Moja ya vitu ambavyo dunia imekuwa inatudanganya sana, na tunadanganyika ni kwamba furaha ipo mwisho. Yaani teseka sasa na baadaye utakuwa na furaha, baada ya kufikia kile ambacho unakitafuta au kukifanyia kazi.
Huu ni uongo, na ndio imesababisha maisha ya wengi kuendelea magumu hata baada ya kupata kile ambacho wamekuwa wanakipigania kwa muda mrefu.
Ukweli ni kwamba furaha haipatikani mwisho wa kitu, bali inapatikana kwenye mchakato zima wa kufikia kile ambacho unakitaka.
Kwa mfano ukiwa shuleni, ni rahisi kushawishika kwamba siku utakayomaliza ndiyo utakuwa na furaha sana. Na unaweza kuipata furaha hiyo kweli, lakini miaka inayokuja ni kipi utakikumbuka? Utakumbuka siku ile ya kumaliza au siku zote za masomo yako? wote tunajua unakumbuka zaidi zile siku zote za masomo, na mambo yaliyokuwa yanaendelea kuliko utakavyokumbuka ile siku ya kuhitimu.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye malengo yetu ya maisha, hata kama ni makubwa kiasi gani, furaha haiji pale unapoyafikia, bali pale unapoyaendea malengo hayo. Furaha haitakuja pale unapopata mabilioni, bali kwenye mchakato mzima wa kuyapata mabilioni hayo. Kile unachofanya na jinsi unavyokwenda na wengine, vitabaki kwenye kumbukumbu zako daima kuliko kumbukumbu za kufikia lengo hilo.
Kinachofanya furaha kuu isiwe mwishoni mwa lengo ni kwa sababu unapokamilisha lengo moja, kuna lengo jingine kubwa zaidi la kufikia. Hivyo kama unasubiri ukikamilisha ndio uwe na furaha, itaisha haraka kwa sababu kuna lengo jingine kubwa zaidi unahitaji kuanza kulifanyia kazi. Kama umemaliza sekondari, unahitaji kuendelea na chuo, kama umefikia lengo la milioni 100 unahitaji kuwa na lengo la bilioni 1.
Chukua hatua sasa ya kufurahia ile safari unayopita, usisubiri mpaka mwisho, anza sasa kufurahia, kwa kila hatua unayopiga kwenye maisha yako. na maisha yako yatakuwa bora sana.
SOMA; Fanya Mambo haya matatu kuwa na maisha bora na yenye furaha.
TAMKO LANGU;
Nimejikumbusha ya kwamba furaha haitokani na kufikia kitu, bali inatokana na mchakato mzima wa kufikia kitu hiko. Sitakubali kudanganyika tena kusubiri kitu ndio niwe na furaha, nitakuwa na furaha kwenye kila hatua ninayopiga kwenye maisha yangu, kwenye kila kitu ninachofanya.
NENO LA LEO.
“Happiness is a journey, not a destination; happiness is to be found along the way not at the end of the road, for then the journey is over and it’s too late. The time for happiness is today not tomorrow.” ~ Paul H Dunn
Furaha ni safari na sio mwisho; furaha inapatikana wakati wa safari na sio mwisho wa safari, kwa sababu mwisho wa safari, safari inakuwa imeisha na umeshachelewa. Muda wa kuwa na furaha ni leo na sio kesho.
Usisubiri mpaka upate kitu fulani ndiyo uwe na furaha, kuwa na furaha sasa wakati unaendea hiko unachotaka. Furaha ipo kwenye mchakato na sio mwishoni.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.