Moja ya vitu ambavyo huwa nawashauri watu kwenye biashara na hata maisha ya kawaida ni kutokushindana. Ndiyo sisi binadamu tunapenda ushindani, lakini kushindana kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida huwa sio kuzuri.
Sasa kama umeamua kutokushindana lakini ukaanzisha biashara kwa ubunifu wako mwenyewe na ukashangaa baada ya biashara kuonesha mafanikio, wakaja watu wengine na kuiga biashara unayofanya? Sasa hapa unafanyaje? Unawaacha waendelee tu au unashindana nao? Najua hatua ya kwanza ni kutaka kushindana, lakini hilo litakupoteza.
Kabla hujakimbilia kushindana ni lazima ujue jambo hili moja muhimu, kama kua watu wameiga biashara yako na wanapata wateja wengi, basi jua kuna mapungufu ambayo wewe unayo kwenye biashara. Kuna kitu fulani ambacho wateja walikuwa hawakipati kwako na sasa wamepata sehemu ya kukipata, na hivyo lazima waende kule wanakokipata.
Hivyo badala ya kupambana naye, wewe iangalie biashara yako vizuri, angalia ni kitu gani ambacho wateja kwako hawapati lakini wakienda kwingine wanapata. Na ukishajua jukumu lako ni moja, boresha zaidi.
Unajua uboreshaji wa biashara yako ni kitu ambacho kinatakiwa kiwe kinatokea kila siku. Ila unapokuwa mwenyewe ni rahisi kujisahau. Hivyo wanapokuja wengine wanakuamsha na kukumbusha jukumu lako muhimu la kuboresha biashara yako.
Mtu anapoiga biashara yako usikazane kushindana naye ili umshinde, badala yake boresha biashara yako ili uendelee kuikuza zaidi.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,