Linapokuja swala la kuongeza mauzo na kukuza biashara, wafanyabiashara wengi huangalia eneo moja rahisi, kupunguza bei, au kuuza bei rahisi kuliko wengine. Hii inaweza kuonekana kufanya kazi kwa muda lakini baadaye itakuumiza, hasa kama utakuwa ndio bei nafuu kuliko wengine wote.

Kama lengo lako ni kutengeneza biashara itakayokua na kudumu kwa muda mrefu, usikimbilie kuwa wa bei nafuu kuliko wengine wote. Hapa nakupa sababu chache kwa nini usifanye hivyo.

1. Kisaikolojia watu wanahusisha nafuu na ubora mdogo. Watu wengi wanajua kitu chochote nafuu ubora wake ni mdogo na kitu chochote ghali ubora wake ni mzuri, lakini huu sio ukweli. Na kwa sababu watu wanaongozwa na hisia, ni vyema nawe ukaenda na hisia hizo. Japo sio lazima uwe ghali sana, lakini usiwe rahisi kuliko wote.

2. Kwa kuwa bei nafuu utashindwa kutoa huduma zilizo bora. Kwa sababu utapata faida ndogo, utaajiri watu wenye uwezo mdogo na watadumaza biashara yako. unapoweka gharama za wastani na kupata faida nzuri unaweza kuendesha kwa ubora wa hali ya juu.

3. Rahisi sana inakaribisha wateja wasumbufu. Sikuambii uwatenge wateja lakini kama umekuwa kwenye biashara kwa muda umeshaliona hili, wale wateja ambao wanataka bei ndogo sana, mara zote huwa ndio wanakuwa wasumbufu, kulalamika na kutaka zaidi, japo wamelipa kidogo. Hivyo weka bei za wastani ambazo zitawavutia wale wanaohitaji kweli bidhaa au huduma unayotoa.

Usifanye biashara yako kuwa ndiyo ya bei nafuu kuliko zote, utapoteza wateja wengi wazuri ambao wataona biashara yako siyo ya ubora.

Kila la kheri.

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz