Kitabu WHY MOTIVATING PEOPLE DOESN’T WORK, kinaangalia kwa undano sayansi ya hamasa. Katika kitabu hiki tunajifunza mbinu mpya za kuwafanya watu wahamasike na kuchukua hatua zaidi. Kupitia kitabu hiki mwandishi Susan Fowler anatukumbusha kwamba huwezi kumhamasisha mtu, kwa sababu kilamtu tayari amehamasika. Unachoweza kufanya ni kujua mtu amehamasika kwenye nini ili aweze kubadilika na kuwa na hamasa sahihi kwake.

Kitabu hiki kinaweza kukusaidia mtu binafsi kubadili mtazamo wako wa kazi na maisha. Pia kinaweza kukusaidia kama wewe ni kiongozi au mwajiri ili kujua njia sahihi za kuwafanya wale unaowaongoza wahamasike na kuchukua hatua ya kuweka juhudi zaidi kwenye kazi zao na hata maisha yao.

Hapa nimekushirikisha mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu hiki. Yapitie na utapata vitu muhimu vya kufanyia kazi.

1. Watu mara zote wamehamasika, hivyo swali la kuuliza sio kama watu wamehamasika au la, ila kuuliza wamehamasika kufanya nini. Mtu kila mtu anafanya kile anachofanya kwenye maisha kutokana na hamasa aliyonayo. Hivyo njia ya kwanza kabisa ya kumsaidia mtu, au ya kumfanya awe na hamasa sahihi, ni kujua kwa sasa amehamasika na nini ndipo uweze kumpeleka kwenye hamasa sahihi kwake.

2. Kuna hamasa za aina mbili, hamasa ambazo ni chanya na hivyo zinamsukuma mtu kuchukua hatua bora zaidi. Na kuna hamasa ambazo ni hasi, ambazo zinamfanya mtu kuchukua hatua ambazo sio bora. Hamasa chanya inaanza na uwezo wa mtu kuchagua kile anachotaka yeye, na kukifanya kwa sababu kinaendana na misingi yake, madhumuni yake na anapendelea kukifanya. Hamasa hasi inaanza na pale mtu anafanya kitu kwa sababu analazimika kufanya, na pia kufanya kitu ili kuonekana, au kupata kitu fulani. Ni vyema mtu kuendeshwa na hamasa chanya kuliko hasi.

3. Mtu anapokuwa na hamasa chanya anakuwa na nguvu ya kuchukua hatua zaidi. Anakuwa anaona maana kubwa kwenye kile anachofanya na hii inamsukuma kuchukua hatua zaidi. Kwa njia hii anakuwa na maisha bora na yenye mafanikio.

4. Kuna makundi sita ya hamasa ambapo mtu anaweza kuwepo kwenye moja kati ya hilo. Na kila kundi mtu anakuwa na hali fulani inayomhamasisha au kutokumhamasisha kuchukua hatua.

Kundi la kwanza ni wale ambao wanafanya kitu ila mawazo yao hayapo pale kabisa. Kama ni mkutano wapo tu lakini hawafuatilii chochote kinachoendelea. Hawaoni thamani yoyote kwenye kile kinachoendelea na hivyo wanaona ni upotevu wa muda kwao tu.

Kundi la pili ni wale wanaosukumwa na hamasa ya nje, kama kuonekana, kupewa zawadi au motisha na vitu vingine vya nje. Hamasa hii ina kikomo chake.

Kundi la tatu ni wale ambao wanafanya kitu kwa sababu ni lazima wafanye, hawana namna nyingine. Hapa unafanya kitu kwa sababu usipofanya kuna adhabu, au utaonekana wa tofauti kwenye jamii.

Kundi la nne ni wale wanaofanya kitu kwa sababu kuna kitu fulani wanakithamini kwenye kile ambacho wanafanya. Hapa mtu anaona kua mchango kwake na kwa wengine kwa yeye kufanya hivyo.

Kundi la tano ni wale ambao wanafanya kitu kwa sababu kinatimiza moja ya madhumuni yao kwenye maisha. Hapa mtu anaona ana mchango mkubwa sana na maisha yake yanakuwa bora sana kwa yeye kufanya hivyo.

Kundi la sita ni wale ambao wanapenda na kufurahia sana kile wanachofanya.

Makundi matatu ya kwanza yanaongozwa na hamasa hasi na hivyo kushindwa kufanya makubwa, na makundi matatu ya mwisho wanaongozwa na hamasa chanya na hivyo kuweza kufanya makubwa.

5. Wazazi, walimu na viongozi wamekuwa wakitumia hamasa ya nje kuwafanya watu waongeze juhudi zaidi. Vitu kama zawadi, kupewa vyeo na vitu vingine vinavyohamasisha watu kufanya zaidi, vimekuwa vinatumiwa sana. Vitu hivi vinatoa hamasa ya muda mfupi tu ila baadae vinakuwa na madhara hasi kwa yule anayehamasika kwa vitu vya nje. Hamasa ya kweli ni ile inayotokana na vitu vya ndani ya mtu mwenyewe, kuthamini kitu, kukipenda na kuwa kinaendana na madhumuni yake.

6. Watu pia hawajui hamasa yao ya kweli inatoka wapi. Hivyo wanapokuwa hawapati furaha kupitia kazi zao hudai mshahara zaidi. Na hata wanapopata mshahara ule bado hujikuta wakiwa kwenye hali ile ile. Hii ni kwa sababu hamasa ya ndani yao wenyewe bado hawajaijua na hivyo kusumbuka sana. Wengine hubadili hata kazi, na kujikuta bado wanajiona hovyo vile vile. Suluhisho ni kujua hamasa ya ndani ya mtu inatokana na nini.

7. Kadiri viongozi wanavyoshindwa kujua hamasa halisi ya mtu, na hivyo kutumia hamasa za nje, ndivyo wanavyozidi kukosa matokeo wanayotarajia. Viongozi hufikiri wakiwaongezea watu kipato au kuwapa zawadi basi watazalisha sana, wanafanya hivyo na uzalishaji unakuwa kidogo sana. Wanapozidi kusukuma ili wapate matokeo wanayotaka, ndivyo mambo yanazidi kuwa mabaya.

8. Kuna kitu kimoja ambacho kipo ndani ya kila mwanadamu, na kitu hiki kinaweza kutumika vizuri sana kwenye kuhamasisha zaidi. Kila mtu ana tamaa ya kustawi. Kila mtu anataka kukua zaidi, kuendelea zaidi na kuwa bora zaidi ya alivyokuwa hapo nyuma. Kila mmoja wetu anakazana afikie uwezo mkubwa ulio ndani yao. Mtu akishajua lile eneo ambalo anataka kukua zaidi, basi hamasa yake imeshajulikana.

9. Kuna mahitaji matatu ya kisaikolojia ambayo watu wanayatafuta kwenye maisha na kazi zao. Kwa kuwepo na mahitaji hayo watu wanahamasika sana kufanya kitu chochote ambacho kinawapatia mahitaji hayo matatu.

Hitaji la kwanza ni UHURU. Kila mtu anapenda kuwa huru kuchagua kile ambacho anajua ni muhimu kwake na anapenda kufanya. Kama kazi inampa mtu uhuru wa kuchagua anaifanyaje, inamhamasisha mtu kufanya zaidi.

Hitaji la pili ni UHUSIANO, hapa ni yale mahusiano yetu na wengine kupitia kile ambacho tunafanya. Kama tunachofanya kinawasaidia wengine au kufanya maisha yao kuwa bora zaidi, basi tunahamasika ziadi.

Hitaji la tatu ni UWEZO/ UBOBEZI, hapa mtu anakuwa na uwezo wa kufanya kazi yake kwa ubora wa hali ya juu na anakuwa amebobea. Wale ambao wanaweza kuifanya kazi yao vizuri, wanakuwa wamehamasika zaidi kuliko ambao hawawezi.

10. Sababu nyingine kubwa ambayo inafanya hamasa ya nje isiwasaidie watu ni kwamba inawalazimisha kujifunza. Kujifunza hakulazimishi, bali ni kitu kinachotoka ndani ya mtu mwenyewe. Huwezi kumlazimisha mtu kujifunza, bali unaweza kumjengea mazingira mazuri kwake yeye kujifunza na akawa bora zaidi.

11. Mahitaji hayo matatu ya kisaikolojia, yaani UHURU, UHUSIANO NA UBOBEZI, yana mchango mkubwa sana kwenye hamasa ya mtu. Mtu yeyote ambaye anafanikiwa kwenye kile anachofanya, lazima vitu hivyo vitatu vipo pamoja. Na wale ambao wapo tu na hawajui wanaelekea wapi, mara zote utakuta wanakosa kimoja au hata vyote kati ya hivyo. Mjumuiko huo ni muhimu sana, hakikisha kwenye kitu chochote unafanya, unatimiza mahitaji hayo matatu.

12. Hadithi halisi ya hamasa ni kwamba watu wanapenda kujifunza, kukua, kufurahia kile wanachofanya, kujenga mahusiano mazuri na wengine na kuwa na mchango chanya kwenye maisha ya wengine. Hii inatokea ndani ya kila mtu na tunayo kwa asili. Hivyo kama unataka kuhamasika au kuhamasisha wengine, angalia ni jinsi gani wanaweza kupata vitu hivyo kwa kile wanachofanya au kutaka kufanya.

13. Kufanya kitu kwa sababu umesukumwa kufanya, ni hatari zaidi. Hata kama msukumo huo unatoka ndani yako mwenyewe. Ni hatari kwa sababu msukumo wowote huwa haudumu, na hivyo msukumo unapoisha na wewe unakuwa umekwisha. Kitu muhimu ni kuwa na hamasa ambayo inatoka ndani, hii ndio itakuwezesha kuendelea kuweka juhudi hata kama mambo yamekuwa mabaya au mazuri. Msukumo huisha pale mambo yanapokuwa mazuri.

14. Ili kuweza kuitumia hamasa vizuri, ni lazima mtu aweze kujiongoza na kujidhibiti mwenyewe. Kushindwa kujisimamia na kujidhibiti utashindwa kuendelea kufanya makubwa hata kama umehamasika kiasi gani. Kwa kuweza kujidhibiti unazuia hisia zako kuingilia kile ambacho unakifanya.

15. Kuna vitu vitatu ambavyo unaweza kufanya ili kuweza kujisimamia na kujidhibiti kwenye maisha yako.

Kitu cha kwanza ni kuwa na fikra sahihi juu ya kile ambacho kinaendelea kwenye maisha yako kwa wakati husika. Kujua unafanya nini na kwa nini na vitu gani vinakuzunguka.

Kitu cha pili ni thamani, hii ni ile thamani ambayo umeweka kwenye kitu ambacho unakifanya.

Kitu cha tatu ni dhumuni, kujua dhumuni kubwa la kile ambacho unakifanya, kunakusaidia sana katika kukifanya.

16. pale ambapo unakuwa hufikiri sawa sawa kwenye kile unachofanya au kinachoendelea ni rahisi sana kujikuta unaingia kwenye hasira au ugomvi na wengine. Hapa unajikuta unapoteza muda wako kwa mambo ambayo sio muhimu kwako. Kwa kuhakikisha kila wakati una fikra sahihi, kunakusaidia kuepuka mambo ambayo sio muhimu, ambayo yangekupotezea muda.

17. Watu wanaofanikiwa sana na wanaofikia makubwa hawasukumwi iwe kutoka nje au ndani yao, bali wanakuwa na dhumuni kubwa ambalo kulitekeleza ndio jukumu kubwa kwenye maisha yao. Dhumuni hilo linakuwa na maana kubwa kwenye maisha yao.

18. Watu ambao wanathamini au wana maadili ambayo wanayasimamia, wanahamasika zaidi kuchukua hatua kuliko wale ambao hawana maadili. Maadili ni sehemu muhimu sana ya kumsaidia mtu kuweza kujisimamia na kujidhibiti. Kwa kuwa na utaratibu wa vitu fulani ambavyo ni lazima kufanya na vingine ambavyo ni mwiko kufanya, kunamfanya mtu apunguze kupoteza muda.

19. Kumpa mtoto zawadi kwa kufanya kile ambacho anatakiwa afanye, mfano kusoma au kufanya kazi zake za nyumbani, ni njia ambayo wazazi wengi wanaona ni rahisi kujenga tabia nzuri kwa watoto. Ila hii ni njia mbovu sana kwa sababu inaua kabisa vipaji na ubunifu wa watoto. Kwa sababu wanaacha kufanya kwa sababu wanapenda na badala yake wanafanya ili wapate kitu fulani.

20. Sayansi mpya ya mafanikio inatutaka sisi kujua kile ambacho kinawahamasisha watu kutoka ndani yao wenyewe. Badala ya kukazana na vitu vya nje ambavyo vinaleta hamasa ya muda tu, kujua hamasa ya ndani kunamwezesha mtu kufanya kwa ubora na kuweza kufikia mafanikio makubwa. kama bado wewe mwenyewe hujajua hamasa yako ya ndani inatokana na nini fanyia kazi hilo. Kama una wafanyakazi au hata watoto ambao unataka wahamasike zaidi, jua ni kipi kinawahamasisha kutoka ndani yao, na wawezeshe kutumia hiko.

Bila ya hamsa ni vigumu sana kwako kufikia mafanikio makubwa. Hakikisha unayo hamasa ya kutosha na hamasa hii inatoka ndani yako mwenyewe na sio nje. Pia kama kuna watu unahusika nao, wasaidie pia wapate hamasa kutoka ndani yao. Kila la kheri.