Kocha mmoja wa timu ya mpira alikuwa anapata matokeo mazuri sana kwa timu yake. Alikuwa anashinda michezo mingi na wachezaji wake walikuwa wanajituma sana uwanjani. Watu wengi walitaka kujua ni siri gani ambayo kocha yule amekuwa akiitumia na kusababisha timu yake kupata matokeo mazuri kiasi kile.

Baadae iligundulika kwamba kila baada ya mchezo, alikuwa anakaa na timu yake na kuupitia mchezo mzima.

Kama mchezo haukuwa mzuri, yaani timu yake haikufanya vizuri na hivyo kuwa imefungwa alikuwa anawaambia wachezaji wake MIMI nimeshindwa kuwawezesha mfanye vizuri. Hili ni kosa langu na kocha wa timu pinzani amefanya kazi yake vizuri. Sikufanya kazi yangu vizuri ndio maana nyie vijana wangu mmeshindwa.

Kama mchezo ulikuwa wa kawaida, yaani wachezaji wamecheza kawaida na hivyo kupata ushindi mdogo au kutoka suluhu, kocha huyu alikuwa anawaambia SISI tumejitahidi katika mchezo huu, na tunahitaji kuweka juhudi zaidi kwenye mchezo ujao.

Kama timu yake imeibuka na ushindi mkubwa sana, yaani kucheza mchezo bora na kupata ushindi mkubwa, kocha yule alikuwa anawaambia wachezaji wake NYINYI mmecheza vizuri sana leo, mmeweka juhudi kubwa na hatimaye mmepata ushindi mkubwa.

Nafikiri umeona mbadiliko wa hali katika matokeo hayo matatu. Sio kwamba kocha alikuwa akijidharau, ila alikuwa nakubali majukumu yake na anatambua juhudi za wachezaji wake. Ingelikuwa kocha mwingine wakishindwa anawaambia nyinyi mmeshindwa na wakishinda anasema yeye ameshinda.

Tunajifunza nini hapa?

Tuyakubali majukumu yetu, na tuyafanyie kazi. Pale inapotokea kwamba umepata matokeo ambayo hukuyategemea, usijaribu kuyakimbia, usijaribu kutafuta sababu, badala yake tambua kuna kitu hujafanya na amua kukifanya wakati mwingine.

Ukitaka kutafuta sababu kwa nini hujapata matokeo uliyotarajia kupata, utapata sababu nyingi sana, yaani sana na zote zitaonekana ni sahihi. Lakini sababu hizo hazitakutoa hapo ulipo, badala yake zitakufanya uzidi kuwa mzembe.

Chukua hatamu ya maisha yako, kubali majukumu yako, na weka juhudi za kutosha. Hayo ndiyo maisha ya mafanikio.

SOMA; Jukumu Lako, Matatizo Yako, Uzembe Wako…

TAMKO LANGU;

Nimeshaamua kushika hatamu ya maisha yangu, najua maisha yangu na kazi/biashara zangu ni jukumu langu. Matokeo yoyote nitakayopata nitayapokea na kuchukua hatua kama siyo matokeo niliyotegemea. Sitatafuta sababu za kwa nini nimeshindwa, badala yake nitatafuta sababu kwa nini nishinde wakati mwingine.

NENO LA LEO.

You must take personal responsibility. You cannot change the circumstances, the seasons, or the wind, but you can change yourself. That is something you have charge of. – Jim Rohn

Ni lazima uchukue jukumu la maisha yako. huwezi kubadili hali, huwezi kubadili majira, huwezi kubadili upepo, ila unaweza kujibadili wewe mwenyewe. Hiko ni kitu ambacho unakimiliki wewe.

Shika hatamu ya maisha yako, na jua chochote kinachotokea ni juu yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.