Moja ya falsafa nzuri na iliyodumu kwa miaka mingi kuhusu upendo ni mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Hii ni falsafa nzuri sana kwa sababu wote tunajua dunia bila ya upendo haiwezi kwenda. Upendo ndio umeifikisha dunia hapa, na upendo ndio utaendelea kuifanya dunia iendelee kuwepo. Japokuwa kuna matukio yasiyo ya upendo yanayoleta matatizo kwa wengine, lakini bado upendo ni muhimu na tunauhitaji sana.
Wanafalsafa wengi na walimu wazuri wa enzi na enzi walisisitiza sana falsafa hii ya mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Na pia kuna ile sheria kuu isemayo usimfanyie mwingine kile ambacho usingependa kufanyiwa wewe. Zote hizi ni falsafa zinazohamasisha upendo kwa wengine na kupitia upendo kwa pamoja tunaendelea zaidi.
Lakini kuna tatizo moja kubwa sana kuhusu falsafa hii ya mpende jirani yako kama unavyojipenda wenyewe. Na tatizo hili ndio linapelekea tunaona matukio mengi yanayotokea baina ya watu ambayo yanaashiria kutokuwepo kwa upendo leo tutajadili tatizo hili kwa kina, tutaona suluhisho la tatizo hili na tutaondoka na njia mpya ya upendo.
Tatizo la mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe ni kuweka msisitizo kwenye kuwapenda wengine. Na kusahau chanzo kikuu muhimu cha upendo, ambacho ni kuanza kujipenda wewe mwenyewe kwanza. Msisitizo wa kwanza kabisa kwenye upendo ni mtu kujipenda yeye mwenyewe, ndiyo sasa aweze kumpenda jirani yake. Mtu ambaye yeye mwenyewe hajipendi, akitumia falsafa hiyo ataharibu wengi zaidi.
Ni rahisi kuona kwamba kila mtu anajipenda, na hivyo msisitizo uwe kwamba watu wawaende wengine kama wanavyojipenda wao wenyewe. Lakini hii siyo kweli, watu wengi wanaotuzunguka hawajipendi, huenda hata sisi wenyewe hatujipendi, sasa tutawezaje kuwapenda wengine kama tunavyojipenda sisi wenyewe?
kwa mfano mtu ambaye ni mlevi wa kupindukia, anajua kabisa ulevi anaotumia una madhara kwake, lakini bado anatumia, unafikiri anajipenda kweli? Anaithamini nafsi yake na hata maisha yake? Au mtu ambaye anavuta sigara, pakiti yenyewe ya sigara imeandikwa uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako, lakini bado yeye anavuta, unafikiri anajipenda kweli? Najua kuna kuingia kwa tabia hapo, lakini bado nashawishika kwa mtu anayefanya hivyo bado ule upendo wa kweli haujaingia kwenye maisha yake.
Mifano ipo mingi sana, ya namna gani watu wengi hawajipendi wao wenyewe. Kama tulivyojifunza kwenye makala za nyuma za falsafa, kinyume cha hofu ni upendo, hii ina maana kuwa, unapokuwa na hofu upendo unakuwa haupo. Je ni wangapi ambao wanaishi maisha yao yote kwa hofu? Ni wangapi ambao wanahofia biashara zao zitakufa, kazi zao zitaisha na maisha yao yatakuwa magumu sana? Watu hawa wenye hofu watakuwa tayari kufanya jambo lolote, hata kama litakuwa na madhara kwa wengine. Ni vigumu sana mtu huyu kuweza kumpenda mtu mwingine, maana hata kwake mwenyewe upendo haupo.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Nguvu Moja Unayomiliki Yenye Uwezo Wa Kuibadili Dunia.
Tunafanya nini ili kuweza kuimarisha falsafa hii?
Kama tulivyoona hapo juu, kama kuna kitu muhimu kwenye dunia hii basi ni upendo. Na mara zote zimekuwa nikiamini kwamba dini ya kweli kabisa ni upendo, maana upendo ndio utatuwezesha sisi kuishi maisha ya furaha na mafanikio.
Suluhisho la kweli la upendo ni kuanzia kwenye misingi kabisa. Na hapa kuna misingi mitatu mikuu ya upendo, ambayo kila mmoja wetu ni lazima aanze kuifanyia kazi sasa kama anataka kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa. na kwa kuwa lengo letu ni kutengeneza falsafa mpya ya maisha yetu, basi ni muhimu tufanyie kazi maeneo haya matatu muhimu sana kwenye maisha yetu.
Eneo la kwanza; jipende wewe mwenyewe.
Eneo la kwanza na muhimu sana ni kujipenda wewe mwenyewe. Jipende wewe mwenyewe, na jipende kweli. Kwa kuanzia kwa kujipenda, mengi kwenye maisha yatakwenda vizuri.
Ili ujipende, kwanza ni lazima ujijue vizuri, ujue unatoka wapi, uko wapi na unakwenda wapi. Ni lazima ujue ni lipi dhumuni lako kubwa kwenye maisha yako hapa duniani. Na lazima ujue ni alama gani unataka kuacha hata pale utakapoondoka kwenye dunia hii.
Pia unahitaji kuujua mwili na akili yako, na unahitaji kuvilinda vizuri sana kwani hivi ndio vinavyokutambulisha wewe. Chochote kinapopata tatizo, ni vigumu kuendelea kujipenda wewe mwenyewe.
Kwa kujijua vizuri, na kujua ni kipi unataka kwenye maisha yako, kunakuondolea hofu na kukuletea kujiamini. Ni kupitia kutokuwa na hofu na kujiamini ndipo unapata upendo mkubwa sana kwako binafsi.
Eneo la pili; wapende wote wanaokuzunguka.
Hapa sasa ndio tunakuja kwenye falsafa ile ya enzi na enzi, mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Jirani yako ni mtu yeyote anayekuzunguka, kuanzia kwenye familia, ndugu, jamaa, marafiki na hata wale wanaokuzunguka kwenye eneo lako la kazi.
Ukishajipenda wewe mwenyewe, na ukajua ni kipi unataka kufanya na maisha yako, hapa sasa unaweza kuhamishia upendo huu kwa wengine. Unawapenda wengine pale unapojali kuhusu maisha yao, pale unapokuwa na mchango kwa wao kuweza kuwa na maisha bora.
Upendo kwa wengine unachochea ushirikiano na kupitia ushirikiano hakuna kinachoshindikana. Ndio maana ni muhimu sana tukaanza na upendo. Matatizo mengi ambayo tunayapitia kwenye maisha, baina yetu na wengine, yanaanzia pale ambapo upendo unakuwa umekosekana. Upendo ukikosekana watu wanawaibia wengine, wanajaribu kuwaua, au wanawatapeli. Lakini upendo unapokuwepo, matendo haya yanapotea kwa sababu upendo una nguvu kubwa sana.
Eneo la tatu; penda kile unachofanya.
Hapo ulipo, kuna kitu unafanya ambacho ndio kinakuwezesha kuendesha maisha yako. Inawezekana umeajiriwa na hivyo ni mfanyakazi, inawezekana umejiajiri au unafanya biashara na shughuli nyingine nyingi. Shughuli unazofanya, zina mchango muhimu sana kwenye maisha yako binafsi na maisha ya wale wanaokuzunguka pia.
Ukipata matatizo kwenye kazi yako au biashara yako, ni rahisi sana kwa matatizo hayo kuingia kwenye maeneo mengine ya maisha yako, kama familia na mahusiano. Kwa mfano kama kazi inakupa msongo wa mawazo, msongo huu utaathiri familia yako na hata marafiki zako.
Ili kuhakikisha shughuli zetu haziwi chanzo cha kuharibu upendo, tunahitaji kupenda sana kile ambacho tunafanya. Iwe ni kazi au biashara, kama ndiyo unafanya kwa sasa, ipende sana, yaani sana. Hata kama sio kazi ya ndoto yako, kwa kuwa umechagua kuifanya sasa, ipende sana. Upendo huu kwenye kile unachofanya kwanza unafanya maisha yako kuwa ya furaha na pia unakuwezesha kuziona fursa nyingi zaidi kwenye kile unachofanya.
Kwa kupenda kile unachofanya utakifanya kwa moyo na hivyo kutoa majibu mazuri sana. Wale wanaotegemea majibu hayo watakuwa na maisha bora na hivyo utakuwa umezidi kusambaza upendo. Na kitu muhimu zaidi ni kwamba wanaofanikiwa ni wale wanaopenda sana kile wanachokifanya.
Katika falsafa yetu mpya ya maisha tunayoijenga, upendo ndiyo nguzo kuu. Na upendo huo unaanza na sisi kujipenda wenyewe, kuwapenda wale wanaotuzunguka na kupenda kile ambacho tunakifanya. Tukiweza kuweka upendo kwenye maeneo yote hayo matatu maisha yetu yatakuwa bora sana.
Nakutakia kila la kheri katika kujenga falsafa mpya ya maisha ya mafanikio.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.