Kuna njia mbili za kupoteza muda. Njia ya kwanza ni kupoteza dakika na njia ya pili ni kupoteza masaa. Ni njia tofauti kwa sababu upotevu wa muda unatofautiana kwenye njia hizo.
Tunapoteza dakika kwa bahati mbaya, bila ya kujua, yaani ni kama zinatuponyoka. Na ni vigumu sana kujua kwa hakika ya kwamba unapoteza dakika. Kwa sababu zinapotea haraka sana na ni vigumu kuona kama haupo makini.
Unapotezaje dakika? Unapoteza dakika pale ambapo unafanya jambo moja, halafu kitu kingine kidogo kikaingilia. Labda simu imeita, ukaacha na kupokea simu hiyo, na huenda simu hiyo siyo muhimu kama jambo ulilokuwa unafanya. Au unafanya jambo na ghafla mawazo yakahama kutoka kwenye jambo hilo na ukaanza kufikiria kitu kingine ambacho hakihusiani kabisa na unachofanya. Hapo kuna dakika unazipoteza, na usipokuwa makini zinaweza kuwa nyingi sana.
Tunapoteza masaa kwa makusudi, kwa kujua kabisa, yaani ni kama unaamua kuyatupa masaa. Unaweza kuwa unajua kabisa ya kwamba unapoteza masaa yako, lakini hutaki tu kuchukua hatua, au umeamua kupuuzia, na hii inazidi kukupoteza.
Unapotezaje masaa? Unapoteza masaa kwa kuamua kufanya kitu ambacho wewe mwenyewe unajua siyo muhimu. Unajua kabisa unafanya kitu na unajua kuna kingine muhimu ungeweza kuwa unakifanya kwa muda huo. Lakini unaamua tu kutokufanya, kwa sababu unazoweza kuwa nazo wewe mwenyewe. Kwa mfano ni muda umepanga kufanya kazi lakini upo kwenye mitandao ya kijamii, upo kwenye mabishano au unafuatilia udaku.
Wote tunajua muda ndiyo rasilimali adimu na ghali sana kuliko rasilimali nyingine zote. Lakini hatulioni hilo kwa sababu tunaona muda tunao kila siku. Mpaka pale unapokuwa umeshachelewa ndiyo unaanza kuiona thamani ya muda.
Linda dakika zako, okoa masaa yako. linda dakika kwa kuhakikisha vitu vidogo vidogo havikutoi kwenye jukumu lako kubwa unalofanya. Na okoa masaa yako kwa kuhakikisha kile unachofanya ndiyo muhimu sana kwako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba nimekuwa napoteza dakika zangu bila ya kujua na nimekuwa napoteza masaa kwa kujua kabisa. Kuanzia sasa naimarisha ulinzi wa muda wangu, nitalinda kila dakika na nitaokoa kila saa yangu ambayo ingeotea kwa kufanya kitu ambacho sio muhimu kwangu.
NENO LA LEO.
We must use time wisely and forever realize that the time is always ripe to do right.
Nelson Mandela
Ni lazima tutumie muda wetu kwa busara na tujue ya kwamba mara zote muda ni muafaka wa kufanya kilicho sahihi.
Linda dakika unazopoteza bila ya kujua na okoa masaa unayopoteza kwa kujua. Tumia muda wako vizuri kufanya kile kilicho sahihi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.