Moja ya changamoto ambayo wafanyabiashara wapya wanakutana nayo pale wanapoingia kwenye biashara, ni kukazana kwa kila kitu na hatimaye kuanza biashara, halafu wanakuta kwamba biashara haina wateja.

Hii ni hali ambayo inaumiza sana hasa pale ambapo umejipanga kwa muda mrefu kuingia kwenye biashara husika.

Hata kama upo kwenye biashara na umeona unaweza kuongeza biashara nyingine au bidhaa nyingine au huduma nyingine, inaumiza sana pale unapotoa kile kipya halafu unagundua wateja hakuna.

Ili kuepuka maumivu haya na ili kuhakikisha unaanza biashara ambayo unaweza kuisukuma, chagua wateja kabla hujaanza biashara au hujaanzisha kitu kipya.

Hii ina maana kwamba wakati unaanza tayari kwenye mawazo na mipango yako unajua unawalenga watu fulani. Na kwa kujua watu hao itakuwa rahisi kwako kujua unawapata wapi au unawafikia vipi.

Biashara za sasa sio na za zamani kwamba fungua na watu watakuja, badala yake unahitaji kujua nani anayehitaji kile unachotaka kutoa na utampata wapi au utamfikiaje.

Kuwa na wazo la mteja wako, yule ambaye atanufaika na kile unachotoa, kabla hata hujaanza biashara. Itakuwa njia rahisi sana kwako kuikuza biashara yako hata kama mambo yataonekana magumu.

Kila la kheri.

SOMA; Jinsi ya kujua biashara bora kwako kufanya kwa mtaji wowote unaoweza kuanza nao.

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz