safari ya mafanikio, ni neno ambalo linatumika kuficha hali halisi.
Ukweli ni kwamba siwezi siyo neno linalosimama lenyewe, ni neno linaloficha vitu vingine ambavyo mtu anavyo. Na mara nyingi neno hili SIWEZI, halina uhalisia kwa yule anayelitumia. Japo wengi wamekuwa wakilitumia, hasa pale wanapokutana na wakati mgumu, au wanapohitajika kuweka juhudi zaidi.
Neno SIWEZI linaweza kuwa na maana mbili kubwa.
Maana ya kwanza ni SIJUI.
Kwa kuwa kusema sijui ni kitu kinachoweza kuonekana kama ujinga, lakini mara nyingi watu wanaposema SIWEZI sababu halisi ni kwamba hawajui. Mtu anaposema siwezi kufanya jambo fulani, ambalo ni muhimu sana kwake kufikia mafanikio, sababu halisi inaweza kuwa ni hajui jinsi ya kufanya jambo hilo.
Uzuri wa sababu ya SIJUI ni kwamba unatibika, na unatibika kwa kujifunza. Hivyo unaposema siwezi, hebu nenda ndani zaidi na jiulize kwa nini huwezi. Kama ni kwa sababu hujui, basi anza kujifunza mara moja. Unaweza kujifunza vitu vingi sana ambavyo ni muhimu kwako kufikia mafanikio.
Maana ya pili ni SITAKI.
Neno SITAKI ni neno kali sana, ambalo wakati mwingine unaweza kuogopa kumwambia mtu. Kwa sababu unaona atakuchukulia vibaya ya kwamba una kiburi au mkorofi. Hivyo umekuwa unatafuta neno laini kidogo, na hapo ndio unapoangukia kwenye neno SIWEZI. Mara nyingi unasema siwezi kuficha ukweli ambao ni SITAKI. Pale ambapo hutaki kufanya kitu, kwa sababu labda unaona siyo muhimu kwako, lakini bado unahitajika kufanya, ni rahisi kutumia neno SIWEZI na hakuna atakaye kusumbua zaidi. Na wakati mwingine unakuwa unajidanganya tu wewe mwenyewe, labda umefika hatua unatakiwa kuweka juhudi kubwa zaidi, na wewe hupo tayari kufanya hivyo basi unasema huwezi.
Uzuri wa sababu ya sitaki ni kwamba unaweza kuibadili kama utaanza kwa kubadili mtazamo wako. Kinachokufanya uone kwamba hutaki kufanya kitu fulani, ambacho ni muhimu kwako ni ule mtazamo ulioweka kwenye kitu hiko. Labda unaona ni kigumu, labda unaona siyo muhimu na mitazamo mingine. Hapa unaweza kuondokana na hali hii kwa kubadili mtazamo wako. Badala ya kuwa na mawazo hasi juu ya kitu, tafuta eneo chanya la kitu hiko na fikiri kwa uchanya, utapata hamasa ya kuendelea kufanya.
SIWEZI maana yake ni SIJUI au SITAKI. Ni vyema ukajua ipi sababu halisi ili uweze kuchukua hatua husika.
SOMA; Una Sababu Moja Tu, Nyingine Zote Ni Kuchagua.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba nimekuwa najiambia siwezi lakini kuna sababu ambazo zipo ndani ya neno hilo siwezi. Mara nyingi nakuwa sijui jinsi ya kufanya kitu au sitaki kufanya kitu hiko. Kwa yale mambo ambayo ni muhimu kwangu kufikia mafanikio, kama sijui nitajifunza na kama sitaki nitabadili mtazamo wangu juu ya mambo hayo.
NENO LA LEO.
“Whether you think you can, or you think you can’t–you’re right.”
― Henry Ford
Kama unafikiri UNAWEZA au unafikiri HUWEZI, uko sahihi kabisa.
Kile unachofikiri ndio kinachotawala maisha yako, kama unafikiri huwezi hakuna atakayekuwezesha. Kama unafikiri unaweza hakuna atakayekuzuia.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.