Tukiangalia kwa undani kabisa, kama utaamua kuweka sababu nyingine zote pembeni ni kwamba kuna kitu kimoja tu kinachokuzuia wewe kuishi yale maisha ambayo unajua unataka kuishi.

Nina uhakika una picha fulani ya maisha ambayo unajua ni bora kwako. Unaona kabisa kama maisha yako yangekuwa hivi basi mambo yangekuwa mazuri. Na unajua pia kwamba hapo ulipo sio unapotaka kuwa kwenye maisha yako. na unajua kabisa unahitaji kuchukua hatua. Na tena unajua ni hatua gani unatakiwa kuchukua.

Lakini sasa……

Huchukui hatua, kila siku unazidi kutamani kufika pale unapotaka kufika lakini hatua huchukui. Na hii yote inasababishwa na kitu kimoja ambacho kipo ndani yako na hakitaondoka leo, hakitaondoka kesho na hakitaondoka milele. Kadiri utakavyoendelea kusubiri usichukue hatua, kadiri kitu hiko kinaendelea kuwepo.

Kitu hiko ni HOFU, na najua tumeshajadili mengi sana kuhusu hofu lakini bado unashindwa kushinda hofu. Hii ni kwa sababu hofu ni sehemu yako, na wala haitakuja iondoke kabisa ndio uwe tayari kufanya kitu, kama hiko ndio unachosubiri rafiki yangu unajipoteza.

Kadiri utakavyokuwa unaishi, hofu itaendelea kuwepo, ni sehemu ya asili ya maisha yako, ambayo imekuwepo kwa lengo zuri la kuhakikisha unajilinda, ila sasa inavuka mstari na kukuzuia kuchukua hatua bora kwenye maisha yako.

Ufanye nini sasa?

Chochote ambacho unataka kwenye maisha yako, anza kukifanyia kazi mara moja. Usikubali kutafuta sababu za kuficha hofu zako. Maana hutazikosa, utakuja na kwamba hupo tayari, kwamba ngoja hiki kipite, ngoja kile kipite, na baadaye uje kusema muda umepita.

Ninakuhakikishia utapata mawazo mengi sana ya kutaka kukurudisha nyuma pale utakapotaka kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yako, je nitaweza, vipi kama nikishindwa, watu watanichukuliaje, si nitapoteza kila kitu, na mengine mengi. Ni muhimu kuzielewa hofu zote ulizonazo kisha kuangalia unaanzia wapi licha ya hofu hizo ulizonazo.

Na anza kufanya, maana dawa pekee ya kuondoa hofu ni kufanya kile ambacho unahofia kufanya.

SOMA; Hofu Nimekuelewa Na Sasa Nasonga Mbele.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba hofu ni sehemu ya maisha yangu, ni kitu ambacho hakiwezi kuondoka chenyewe. Nahitaji kuchukua hatua ya kufanya kile ambacho nahitaji kufanya kwenye maisha yangu licha ya kuwa na hofu. Maana najua njia pekee ya kuondokana na hofu ni kufanya kile ambacho ninahofia kufanya.

NENO LA LEO.

Try a thing you haven’t done three times. Once, to get over the fear of doing it. Twice, to learn how to do it. And a third time to figure out whether you like it or not.

Virgil Thomson

Jaribu mara tatu kitu ambacho hujawahi kufanya. Mara ya kwanza kuondoa hofu ya kukifanya. Mara ya pili kujifunza jinsi ya kukifanya. Na mara ya tatu kujua kama unapenda kukifanya au la.

Hofu ni kitu ambacho kinaweza kukuzuia kuishi maisha unayotaka, lakini utakapoanza kufanya vile unavyohofia, hofu inakimbia yenyewe.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.